TIMU 13 kushiriki ligi ya Mkoa wa Tanga"

March 08, 2013
Na Mwandishi Wetu, Tanga.
JUMLA ya timu 13 zimefunzu kucheza Ligi ya Mkoa wa Tanga mzunguko wa pili baada ya kufanya vizuri mzunguko wa kwanza na itachezwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini.

Akizungumza na Blogi hii Katibu wa chama cha soka Mkoa wa Tanga (TRFA), Beatrice Mgaya alisema maandalizi ya hatua hiyo yamekamilika na mzunguko huo utaanza Machi 9 mwaka huu.

Mgaya alisema katika ufunguzi wa mzunguko huo, timu za soka Lushoto Shooting na Korogwe United zinatarajiwa kuonyeshana kazi katika uwanja wa soka Lushoto na unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa.

Alisema mchezo mwengine utakaochezwa siku hiyo utafanyika kwenye uwanja wa Mkwakwani ambapo timu ya maafande wa jeshi la magereza mkoani hapa Small Prison watakapoikabili Viva Dynamo ya Maramba wilayani Mkinga.

Katibu huyo alizitaka timu zinazoshiriki ligi hiyo kuonyesha nidhamu ya hali ya juu ili kuweza kuleta ushindani pamoja na kuziasa zifanye maandalizi ya kutosha kabla ya mechi zao.

Mgaya alizitaja timu zinazoshiriki kuwa ni Lushoto Shooting, Korogwe United,Halmashauri Fc,Lushoto Star,Small Prison,Viva Dynamo, ,Veteran FC,Monga Star,African Sports,Black Burn,Eagle Rangers na Moa Original na Makorora Star.

Timu hizo zitachukuana ili kuweza kupatikana bingwa wa mkoa katika msimu huu ambapo ataweza kushiriki mashindano ya mabingwa wa mikoa itakayochezwa baada ya kumalizika ligi za mikoa.

Mwisho.

"Bondo United watwaa ubingwa wa Kombe la Diwani Handeni"
 
Na Mwandishi Wetu,Handeni

LIGI ya soka kuwania kombe la Diwani kata ya Kwamgwe wilayani hapa,juzi ilifikia tamati kwa mchezo kati ya Bondo United na Mungano FC ambapo matokeo ya mchezo huo Bondo ilitwaa ubingwa kwa njia ya penati kwa kuwanyuka wapinzani wao kwa 3 - 0.

Katika mchezo huo wa fainali uliofanyika uwanja wa Kwedigongo hadi muda wa kawaida unamaizika hakuna mbabe ambapo mwamuzi wa mchezo huo Mohamed Chombo aliongeza muda wa nyongeza dk 15 ambazo pia hazikutoa mshindi hadi hatua ya penati.

Waliofanikiwa kuzikwamisha wavuni penati za Bondo ni Charles Ernest,Hemed Athumani na Hamisi Mohamed wakati ile ya Muungano ilifungwa na mchezaji Enock Juma matokeo ambayo yaliifanya Bondo United kuwa bingwa baada ya penati tano tano kupigwa.

Bingwa wa ligi hiyo ambayo hufanyika kila mwaka aliweza kuzawadiwa kikombe,jezi seti moja na Tsh 100,000, wakati mshindi wa pili timu ya Muungano ilizawadiwa Tsh 70,000 na mshindi wa tatu Tsh 50,000 ambazo zilikwenda jkwa klabu ya soka ya Mbogoni FC.

Mratibu wa mashindano hayo ambaye ni diwani wa kata ya Kwamgwe Sharrifa Abebe akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika alisema,amefurahishwa na wachezaji pamoja na mashabiki wa timu zilizoshiriki kuzingatia suala la nidhamu mchezoni.

Alisema mashindano hayo yameweza kutoa timu ya kata ainayoundwa na wachezaji wapatao 40  ambao watakuwa chini ya mwalimu wao msaidizi aliyemtaja kwa jina la Hamza Manulanula huku jitihada za kumtafuta kocha mkuu zikiendelea kufanywa.

"Nimefurahi ligi kumalizika kwa amani na sasa tunaangalia suala la timu yetu ya kata,mwalimu msaidizi amepatikana...mimi na wafadhili wengine tunasaka kocha mkuu ili kuwanoa vyema vijana wetu,tutakuwa na mechi nyingi za majaribio"alisema Sharrifa.

Alisema,lengo la kuanzishwa ligi hiyo ni kukuza vipaji sanjari na kutengeneza ajira kwa vijana huku akibainisha kuwa kupitia ichezi pia vijana itawasaidia kuepukana na mazingira ambayo yanaweza kuwatumbukiza katika vitendo hatarishi na kuharibu maisha yao.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »