Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Peter Msofwe akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la mradi wa kufundisha wataalamu wa Afya (THET), ambapo mbali na mambo mengine wamejadili kuanzishwa kwa Academy ambayo itatumika kuboresha mafunzo ya walimu wa vyuo vikuu katika sekta ya afya, kutengenezwa na kuanza kutumika kwa mitaala linganifu kwenye vyuo vikuu vya afya nchini na kutengenezwa kwa mfumo wa kuunganisha wahitimu wa afya nchini. Kongamano hilo imefanyika leo Agosti 26,2024 MUHAS Jijini Dar es Salaam.
Makamu Mkuu wa chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Prof. Apollinary Kamuhabwa akizungumza wakati wa kongamano la wa THET leo Agosti 26,2024 jijini Dar es Salaam.
Prof. Blanding Mbaga kutoka kutoka Kilimanjaro Christian Medical University College, akizungumza wakati wa kongamano hilo.
Mratibu wa mradi wa mapitio wa namna ya kufundisha wataalamu wa afya (THET) Profesa Gideon Kusigabo akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo lililofanyika leo Agosti 26,2024 katika chuo cha MUHAS Jijini Dar Es Salaam.
Na Karama Kenyunko Michuzi TV
SERIKALI imevielekeza vyuo vyote vya Afya na Sayansi Shirikishi nchini kutumia mtaala mmoja ili kuwa na watoa huduma wenye ujuzi na ubora unaolingana baada ya mtaala wa awali kuonekana kutotosheleza mahitaji.
Hayo yamesemwa leo Agosti 26,2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msofwe wakati wa kongamano lililoandaliwa na Mradi wa THET.
Mradi huo wa mapitio wa namna ya kufundisha wataalamu wa afya (THET) ulishirikisha vyuo vikuu vya Afya na Sayansi Shirikishi vya Muhimbili (MUHAS), KCMC, Chuo cha Katoliki CUHAS, San Francisco na Chuo Kikuu cha Duke.
Ameeleza kuwa wadau walipendekeza kutumika kwa mbinu za kibunifu kwa ajili ya kuhakikisha elimu ya juu kwa upande wa vyuo vya Afya vinakuwa na ubora ili kuondoa mashaka kwa wagonjwa pindi wanapohudumiwa.
"Tuna Sera ya Elimu ya mwaka 2023 imebadilisha mitaala kwa ngazi zote kuanzia shule ya msingi hivyo nasisitiza vyuo vya Afya viwe na mtaala mmoja," alisema Profesa Msofwe.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Apollinary Kamuhabwa amesema kuwa mradi huo uliangalia namna wanavyowatahini madaktari wa binadamu na wauguzi.
Alisema kuwa mtaala huo utainua ubora na mafunzo ya elimu ya juu nchini kwa madaktari na wauguzi watakuwa na uelewa wa pamoja.
"Teknolojia imebadilika magonjwa yamekuwa mengi na watu wengi hupitia kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kwenda kuonana na daktari hivyo ni lazima wataalamu wa afya wajiandae na mabadiliko haya," amesema Profesa Kamuhabwa.
Naye, Mratibu wa THET Profesa Gideon Kusigabo amesema kuwa mtaala wa awali waliokuwa wanautumia haukuwa vizuri kwani walimu walikuwa wanashindwa jinsi ya kuandaa mafunzo kwa vitendo.
Pia amesema wanalenga kuhamasisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa ajili ya kutekeleza mtaala na kuongeza uwezo wa walimu wawe bora katika masuala ya afya.
"Tunalenga kuendeleza tafiti ndani ya ufundishji ili tuwe na walimu bora kwani walimu wengi wanaingia kufundisha lakini hawana viwango bora na athari zake ni kutoweza kutahini wauguzi na madaktari wazuri na kutoweza kufundisha vizuri," amesisitiza.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa malalamiko kwamba watoa huduma za afya hususan wahitimu wa udaktari na uuguzi kutokuwa na ubora unaotakiwa.
EmoticonEmoticon