SIKU Chache baada ya Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo Taifa (Chadema) kuamua kumvua uongozi ndani ya chama hicho aliyekuwa
katibu Msaidizi Zitto Kabwe chama hicho mkoani hapa kimeipongeza hatua hiyo kwa
kusema italeta umakini mkubwa kwa viongozi waliobaki.
Uamuzi huo ulitolewa kwa mujibu ibara ya 7.7.16 kifungu (V) ambayo
inaeleza kuwa kamati hiyo ina mamlaka ya kumwachisha ujumbe wa kamati kuu
mjumbe mteule ambaye ataenda kinyume cha katiba, kanuni na maadili au kushindwa
kukidhi matakwa ya kuteuliwa kwake.
Akizungumza na Tanga Raha,Katibu wa Chadema Mkoa wa Tanga,Jonathan
Bahweje alisema suala hilo lilipaswa kufanywa na kamati hiyo kwa sababu ni
sahihi kwa mtu yoyote anayekiuka kanuni na taratibu za uongozi ndani ya chama
hicho.
Bahweje alisema hatua ya Zitto kukiri kuwa alikosea na
kupewa adhabu ya siku kumi na nne kujitetea kwa kamati kuu ya chama hicho
alitumia busara kubwa sana
na kuwataka wanachama kuwa na utulivu wakati mchakato huo ukiendelea.
“Maamuzi ya kamati
kuu yaliyofanywa sidhani kama yanaweza kuingiliwa na upande mwengine hivyo
napenda kuwaasa viongozi wa ngazi za chini kuacha kuingilia suala hilo kwani tayari
limeshapata muafaka “Alisema Bahweje.
Alisema wanaiomba kamati kuu ya chama hicho kumaliza mgogoro
uliopo huo mapema ili kuweza kujiandaa na uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa
mwaka 2014 kwani wamedhamiri kuhakikisha
wanashinda katika chaguzi hizo.
Katibu huyo aliitaka kamati hiyo kukemea viongozi ambao
wanapiga maamuzi yao
kwani wao ndio chombo cha mwisho ambacho kinauwezo wa kufanya jambo lolote
ambalo linaweza kuleta mgawanyiko ndani ya chama hicho.
“Naishauri kamati
kutumia nafasi yao
kuwaonya viongozi kuanzia ngazi za chini na kuweza kuleta mshikamano wa pamoja
ambao utaweza kuleta mafanikio katika chama chetu kwani uongozi imara ndio
utakiwezesha kuwatumikia wananchi “Alisema Bahweje
EmoticonEmoticon