Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Ligi ya Mabingwa wa
Mikoa kutafuta timu tatu zitakazopanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza(FDL) msimu
ujao chini ya usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itaanza
Mei 12 mwaka huu.
Mwisho wa mikoa kuwasilisha majina ya mabingwa wao ni
Mei 1 mwaka huu wakati ratiba ya ligi hiyo itapangwa mbele ya waandishi wa
habari Mei 3 mwaka huu kwenye ofisi za TFF.
Uwasilishaji wa jina la bingwa wa mkoa unatakiwa
kufanyika pamoja na ulipaji ada ya ushiriki ambayo ni sh. 100,000. Mfumo wa ligi
hiyo ni bingwa wa mkoa X kucheza na bingwa wa mkoa Y nyumbani na ugenini ambapo
mshindi ndiye anayesonga mbele katika hatua inayofuata.
Usajili wa wachezaji wa timu hizo ni uleule uliofanyika
katika hatua ya mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa ajili ya uthibitisho. TFF
inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa wachezaji kwa ajili ya ligi
hiyo.
Mwisho.
KILA LA KHERI AZAM FC
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia
kila la kheri timu ya Azam FC katika mechi yake ya kwanza ya raundi ya pili ya
Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco itakayochezwa kesho (Aprili
20 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili
jioni.
Azam FC ina fursa nzuri ya kufanya vizuri kwenye mechi
hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Emile Fred kutoka Shelisheli kutokana na
maandalizi iliyofanya, lakini vilevile tunatoa mwito kwa Watanzania kujitokeza
kwa wingi uwanjani kuiunga mkono.
Makocha wasaidizi wa timu zote mbili, Kalimangonga Ongala wa Azam na Lahcen Ouadani wa AS FAR Rabat wamezungumza na waandishi wa habari kuhusu mechi hiyo, kuwa wamejiandaa kuibuka na ushindi.
Kocha Ongala amesema wamepata DVD za mechi tatu za
mwisho za AS FAR Rabat, moja ikiwa dhidi ya timu ya Al Nasir ya Libya ambayo
waliitoa katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho na nyingine mbili za
ligi ya Morocco ambazo wanazifanyia kazi kuhakikisha wanashinda
kesho.
Naye Ouadani amesema hawaifahamu vizuri Azam, lakini
wanaujua mpira wa Tanzania baada ya kuangalia mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia
kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas) iliyochezwa
jijini Dar es Salaam Machi 24 mwaka huu na Stars kushinda mabao 3-1.
Baadhi ya wachezaji ambao Azam inatarajia kuwatumia
kwenye mechi ya kesho ni pamoja na Aishi Manula, Mwadini Ally, Khamis Mcha, John
Bocco na Salum Abubakar ambao pia wamo kwenye kikosi cha sasa cha Taifa Stars
kilicho chini ya kocha Kim Poulsen.
AS FAR Rabat ina wachezaji sita kwenye timu ya Taifa ya Morocco. Wachezaji hao ni mabeki Younes Bellakhdar, Abderrahim Achchakir, Younnes Hammal, na viungo Salaheddine Said, Salaheddine Aqqal na Youssef Kaddioui.
EmoticonEmoticon