WACHEZAJI KIZIMBANI UNITED WATOA YA MOYONI.

November 29, 2013
Na Masanja Mabula -Pemba .

Hatimaye wachezaji na mashabiki wa Klabu ya Kizimbani United wametoa ya moyoni na kusema kuwa sababu zilizopelekea timu hiyo kufanya vibaya kwenye michuano ya ligi kuu Zanzibar ni kuwepo na upendeleo wakati wa upangaji wa timu .

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi , wamesema kuwa tatizo la upangaji wa timu limekuwa ni kikwazo cha kuweza kufanya vizuri ambapo baadhi ya wachezaji wamekuwa wakipangwa kutokana na kuwa na uhusiano wa Kocha pamoja na viongozi wa timu .

Wamesema kuwa licha ya baadhi yao kuwa na viwango  lakini wamekuwa wakikalia benchi , kwa sababu ya kutokuwa na usuhuba na viongozi pamoja na kocha jambo ambalo limeiweka pabaya timu hiyo .

"Unajua kama huna usuhuba na viongozi pamoja na Kocha ,basi utakalia benchi mpaka uchoke , hata kama unakiwango kama Messi na  hii ndiyo iliyopelekea timu kufanya vibaya kwenye michuano ya ligi kuu ya Zanzibar " alieleza mmoja wa wachezaji jina tunalo .

Aidha nao mashabiki wa timu hiyo wamesema kuwa kitendo cha kuchezesha wachezaji wasio na uwezo kunaweza kuleta athari kwa klabu ikiwa ni pamoja na kushuka daraja .

Meneja wa Klabu hiyo Juma Saleh amekanusha taarifa hizo na kusema kuwa mchezaji anaweza kujihakikishia namba kutokana na juhudi yake mazoezini na kwamba suala la upendeleo halipo ndani ya klabu hiyo .

"Kocha anaangalia juhudi ya mtu mazoezini , na bidii ya mchezaji ndiyo inayomfanya mchezaji ajihakikishie namba kwenye kikosi , lakini suala la viongozi kuwa na wachezaji wao halipo ndani ya klabu yetu " alifahamisha meneja .

 Naye Mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya klabu hiyo Juma Mzee amesema kuwa wachezaji wanaolalamika kutochezeshwa hawana elimu na hawajifahamu nini wanatakiwa wafanye , kwani lengo la viongozi ni kuona kuwa timuinafanya vyema na  inasonga mbele .

"Tatizo la wachezaji wetu hawana elimu pamoja na nidhamu ya mchezo , hili ndio chanzo cha baadhi yao kulalamika kwamba hawapewi nafasi ya kucheza , mimi najua wachezaji wote wamechezeshwa kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo  " alifahamisha .

Timu ya soka ya Kizimbani United kwa sasa inaendelea na mazoezi ikiwinda na michuano ya super 8 baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Zanzibar na kuambulia alama 8 katika mechi kumi na moja ilizocheza .

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »