WAZIRI KIJAJI AHIMIZA WATENDAJI KUFANYA KAZI KWA BIDII

July 06, 2024

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na viongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais mara baada ya kupokewa katika Ofisi ndogo jijini Dar es Salaam leo tarehe 06 Julai, 2024.

…..

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amehimiza watendaji wa Ofisi hiyo kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kufikia malengo yaliyowekwa katika hifadhi endelevu ya mazingira.

Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais ni pana na inagusa moja kwa moja maisha ya kila siku ya wananchi hivyo wanahitaji kuelimishwa ili waweze kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira.

Mhe. Dkt. Kijaji amesema hayo wakati akizungumza na viongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais mara baada ya kupokewa katika Ofisi ndogo jijini Dar es Salaam leo tarehe 06 Julai, 2024.

Ametolea mfano wa biashara ya kaboni ni baadhi ya masuala ambayo ni mapya katika jamii hivyo, ni vyema wananchi wakapata uelewa ili kuhusu fursa zinazopatikana katika ili wananchi washiriki kwa kupanda miti ambayo mwisho wa siku pamoja na kusaidia katika hifadhi ya mazingira lakini pia huingiza fedha.

“Katibu Mkuu na timu yako naomba niwahakikishie ushirikiano na ntakuwa mwanafunzi kwenu nikiendelea kujifunza ili kazi iwe rahisi na nawashukuru kwa kunipoka tangu kule Zanzibar hadi hapa (Dar es Salaam), tuchape kazi,” amesisitiza Dkt. Kijaji.

Mhe. Dkt. Kijaji amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua katika nafasi hiyo na kumuahidi kuchapa kazi na kuahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema lipo jukumu la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kufikia maono ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara katika nishati safi na kushirikiana na wadau kuhakikisha wananchi wengi wanaachana matumizi ya kuni na mkaa ili kuokoa misitu.

Halikadhalika, amesema anafarijika kufanya kazi katika Ofisi hiyo chini ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ambapo amemtaja kama mlezi na mchapakazi.

Dkt. Kijaji amewapongeza watendaji kwa kuandaa Mpango kazi wa Utendaji wa Utekelezaji wa Shughuli za Ofisi ya Makamu wa Rais (2024-2025) ambao utawezesha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi na hasa kumsaidia Mhe. Makamu wa Rais katika majukumu yake kazi ya kumsaidia Mhe. Rais.

Amemshukuru Mhe. Dkt. Selemani Jafo ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na kuahidi kuendeleza pale alipoishia ili kuyafikia matamanio ya wananchi katika hifadhi ya mazingira.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja amempongeza Waziri Dkt. Kijaji na kumuahidia yeye na timu yake kumpa ushirikiano katika majukumu yake.

Kikao hicho cha mapokezi Waziri Dkt. Kijaji kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Bi. Christina Mndeme, Naibu Mkuu (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), Profesa Eliakimu Zahabu.

Mhe. Dkt. Kijaji aliteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo na kuapishwa katika Ikulu ndogo ya Tunguu, Zanzibar tarehe 05 Julai, 2024

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »