DC Mwanga aisifu Lushoto Shooting, “Asema fitna zikiwekwa pembeni hakuna timu itakayoifikia mkoani Tanga”

March 06, 2013
Na Oscar Assenga, Lushoto.

MKUU wa wilaya ya Lushoto, Alhaji Majid Mwanga amesema fitna ya michezo zikiwekwa pembeni mpira ukichezwa hakuna timu yoyote mkoani Tanga itakayoweza kuifikia timu ya Lushoto Shooting ya Lushoto.

Mwanga alitoa kauli hiyo juzi wakati wa halfa ya kuipongeza timu ya Lushoto Shooting kwa kufanikiwa kumaliza vema mzunguko wa kwanza wa ligi ya mkoa.

Alisema licha ya timu hiyo kumaliza ligi hiyo wakati katika nafasi nzuri lakini bado haijamfurahisha hivyo kuwataka viongozi kuhakikisha wanaiandaa vema kwa ajili ya duru la pili pamoja na kuchukua ubingwa wa ligi hiyo.

Aidha aliwataka viongozi wa timu hiyo kuwa wabunifu kwa kubuni miradi ambayo inaweza kuwasaidia katika timu yao kuliko kuendelea kuwategemea wafadhili ambao huenda wakati mwengine wasiwasaidie.

Akizungumzia suala la nidhamu,DC Mwanga alisema hategemei kusikia nidhamu kwenye timu za wilaya hiyo hazipo wakati zikiwa zinashiriki katika mashindano mbalimbali ikiwemo kuacha kuingia uwanjani na vitu visivyostahili.

Alisema kazi kubwa ya wilaya hiyo ni kuhakikisha wachezaji hao wanauzwa kwa gharama yoyote ili waweze kuleta mafanikio na watakuwa tayari kuwauza mahali popote duniani kutokana na viwango vyao.

Awali akizungumza ,Katibu wa chama cha soka Mkoa wa Tanga,Beatrice Mgaya aliwataka wachezaji wa timu hiyo kuzingatia nidhamu pamoja na kujiandaa vya kutosha ili kuweza kutimiza azma yao ambayo yamejiwekea na kuhaidi kuisapoti timu hiyo.

Katika halfa hiyo pia wadau wa michezo wilayani humo waliweza kufanya harambee ya kuichangia timu hiyo ambapo jumla ya sh.milioni 3,480,000 zilipatikana ambapo kati ya hizo fedha taslimu zilikuwa ni 150,000 na ahadi zilikuwa ni 3,330,000.

Naye Katibu wa timu ya Lushoto Shooting,Frank Shemptemba  alisema timu hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuwa na vifaa za kufanyia mazoezi ambayo havikizi mahitaji ya wachezaji na mara nyingi wachezaji hujitafutia wenyewe hali ambayo inasababisha  kuwa na vifaa ambavyo sio bora.

Shemptemba alisema pamoja na timu hiyo kufanya vizuri kwenye mzunguko wa kwanza lakini pia waliwashukuru wadau mbalimbali akiwemo mkuu wa wilaya Lushoto na Korogwe ,Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini,Steven Ngonyani “Maji Marefu”Shabani Boznia,Julius Kimako kwa jitihada zao kuisapoti timu hiyo.

Mwisho.

“Wizara itenge bajeti za kutosha kwenye Halmashauri”
 

Na Oscar Assenga, Lushoto.

WIZARA ya Habari,Vijana Utamaduni na Michezo imeshauriwa kutenga bajeti ya kutosha katika Mashindano ya Shimisemita ambayo hushirikisha timu kutoka halmashauri mbalimbali hapa nchini ili kuzipa ufanisi na ushindani timu zinazoshiriki.

Ushauri huo ulitolewa jana na Afisa Michezo wa wilaya ya Lushoto,Stephen Shemdoe wakati akizungumza na gazeti hili na kuongoeza kuwa licha ya kufanya hivyo lakini pia alishauri kuwa uwepo utaratibu wa kushirikisha kila idara ili kuleta hamasa zaidi kwa idara kufanya maandalizi.

Shemdoe alisema suala lengine ni kuhakikisha usafiri kwa timu ambazo zinashiriki mashindano hayo zinawafikia walengo kwa wakati ili kurahisisha ushiriki wao kwani zinapochelewa huwaondolea hamasa washiriki hali ambayo huzifanya timu kushindwa kufanya vizuri licha ya kujiandaa.

Aidha alisema tiyari timu za halmashauri hiyo ambazo zitashiriki mashindano hayo mwaka huu zimekwisha kuanza mazoezi tokea jana na wanatarajia kucheza mechi mbalimbali za majaribio.

Shemdoe alisema ili mashindano hayo msimu huu yaweza kuwa na msisimuko na ushindani waamuzi ambao wanachezesha mashindano hayo wawe wale ambao wanatambulika na chama cha waamuzi nchini FRAT na wenye kujua kutafsiri vema sheria kumi na saba za mpira wa miguu.

Afisa Michezo huyo alisema timu ambazo zilianza kujiandaa ni za mchezo wa mpira wa miguu na mpira wa pete ambazo mwishoni mwa wiki zinatarajiwa kucheza mechi za kujipima nguvu na timu za halmashauri ya Korogwe.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »