“Lushoto waunga mkono Agiza la RC Gallawa”

March 06, 2013
Na Oscar Assenga, Lushoto.
WANANCHI wa wilaya ya Lushoto wameunga mkono Agizo la Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Luteni Mstaafu Chiku Gallawa la kufanya usafi katika maeneo yao kila Jumammosi ya kwanza ya mwezi kwa kuchagua maeneo korofi kwa kufanya usafi wa pamoja.

Mwishoni mwa mwezi uliopita Mwandishi wa blog hiii aliweza kupita maeneo mbalimbali wilayani humo nyakati za asubuhi na kujionea maduka yakiwa yamefungwa huku umati mkubwa wa wananchi wakiwa katika maeneo yao kwa ajili ya kushiriki katika zoezi la usafi.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa zoezi hilo,Mkazi wa Lushoto mjini,Philipo Katemba alisema zoezi hilo la usafi wamelipokea kwa mikono miwili na kueleza kuwa endapo wananchi watashirikiana kwa pamoja kila wakati basi upo uwezekano mkubwa wilaya yao kushika nafasi ya kwanza katika usafi mkoani hapa kutokana na mwamko wa wananchi kijitokeza kushiriki.

Katemba ambaye pia ni mfanyabishara wilayani humo, aliongeza kuwa zoezi la usafi lilianza muda mrefu lakini wakati huu ndio limetiliwa mkazi zaidi ambapo wananchi wameweza kuhamasika zaidi kwa kujitokeza kwa wingi kuliko ilivyokuwa huku nyuma.

Naye Katibu wa Baraza la Biashara wilayani Lushoto (BBW) David Mkami alisema mchakati huo wa usafi ni mzuri kwa kuwa unaufanya mji wao katika hali ya usafi na kuwa na muonekano mzuri zaidi na kuwataka wafanyabishara kuendelea kuunga mkono agizo hilo katika maeneo yao ya kazi.

Mwisho.
DC Mwanga "awataka Vijana kupenda soka"

Na Oscar Assenga, Lushoto.

MKUU wa wilaya ya Lushoto,Alhaji Majid Mwanga amewataka vijana kupenda michezo na kuithamini kwa kuwa michezo ni ajira ambayo inaweza kuwainua kimaisha endapo wataithamini na kuipa kipaumbele kwa kucheza kwa kujituma pamoja na kuonyesha nidhamu wakati wa michezo.

Alhaji Mwanga alitoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati fainali ya Mashindano ya Kombe la Shambalai Cup yaliyofanyika kwenye uwanja wa soka Moa Mwangoi wilayani humo na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa soka wilayani humo akiwemo mdhamini wake Abasi Shambalai.

Alisema michezo mara nyingi huwakinga vijana kujiingiza katika makundi mabaya katika jamii zinazowazunguka pamoja na kuwaepusha kutumia madawa ya kulevya ikiwemo bangi hivyo kuwata vijana kupenda kushiriki katika michezo na kuacha utumiaji wa madawa ya kulevya.

  “Wilaya yetu haipo salama kutokana na kuwepo watu ambao wanaendesha kilimo cha bangi hivyo kupitia mashindano mbalimbali ya mpira miguu wilayani tuwe tunapiga vita matumizi ya madawa ya kulevya “Alisema Mwanga.

Aidha DC Mwanga alisema mashindano hayo yawe chachu kubwa ya wafadhili wengine kujitokeza ili kuweza kuinua kiwango cha soka wilayani humo pamoja na kuhamasisha michezo wilayani humo.

Alieleza endapo suala hilo litatiliwa mkazo mkubwa upo uwezekano wa wilaya hiyo kuwa na timu ambayo itaweza kuja kushiriki ligi daraja la kwanza ikiwemo ligi kuu siku zijazo.

Pamoja na hayo Mkuu huyo wa wilaya alisifu jitihada za waandaaji wa mashindano hayo na kueleza malengo hasa kombe hili yaliyokusudiwa yamefanikiwa kwa asilimia kubwa kutokana na vijana wengi kuhamasika kushiriki.

Katika fainali hiyo,Timu ya Mlalo City waliweza kuibuka kuwa mabingwa wapya wa mashindano hayo na kukabidhiwa Kombe la Mashindano hayo pamoja na kitita cha sh.500,000 jezi na mpira kutoka kwa mdhamini wa mashindano hayo,mshindi wa pili ,alipata kitita cha sh.200,000 na jezi,mshindi wa tatu,Kwemshasha alipewa kitita cha sh.200,000 na mpira na mshindi wa nne,Manyigu Fc alipata 100,000.

Lakini pia washindi wengine waliozawadiwa ni katika awamu ya nane bora ambapo mshindi wa kwanza alipewa kitita cha sh.100, 000 jezi na mpira mmoja, mshindi wa pili alipewa kitita cha sh.50, 000 jezi na mpira na mshindi wa tatu alipewa jezi seti na mpira na kitita cha sh.25,000.

Aidha Mratibu wa Kombe hilo, Fineas Gabriel Mashombela alisema mashindano hayo yalishirikisha timu zaidi ya 50 kutoka maeneo mbalimbali wilayani humo na lengo lake lilikuwa ni kuinua vipaji vya wachezaji wachanga.

                             Mwisho.  

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »