IMEWEKWA DESEMBA 17,2013 SAA 2:15.
Na Oscar Assenga,Tanga.
Na Oscar Assenga,Tanga.
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (MNEC)
wilaya ya Tanga,Salim Kassim Kisauji amesema maisha bora kwa kila mtanzania
yataenda na ufanyaji wa kazi na sio kukaa vibarazani kwa kupiga soga.
Kisauji ambaye pia ni Meya wa zamani wa Jiji la Tanga alitoa
kauli hiyo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata
ya Ngamiani kusini ikiwa ni ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana
Mkoa wa Tanga(UVCCM) Abdi Makange wilayani hapa ulioendana sambamba na ufunguzi
wa matawi.
Kisauji alisema watanzania wengi wamejijengea mazoea ya kuacha
kufanya kazi kwa bidii badala yake wamekuwa wakitumia muda mwingi kukaa
vijiweni na kusema wanamaisha magumu huku wakiacha kutumia vema fursa zilizopo
ili kuweza kujipatia maendeleo.
Alisema kutokana na hali hiyo vijana wengi wameacha kufanya
kazi na kugeuka kuwa omba omba kitendo ambacho ni hatari kubwa sana hasa katika
mustakabali wao na jamii zinazowazunguka.
“Mara nyingi
mnadanganyika kwa kuambiwa vijana mnatekelezwa sio kweli tokeni sasa fanyeni
kazi kwa bidii na matunda yake mtayaona lakini kama
mkiendelea kukaa vijiweni kila siku maisha yatakuwa magumu kwenu “Alisema Kisauji.
Aidha aliwataka wazazi na walezi mkoani hapa kuwahimiza
vijana wao kuacha kukaa mitaani badala yake watoke wakafanye kazi ili waweze
kujiongezea pato ambalo litasaidia jamii zao kujikwamua kimaisha.
Akizungumzia suala la watendaji wa wazembe,Kisauji alisema
dawa yao iko jikoni kwa kuhakikisha wanawashughulikia ipasavyo lengo likiwa ni
kuwa na watendaji wenye kujua wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa wananchi na
sio vyenginevyo.
Aidha aliwataka madiwani kuhakikisha wanalisimamia
kikamilifu suala la mikopo ya vijana na wakina mama asilimia 10 inayotokana na
makusanyo ya halmashauri kila mwezi ili yaweze kufika kwa walengwa
waliokusudiwa.
EmoticonEmoticon