MJUMITA -Wizara ya maliasili inawalinda mabwana Afya wasio waadilifu"

March 06, 2013
Na Oscar Assenga,Korogwe. 

MTANDAO wa jamii usimamizi wa hifadhi ya mazingira ya misitu (MJUMITA) umeishukia wizara ya mali asili na utalii kwa kusema kuwa imekuwa ikiwalinda mabwana miti wasio waadilifu wanaojihusisha na vitendo haramu vya uvunaji wa mazao ya msitu hali inayoweza kusababisha jangwa nchini Tanzania. 

Hivyo kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya watumishi wanaobainika kuhusika uendeshaji hujuma kwenye misitu ya hifadhi, mwenyekiti wa mtandao huo wa jamii Revocatus Njau alisema ni dhahiri kwamba hivi sasa wizara ya mali asili na utalii imepoteza muelekeo wa kusimamia misitu asilia nchini na kubainisha kuwa kila mwaka takribani hekta 130,000 zinapotea kwa miti kukata ovyo ili kuuzwa. 

Mwenyekiti huyo wa Taifa wa mtandao wa MJUMITA,Revocatus Njau alitoa taarifa hiyo juzi kwenye kikao cha ujirani mwema kilichowashirikisha viongozi wa wilaya za Lushoto na Korogwe kilichofanyika mjini Lushoto ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa mkoa wa Tanga Luteni mstaafu Chiku Gallawa.

Akizungumza mbele ya wajumbe wa mkutano huo,Njau alisema kushamiri kwa vitendo haramu vya uvunaji wa mazao ya misitu vinaonekana kupata Baraka ya wizara husika kwa vile mpaka sasa licha ya shughuli ya kuwa na taarifa za uvunaji haramu kuenea kwa kasi hakuna hatu zilizochukuliwa. 

Alisema kuwa MJUMITA kwa upande wake imeshaifahamisha wizara na mamlka nyingine juu ya matukio ya uhalifu yanavyoendelea katika misitu mbalimbali hapa nchini vitendo ambavyo vikiachiwa kuendelea bila hatua za makusudi na moyo wa uzalendo kuwepo basi ni dhahiri kuwa jangwa linaweza kujitokeza. 

Njau alikwenda mbali zaidi akisema hivi sasa inaonekana kuwa kuanzia wizarani umeundwa mtandao wa kuwalinda mabwana miti wanaojihusisha na uvunaji haramu wa misitu vitendo ambavyo alivyovitolea mifano kwenye mkutano huo ambavyo viliwasikitisha na kuwashangaza wajumbe wa mkutano huo. 

Katika kudhibitisha hilo Njau alisema,wakati jitihada mbalimbali zinafanyika kuwadhibiti wahalifu hao viongozi wakuu huchukua hatua ya kuwasaidia kujinanusua na makosa waliyoyafanya ambapo alitolea mfano wa bwana miti mmoja wa wilayani Lushoto aliyefungwa jela na kutolewa akirejeshwa kazini. 

Njau alisema kwamba bwana miti huyo Shabani Kanju mwaka 2008 alifungwa baada ya kubainika kuwa na makosa ya kukata miti asilia lakini cha kushangaza afisa hifadhi wa wilaya ya Lushoto alikwenda kukata rufaa ambapo mfungwa huyo alitolewaa gerezani kwa kuonekana kuwa hakuwa na hatia. 

Aliongeza kusema kuwa hivi sasa bwana miti huyo Shabani Kanju amehamishia makazi yake kwa kujenga nyumba anayoishi na familia yake jirani na msitu wa Kisima Gonja ambako kila uchao magogo,mbao na miti ya aina mbalimbali imekuwa ikivunwa bila huruma bila ya wahusika kukamatwa huku yeye akiwepo.

 “Kwa kweli inasikitisha inavyoonekana mheshimiwa mkuu wa mkoa kuna mtandao ulioanzia wizarani ambao unawalinda mabwana miti wanaokata miti inayohifadhiwa,mazingira mengi yanaeleza hivyo kwa vile wizara tumeipa taarifa kwa maandishi na hata kukaa nao ana kwa ana,hakuna kinachofanyika”alisema Njau akimuomba mkuu wa mkoa wa Tanga kusaidia kunusuru misitu ya Tanga.

 Ili kuweza kuinusuru misitu ya hifadhi hapa nchini Njau alisema iko haja kwa wizara kuona umuhimu wa kuzishirikisha kada nyingine katika dhana nzima ya ulinzi akibainisha kuwa hivi sasa mabwana miti kutoka halmashauri wanaonekana kutoshirikishwa hali inayochangia uhalifu kuongezeka kwa kasi. Mwenyekiti huyo wa MJUMITA alibainisha kuwa mpaka sasa athari kubwa ya mazingira zimeanza kujitokeza katika maeneo mbalimbali nchini akiyataja baadhi yake kuwa ni misitu ya Nguru kusini (Mor),Mamiowa (Kilosa Mor),Oldzungwa (Mor),Ruvu kusini (Pwani) na wilaya za Korogwe na Lushoto. 

Naye meneja mradi wa shirikal la kuhifadhi misitu asilia Simon Lugazo katika mada aliyoitoa kwenye mkutano huo wa ujirani mwema alisema kuwa shirika lake limefanikiwa kusambaza huduma ya maji kwenye maeneo mbalimbali ,usimamizi shirikishi wa misitu na kuandaa mipango ya usimamizi wa upandaji miti lengo likiwa kuhifadhi mazingira na kati ya 1999 hadi 2002 wamepanda miti 2 mil. 

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Tanga Luteni mstaafu Chiku Gallawa aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo alielezea masikitiko yake juu ya vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyoendelea kufanyika hapa nchini akisema vikiachiwa kuendelea njaa na jangwa litaweza kujitokeza hivyo amani na utulivu inaweza kujitokeza jambo ambalo siyo jema kujitokeza hapa nchini. 

Kuhusu taarifa ya bwana miti aliyetuhumiwa kujenga nyumba pembeni ya msitu wa hifadhi Luteni mstaafu Gallawa alimuagiza mkuu wa wilaya ya Lushoto Alhaj Majid Mwanga kuhakikisha kwamba anakamatwa mara moja kwa mahojiano juu ya vitendo ambavyo vinadaiwa kuwa na baraka zake. 

Awali akizungumza kabla ya ufungwaji wa mkutano huo mkuu wa wilaya ya Korogwe Mrisho Gambo aliwaasa viongozi wa wilaya ya Lushoto anayopakana nayo kujitahidi kutoruhusu vitendo vya uharibifu wa mazingira havifanyika katika maeneo yaliyo mipakani mwa wilaya zao ambapo alisisitiza akisema hatua za kali za kisheria zitawabana watu wote bila kujali vyeo vyao,itikadi za kisiasa wala dini. 

Kama vile haitoshi naye mkuu wa wilaya ya Lushoto Alhaj Majid Mwanga alitanabaisha kuwa ushirikiano zaidi unahitajika baina ya pande zote mbili kwa kuwashirikisha viongozi wa wilaya za Korogwe na Lushoto katika masuala yote yanayolenga kuongeza tija kwa jamii ambapo alitilia mkazo juu ya kushirikishana kwenye suala la utozaji ushuru wa mazao.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »