Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
"TFF BADO YASISITIZA KUMUONA WAZIRI MUKANGARA"
RAIS
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
amemshukuru Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela
Mukangara kwa kukubali ombi la Shirikisho la kutaka kukutana naye kwa
mazungumzo na kumsihi asitishe hatua anazodhamiria kuchukua hadi hapo
kikao hicho kitakapofanyika.
Waziri
Mukangara ameiagiza TFF kuitisha Mkutano Mkuu wa marekebisho ya katiba
ifikapo tarehe 15 Aprili 2013 na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi ifikapo tarehe
25 Mei 2013 na kwamba tamko la TFF kutekeleza maagizo hayo liwe
limetolewa katika muda wa siku tano zinazoishia Jumatatu (Machi 11,
2013).
Katika
barua pepe ambayo amemuandikia Waziri ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi,
Rais Tenga ameeleza kuwa alikwenda ofisini kwake tarehe 7 Machi 2013
kujaribu kumuona lakini akaambiwa amesafiri, hivyo kuomba kukutana na
Katibu Mkuu wa Wizara, ambaye pia hakuwepo ofisini na hatimaye akakutana
na Naibu Katibu Mkuu.
Katika
barua hiyo pepe, Rais Tenga ameeleza madhumuni ya kutaka kuonana na
Waziri Mukangara kuwa ni kwanza “kukushukuru kwa kukubali kuonana na
ujumbe wa TFF ulioongozwa na mjumbe wetu wa Kamati ya Utendaji, Bw. Alex
Mgongolwa, akiongozana na Katibu Mkuu wa TFF, Bw. Angetile Osiah, jana
tarehe 6 Machi 2013.
“Kukushukuru kwa kukubali kukutana nasi tena siku ya tarehe 19 Machi, kwa ajili ya mazungumzo juu ya maagizo yako.
“Kukuarifu kuwa nimepokea maagizo yako uliyoyatoa jana kupitia kwa Mjumbe wetu wa Kamati ya Utendaji na kwa njia ya barua; na
“Kwa heshima na taadhima, kukuomba usitishe hatua yoyote ile unayodhamiria kuchukua hadi hapo tutakapokutana na kupata maelezo yetu, TFF, juu ya maamuzi na maagizo uliyoyatoa.”
“Kwa heshima na taadhima, kukuomba usitishe hatua yoyote ile unayodhamiria kuchukua hadi hapo tutakapokutana na kupata maelezo yetu, TFF, juu ya maamuzi na maagizo uliyoyatoa.”
Tenga,
ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
la Afrika (CAF) aliondoka jana (Machi 7 mwaka huu) kwenda Marrakech,
Morocco kuhudhuria kikao cha kamati hiyo na pia Mkutano Mkuu wa CAF
ambao umepangwa kufanyika Machi 10 mwaka huu ukihusisha pia ajenda ya
uchaguzi wa rais.
Mwisho.
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
"KAIJAGE KOCHA MPYA TWIGA STARS"
ROGASIAN
Kaijage ameteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya mpira wa miguu
ya wanawake, Twiga Stars baada ya kocha wa zamani, Charles Boniface
Mkwasa kujiuzulu katikati ya mwaka jana.
Mkwasa,
ambaye alikuwa nyota wa Yanga na Taifa Stars, alijiengua kufundisha
timu hiyo aliyoiongoza kwa muda mrefu, baada ya Twiga Stars kuondolewa
katika kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika
kwa Wanawake (AWC) zilizofanyika nchini Equatorial Guinea.
Twiga
ilipata bao muhimu la ugenini jijini Addis Ababa ilipofungwa na wenyeji
wao Ethiopia mabao 2-1, lakini ikiwa na matumaini ya kutumia vyema bao
la ugenini ilijikuta ikilala bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa katika
mchezo wa marudiano na hivyo kukosa tiketi ya kurudi tena kwenye fainali
hizo.
Kaijage
ambaye kwa sasa anajihusisha na mradi wa vijana (grassroots) pamoja na
programu nyingine za kukuza vipaji zilizo chini ya TFF, aliteuliwa na
Kamati ya Ufundi ya TFF kufanya kazi hiyo na ameita kikosi cha Twiga
Stars kwa mazoezi ya siku kumi kuanzia Machi 10 hadi 23 mwaka huu Uwanja
wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Wachezaji
walioitwa ni Amina Ally (Lord Barden), Asha Rashid (Mburahati Queens),
Aziza Mwadini (Zanzibar), Esther Chabruma (Sayari), Esther Mayalla (TSC
Academy), Etoe Mlenzi (JKT), Evelyn Sekikubo (Mbarahati Queens), Fatuma
Bushiri (Simba Queens), Fatuma Mustafa (Sayari) na Fatuma Omari
(Sayari).
Flora
Kayanda (Tanzanite), Hamisa Athuman (Marsh Academy), Hellen Maduka
(Bujora), Hellen Peter (JKT), Irene Ndibalema (TSC Academy), Maimuna
Said (JKT), Mwajuma Abdallah (Tanzanite), Mwanaidi Tamba (Mburahati
Queens), Mwanahamis Omari (Mburahati Queens) na Mwapewa Mtumwa (Sayari).
Nabila
Ahmed (Marsh Academy), Nasiria Hashim (Zanzibar), Pulkeria Charaji
(Sayari), Rukia Khamis (Sayari), Semeni Abeid (Tanzanite), Sharida
Boniface (Makongo Sekondari), Sophia Mwasikili (Luleburgaz Gucu Spor,
Uturuki), Theresa Yona (TSC Academy), Vumilia Maarifa (Evergreen) na
Zena Khamis (Mburahati Queens).
Mwisho.
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
"YANGA, TOTO AFRICANS KUUMANA DAR"
MICHUANO
ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea
kesho (Machi 9 mwaka huu) kwa mechi mbili ambapo vinara Yanga watakuwa
wenyeji wa Toto Africans kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwamuzi
wa mechi hiyo namba 135 atakuwa Andrew Shamba kutoka Pwani akisaidiwa
na Abdallah Mkomwa na Abdallah Rashid pia wote kutoka Pwani. Kamishna ni
Salim Singano kutoka Tanga wakati Mtathmini wa waamuzi ni Alfred Lwiza.
Nayo
Polisi Morogoro itakuwa mgeni wa Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex
ulioko Chamazi, Dar es Salaam. Azam katika mechi hiyo namba 136 na
nyingine mbili zinazofuata itakuwa bila kocha wake Steward John Hall
ambaye Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
imemfungia mechi tatu.
Charles
Komba kutoka Dodoma ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo namba 136
itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka mkoani Pwani.
Ligi
hiyo itaendelea tena keshokutwa (Machi 10 mwaka huu) ambapo Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam utashuhudia mechi kati ya Simba na Coastal Union ya
Tanga. Waamuzi wa mechi hiyo ni Martin Saanya akisaidiwa na Jesse
Erasmo na Vicent Mlabu wote kutoka Morogoro.
Mwisho.
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
"RHINO, KANEMBWA ZASAKA TIKETI VPL"
KINDUMBWENDUMBWE
cha Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kinaendelea kesho (Machi 9 mwaka huu)
katika makundi yote matatu, lakini macho na masikio ya washabiki wa
mpira wa miguu yakiwa kwenye mechi za Rhino Rangers ya Tabora na
Kanembwa JKT ya Kigoma.
Timu
hizo ndizo ziko katika nafasi nzuri ya kupata tiketi ya kucheza Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao kutoka kundi hilo la C. Tayari Mbeya
City ya Mbeya na Ashanti United ya Dar es Salaam zimeshapata tiketi za
kucheza VPL msimu ujao kutoka kundi A na B.
Rhino
Rangers itaikaribisha Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi
mjini Tabora, wakati Kanembwa JKT itakuwa mgeni wa Pamba kwenye Uwanja
wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mechi
nyingine za kundi C ni Mwadui vs Polisi Tabora (Kambarage, Shinyanga),
na Morani vs Polisi Mara (Kiteto, Manyara). Mechi za kundi A ni Majimaji
vs JKT Mlale (Majimaji, Songea), Mkamba Rangers vs Mbeya City (Sokoine,
Mbeya) na Polisi Iringa vs Burkina Faso (Samora, Iringa).
Mshikeshike
ya kundi B ni Ndanda vs Ashanti United (Nangwanda Sijaona, Mtwara),
Villa Squad vs Green Warriors (Karume, Dar es Salaam), Polisi Dar vs
Transit Camp (Mabatini, Mlandizi) wakati Tessema na Moro United
zitacheza Machi 10 mwaka huu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Mwisho.
EmoticonEmoticon