MICHUANO YA CHAMPIONSHIP KUONESHWA TV3 BILA CHENGA

September 14, 2023

  Na Khadija Seif, Michuzi TV


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limeingia makubaliano ya thamani ya shilingi Milioni 613 na Kampuni ya Startimes kuonesha mubashara michuano NBC Championship 2023 kwa mechi 170 kupitia TV3.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar, Rais wa Shirikisho hilo, Wallace Karia amesema katika kipindi cha miaka 11 imekuwa mara ya pili kuingia makubaliano ya kuruhusu wadau kurusha matangazo ya mpira wa miguu (NBC Championship).

“Tutakuwa pamoja katika uongozi wangu sisi ni waungwana nathamini Tv3 kuja wakati Championship ikiwa katika kipindi kigumu, hivyo mtaendelea kuwa kipaumbele chetu kwa miaka ijayo baadae mambo yakiwa mazuri najua watu watakuja lakini sisi tutawapa kipaumbele Tv3,” amesema Karia 

“Tv3 itafika mbali na Championship itafika mbali pia mkataba huu ni wa miaka 3 wenye thamani ya Milioni 613 za kitanzania,” ameeleza Karia 

Karia amesema kuwa Ligi hiyo ni miongoni mwa ligi 5 kwa ubora Afrika hivyo inaenda kuwapa fursa watu wengi duniani kushuhudia vitu mbalimbali na ugumu wa ligi hiyo huku akiwatia moyo wadhamini hao (TV3) kuwa kwa sasa kuna miundombinu mizuri kwenye viwanja vilivyokidhi vigezo tayari kwa mechi hizo za NBC Championship.

Naye Meneja Masoko wa Kampuni ya Startimes, David Malisa amesema namna Tv3 ndani ya Kisimbuzi cha Startimes inakuwa kwa kasi na ndio Tv3 yenye miaka miwili tangu kuanzishwa kwake lakini tayari imeonesha michuano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Aidha, Malisa ameongeza kuwa watatoa ushirikiano wa hali ya juu na mashabiki wa soka wategemee kuona picha angavu zenye ubora zaidi kama ilivyo dhamira ya Kampuni hiyo kuhakikisha mlaji anapata kilichobora siku zote.


Pia ameeleza kuwa mbali na mashabiki kupata fursa ya kushuhudia mubashara michuano hiyo pia watapata nafasi kila mkoa kutoa maoni ya namna ya mienendo ya ligi hiyo inavyokwenda na nini kifanyike ili kuwepo na maboresho mbalimbali. 

Kwa Upande wake, Msimamizi wa vipindi kutoka Tv3, Emmanuel Sikawa amesema ni hatua kubwa kufikia makubaliano hayo yenye tija na lengo la kukuza na kuinua mchezo wa soka la Tanzania. 

"Tumejipanga kutoa madhui ya Ligi hiyo ya NBC Championship 2023 kwa mechi zisizopungua 170 mubashara na tutegemee vilabu mbalimbali vinaenda kunufaika kupitia makubaliano haya,” amesema Sikawa.

Vile vile, Sikawa amewataka mashabiki wa michezo nchini kukaa tayari kwani wamejipanga vizuri kutoa maudhui ya kimichezo na hivi karibuni itawajia Tv3 Sport lengo ni kuweka Maudhui yote ya kimichezo kwa undani zaidi.

Aidha katika kuhakikisha ligi inakuwa bora Tv3 na StarTimes tumejipanga kweli kweli na Chaneli zote mbili za Tv3 na Tv3 Sports zitakuwa kwenye mfumo wa picha angavu,” amesema Malisa.

Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) Wallace Karia, akiwa na wasimamizi wake wa Shirikisho hilo Msimamizi wa vipindi kutoka Tv3 Emmanuel Sikawa kushoto kwake Meneja Masoko wa Kampuni ya Startimes wakiwa picha mara baada ya kusaini mkataba  na baadae  kupokea mfano wa hundi ya shilingi milioni 613 za kitanzania kuonyesha michuano ya Nbc Championship kwa mechi 170 mubashara tv3 kupitia Kisimbuzi cha Startimes ambapo Leo Septemba 13,2023 wamesaini mkataba huo wa miaka mitatu.

Rais wa Mpira wa Miguu nchini (TFF) Wallace Karia akizungumza na Wanahabari Leo Septemba 13,2023 mara baada ya kusaini mkataba wa makubaliano kati ya Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) pamoja na tv3 kuonyesha mubashara Ligi ya Nbc Championship kwa zaidi ya miaka mitatu mkataba wenye thamani ya shilingi Milioni 613 za kitanzania 
 Msimamizi wa vipindi kutoka Tv3 Emmanuel Sikawa akizungumza na Wanahabari, wadau wa Michezo pamoja na viongozi kutoka Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) akieleza zaidi kuwa tv3 imejipanga kutoa maudhui ya kimichezo na mashabiki wa michezo nchini watarajie ujio wa tv3 Sport lengo ni kukuza michezo nchini Tanzania 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »