Na Oscar Assenga, Tanga.
MBUNGE wa Jimbo la Tanga, Omari Nundu amewataka waislamu
mkoani kuendelea kudumisha amani iliyopo hapa nchini pamoja na kuilinda kwa
kufanya mambo mema yanayompendeza mwenyezi mungu ikiwemo kuacha kufanya yale
yote yaliyokatazwa.
Nundu alitoa kauli hiyo wakati akitoa hotuba yake
kwenye baraza la Iddi lililofanyika ukumbi wa shule ya sekondari Jumuiya mkoani
Tanga ambalo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini akiwemo Meya wa Jiji la Tanga Omari Guledi
ambapo alisema waislamu hawana budi kuendelea kutenda mema ili kuweza kupata
dhawabu.
Alisema waislamu wanapaswa kuwa na tahadhari kwa kuepuka
kuwa na vikundi ambavyo vinalenga kuleta chokochoko ya kidini kwenye jamii
zinazowazunguka kwani kufanya hivyo kunapelekea uvunjifu wa amani badala yake
waishi kwa kutii na kuheshimu sheria zilizopo hapa nchini.
Mbunge huyo alitumia nafasi hiyo kuwaasa waislamu kutilia
mkazo elimu ya dunia kwa sababu ugunduzi mwingi unaotumika hivi sasa umeelemea
sana kwenye maandiko yatokanayo na kuruhan hivyo kuwataka kuzingatia suala hilo
kiumakini.
“Ndugu zangu
waislamu wenzangu tumemaliza mwenye mtukufu wa ramadhani kwa amani,basi
nawashauri tuendeleze sifa tulizokuwa nazo kwenye mwezi huo kwa kuacha kufanya
maovu badala yake tuelekeze nguvu zetu kwenye kutenda mambo mema “Alisema Nundu.
Aidha aliwataka kuepuka mivurugano ambayo haina tija kwenye
jamii zao kwa kuishi kwa amani ikiwamo kushirikiana na watu wengine malengo yakiwa ni kutimiza
nguzo kuu ya uislamu ya kufanya ibada mara kwa mara ili kuweza kuwa karibu na
mwenyezi mungu.
Awali akizungumza katika baraza hilo,Sheikh wa Mkoa wa
Tanga,Ally Juma Luwuchu alisisitiza suala la waislamu kuendelea kutenda mambo
mema ikiwemo kuendelea kuonyesha ustawi
mzuri kwa jamii kitu kitakachopolekea kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kujenga
umoja ulio imara katika uislamu hapa nchini
Sheikh Luwuchu aliwaomba waslam kuondoa tofauti zao za kiimani na wawe
wamoja , wasikivu kwa viongozi wao wakuu
wa kidini hasa inapofikia wakati wa kupata tamko kutoka kwa viongozi hao kitu
kitakachowapelekea kuonyesha umoja wetu na mshikamano katika maswala yote
yanayohusu uislam.
EmoticonEmoticon