Na Elizabeth Kilindi,Kilindi.
MVUTANO unaoashiria mapigano na mauaji kwa mara nyingine tena unafukuta baina ya wakulima na wafugaji Wilayani Kilindi Mkoani Tanga baada ya wafugaji kuchoshwa na matukio ya kikatili ya mifugo yao kuuawa kwa kuwekewa sumu kwenye malisho na kufia porini.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi katika kitongoji cha Kipaluke, Kijiji cha Kigwama, Kata ya Msanja Tarafa ya Mswaki Wilayani Kilindi ambako ng'ombe nane walifia porini kati ya 14 waliyodaiwa kula majani yenye sumu.
Wakizungumzia tukio hilo la kinyama, jamii ya wafugaji walilalamikia kuchoshwa na maisha ya kunyanyaswa na kufanyiwa vitendo vya ukiukwaji wa haki na wakulima ambao wanalindwa na kupewa baraka na baadhi ya viongozi.
Wilaya
ya Kilindi imekuwa ikikabiliwa na machafuko ya mara kwa mara na
kusababisha vifo na majeruhi kwa kile kilichokuwa kikielezwa kuwa ni
viongozi kutokuwa na tahadhari ya kushughulikia migogoro mapema hadi
yanapotokea maafa.
Wakizungumza
katika mkutano wa dharula wa wafugaji hao wa jamii ya kimasai
uliyofanyika jana katika kitongoji cha Kipaluke,wafugaji hao wakiongozwa
na Philipo Ngakuru mwenyekiti wa serikali ya kitongoji cha Kipaluke na Marko Issaya kiongozi wa kijadi wa jamii hiyo (Raigwanani), walisema hali ilipofikia watalazimika kuingia msituni kufanya vita.
katika mkutano huo viongozi hao walichukua jukumu la kuzuia machafuko hayo wakiaahidi jamii hiyo kwamba watafuatilia ngazi za juu za serikali ili kupatiwa ufumbuzi wa matukio hayo na hatimaye haki itendeke kwa njia ya amani ambayo ni utamaduni wa taifa letu.
Wakati wakizungumza
kwenye mkutano huo walidai kuwa tatizo lao na wakulima linastawishwa na
vyombo husika kushindwa kusimamia makubaliano ya kisheria juu ya
matumizi halali ya eneo lenye mgogoro na kwamba hata pale wanapoomba
serikali kuingilia kati hakuna kinachotendeka.
Naye
Thomas Tinno aliitaka serikali kutokaa kimya na badala yake itoe tamko
kuhusiana na kitendo cha kumwagwa sugu kwenye malisho ya wanyama na
kusababisha vifo na kueleza kuwa kufanya hivyo kutazuia maamuzi ya hasira ya kulipa kisasi yanayoweza kuchukuliwa na wahanga.
“Mimi
naiomba serikali kupitia nyinyi waandishi wa habari ichukue hatua kwani
waliyohusika na tukio hili wanafahamika isingoje wahanga wachukue
hatua, kwani kukaa kimya itakuwa imebariki machafuko” alisema Tinno.
Abraham Ngakuru alisema
kuwa kutokana na tukio hili, jamii ya wafugaji imetangaza mgogoro na
kwamba kama si busara za viongozi wao wa kijadi amani ingetoweka tangu
pale serikali ilipojidhihirisha kusimama na kutetea upande mmoja wa
wakulima hao.
Aidha Paulo Sinion alidai kuwa siku ya tukio majira ya saa tisa jioni walipata taarifa kutoka kwa mchungaji kuwa ng’ombe zinaanguka na walipofika walizikuta 14 zikigaagaa chini na kwamba sita zilinusurika kufa baada ya kupewa maziwa na sukari ambapo nane kati ya hizo zilikufa hapohapo.
Akitoa tamko
la mkutano huo, Philipo ambaye ni mwenyekiti wa serikali ya Kitongoji
hicho, alisema kuwa tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji limekuwa
sugu na kueleza bayana kuwa unachochewa na uongozi wa Kata na baadhi ya
serikali za vijiji.
Kwamujibu wa Philipo ni kuwa viongozi
wa Kata kwa kushirikiana na wa vijiji wamekuwa na utamaduni wa
kuwanyanyasa wafugaji kwa vitendo mbalimbali kama vile kuunda kikundi
cha vijana kwa ajili ya kuhujumu mifugo yao.
Alisema kuwa kutokana
na hali ilivyo ni lazima serikali ya Wilaya na Mkoa iingilie kati
kukomesha unyanyasaji huo unaofanywa kwa lengo la kuwanufaisha wachache
ili kuzuia vurugu zinazoweza kutokea katika maeneo hayo.
Alishangaa
uongozi wa Kata kutolishughulikia tatizo hilo kwa madai kuwa lipo wazi
kwani sehemu yenye mgogoro inayotumiwa kwa ufugaji ilitengwa na serikali tangu mwaka 1998 kuwa eneo la malisho na kuhoji sababu za kutoheshimiwa.
Kiongozi wa jamii hiyo, Raigwanani Issaya yeye alikitaka Chama cha Mapinduzim CCM kuingilia kati mgogoro huo kwani wafugaji hao wananyanyashwa na watendaji wake na hawapati haki licha ya kuwa ni wafuasi wa Chama hicho.
Aidha
alienda mbali zaidi kwa kukitaka Chama hicho kumshauri Mkurugenzi wa
halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kumuondoa afisa mtendaji wa Kata ya
Msanja akieleza kuwa ni mzigo na chanzo cha unyanyasaji ndani ya Kata
hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Seleman Liwowa alidai
hakuwa na taarifa ya tukio hilo na kuahidi kufuatilia ili kubaini na
kuchukua hatua zinazostahili na kwamba ni kosa la jinai kwa mtu kutumia
vibaya madaraka yake jambo ambalo pia ni kinyume na uwepo wa kiongozi
husika.
“Hapana
Mimi sina taarifa hizo ndiyo unanambia sasa hivi, japo kuwa sipo
Wilayani, nipo Mtwara…..nitawasiliana na (OCD) Mkuu wa polisi Wilaya
afuatilie kwa kuwa wewe unanieleza tofauti na taarifa nilizokuwa
nazo” Liwowa alisema.