LAKE MANYARA MARATHON 2023 FURSA MPYA YA UTALII HIFADHI YA TAIFA ZIWA MANYARA

October 29, 2023

 Na. Jacob Kasiri - Manyara.


Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe.Joshua Nassari ameshiriki mbio za Lake Manyara Marathon 2023 na kusema kuwa ni fursa mpya ya utalii ndani ya Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara, hifadhi inayosifika kwa kuwa na Simba wengi wanaoparamia miti.

Mhe. Nassari alisema "kwa mara ya kwanza Wilaya ya Monduli imeandaa Marathon hii kwa lengo la kufungua fursa mpya ya utalii katika hifadhi yetu na kuongeza mzunguko wa fedha katika wilaya yetu".

"Kwakuwa eneo la Mto wa Mbu liko kimkakati wa kiutalii ndio imekuwa sababu kubwa ya kuvuta watu wengi kiasi hiki. Na tumeona kuanzia tarehe 27.10.2023 wakimbiaji walianza kuwasili hii yote imeongeza pato kwa taifa na mtu mmoja mmoja", aliongeza Mhe. Nassari.

Mbio hizi ndefu (Marathon) licha ya kuongeza fursa za kifedha kwa jamii pia, huimarisha afya na kuondoa magonjwa nyemelezi na kutoa mwanya kwa makampuni makubwa ikiwemo TANAPA kujitangaza na kupata wateja wanaowahitaji.

Afisa Mhifadhi Mkuu Kitengo cha Maendeleo ya Biashara Makao Makuu - TANAPA, Augustine Massesa alisema utalii huu wa michezo umeanza kushika kasi kwa miaka ya hivi karibuni. "Hivyo, niwaase na kuwashauri watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki, licha ya kuimarisha afya pia inakuza utalii".

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Eva Mallya alisema mbio hizi ni fursa kwetu kwa sababu baadhi ya washiriki wamehamasika kuingia hifadhini na kuliingizia Taifa mapato.

"Kwa niaba ya hifadhi tunamshukuru Mkuu wa Wilaya yetu Mhe. Joshua Nassari na waandaaji wa Marathon hii, kwa kipindi chote cha uamasishaji kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii imeleta tija kwa hifadhi yetu.

Mbio hizo zenye lengo la kuhamasisha utalii zilizobeba kaulimbiu "Tukimbie Tukitalii" zimefanyika leo tarehe 29.10.2023 zikianzia katika Lango la Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara iliyopo Mto wa Mbu mkoani Manyara.








Share this

Related Posts

Previous
Next Post »