CCM TANGA YATOA MAELEKEZO KWA MKUU WA WILAYA YA KOROGWE MWEGELO

August 08, 2023

 








NA MASHAKA MHANDO, Korogwe 


CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga, kimetoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya Korogwe Jokate Mwegelo kupitia Katibu Tawala wake (DAS) Mwanaid Rajabu, wahakikishe vituo vya afya vya Kerenge na Mnyuzi vinamalizika haraka ili vianze kutoa matibabu kwa wananchi.



Akizungumza katika siku yake ya kwanza katika mwendelezo wa ziara zake kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa ilani ya chama, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajabu Abdallah ambaye alitoa maelekezo hayo baada ya kutofurahishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi hiyo.


Aidha aliiomba Ofisi hiyo ya DC kufuatilia kwa makini taarifa za kibank ili kuweza kujiridhisha na matuminzi ya fedha za miradi hiyo baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Korogwe Vijijini kueleza kwamba kipo kiasi cha fedha kimebaki ingawa mradi huo umesimama kwa sasa.


Rajabu alisema Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo vya afya kwa lengo la kuwasaidia wananchi wanaoteseka kwa kutembea umbali mrefu zaidi ya km 40 kufuata huduma Korogwe Mjini jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya wananchi hao.


"Mna DC makini sana katika wilaya hii na naomba nitoe maelekezo yafuatayo, DAS hakikasha unamwambia DC mfuatilie majengo haya na yaishe mapema wananchi wetu wapate huduma, lakini pia fatilieni fedha kama ipo kweli kwenye akaunti" alisema na kuongeza,


"Haiwezekani Rais Dkt Samia Suluhu Hassan atafute fedha kwa kuzunguka huko na huko halafu watu washindwe kuzisimamia, watumishi mliopewa dhamana fanyeni kazi kwa weledi wenu na maelekezo haya tunayoyatoa kama hamtayafanyia kazi mtajua chama hiki ni kikubwa kuliko mtu yeyote yule,".


Alisema kinachofanywa na watendaji na Viongozi Wilayani hapo kwa kutokukamilisha ujenzi wa vituo hivyo ni kumchonganisha Rais, Mbunge na hata Diwani dhidi ya wananchi na kuonekana Serikali haiwajali wananchi wake kumbe Korogwe wameletewa fedha nyingi katika miradi mbalimbali lakini watendaji wanashindwa kuzisimamia.


Alisema vipo vituo vya afya vimejengwa kwa gharama hizo hizo za Shs Mil 400 karibu Mkoa mzima wa Tanga na majengo yote yamejengwa tofauti na Korogwe ambapo wamepokea shs Mil 500 kwa kituo kimoja na havijakamilika hali inayoonekana kuna matuminzi mabaya ya fedha.


Aidha alisema pesa nyingi zimeelekezwa Wilayani Korogwe kwa ajili ya miradi ya vituo vya afya jambo la kusikitisha vituo hivyo havijakamilika na ni dalili za wazi zinazoonyesha Wilaya ya korogwe imeonyesha kiasi gani kuna uzembe wa usimamiaji wa miradi ya maendeleo.


Rajabu aliwataka viongozi waliopewa dhama na Rais wafanye kazi kwa weledi na watambue kufanya hivyo kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa kama sio kumaliza kero za wananchi hasa katika miradi ya kimaendeleo.


Kwa upande wake Mbunge wa Korogwe Vijijini Timotheo Mzava alisema kwanza wanamshukuru Mh, Rais kwa kutoa Bil 1 kwa ajili ya ujenzi wa vituo viwili vya afya ambapo Kituo cha afya cha Kerenge Shs Mil 500 na kile cha Mnyuzi Shs Mil 500 na kushukuru maelekezo ya Mwenyekiti huyo kwamba yatasaidia wananchi.


Aidha alisema changamoto ya utekekezaji wa miradi hiyo ni ucheleweshwaji na hata majengo yaliyokuwatayari hayakuanza kutumika ingawa uhitaji wa huduma hiyo ni mkubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.


Alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali ijitoe kwa nguvu zote ili utekelezaji wa vituo hivyo vya afya vikamilike kwa wakati ili kuwaondolea adha wananchi hao kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya.


Akitoa taarifa fupi ya mradi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Korogwe Halfan Magani alisema miradi hiyo imechelewa kutokana na taratibu za kimanunuzi kupitia mfumo wa force Account kupitia kamati ambazo zipo Kijijini.


Alisema mbali ya changamoto hiyo ya mfumo wa kimanunuzi pia  mkandarasi alishindwa kuendelea na mradi na Halmashauri ipo kwenye mchakato wa kumtafuta mkandarasi mwengine ili aweze kumalia sehemu iliyobaki.

Mwisho

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »