NA
K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MBEYA
MSTAAFU
wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kutoka wilaya ya
Kyela mkoani Mbeya, Bi. Monica Kamoza, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajali Wastaafu na Wazee kwa
kuwalipa pensheni na mafao kwa wakati.
Bi. Kamoza ametoa shukrani hizo Jumamosi Agosti 5, 2023 wakati akikabidhi zawadi ya boga kubwa kwa watumishi wa PSSSF kufuatia kile alichoeleza ni kufurahishwa na huduma nzuri anazopata kutoka PSSSF
“Ninamshukuru sana Mhe. Rais kwa upendo wake, anatujali sisi Wastaafu na Wazee,
haya yote tunayofurahia ya kupata huduma bora yanatokana na uongozi wake mzuri.”
Alisema
Bi
Kamoza ambaye alikuwa mfanyakazi katika hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya
Kyela akiwa kama mtaalamu wa afya ya macho, alistaafu Desemba 26, 2021 na
kilichompeleka kwenye banda la PSSSF ni kupata huduma zinazohusiana na taarifa
zake za ustaafu.
“Nimefurahishwa
na huduma safi na za haraka nilizopewa kwenye banda la PSSSF, kilichonileta hapa
ni kupata taarifa yangu ya malipo ya mkupuo ili nijue kama kulikuwa na mapunjo
au la, nimepewa taarifa na ufafanuzi wa kina na hakukuwa na mapunjo yoyote.”
Alifafanua Bi. Kamoza.
Mstaafu
huyo alisema, ukiacha huduma aliyopewa kwenye banda hilo, jambo lingine
lililomfurahisha hata wakati anastaafu alipata malipo yake ya mkupuo ndani ya
mwezi mmoja na hata malipo ya pensheni ya kila mwezi hayajawahi kuchelewa.
“Mwezi
uliopita (Julai) nimepokea malipo yangu ya pensheni tarehe 21, mwezi wa sita
tarehe 24, kwa kweli nawapongeza sana kwa huduma zenu bora na nzuri.”
Alipongeza.
Akizungumza
baada ya kupokea zawadi hiyo kwa niaba ya wafanyakazi wa Mfuko wanaotoa huduma
kwenye banda la PSSSF, Mhasibu Mkuu wa PSSSF, Bi. Grace Kabyemela, alimshukuru Bi.
Kamoza kwa zawadi hiyo kwa wafanyakazi wa PSSSF.
“Zawadi
hii ina maana kubwa sana kwetu, inaonyesha kutambua ubora wa huduma tunazotoa
kwa wanachama na wastaafu wa Mfuko na tunachoahidi ni kuendelea kutoa huduma
bora na za viwango.” Alisema.
Huduma
zinazotoelwa kwenye banda la PSSSF ni kama zile zinazotolewa kwenye ofisi za
Mfuko huo zilizoenea kote nchini.
Mwanachama
wa PSSSF anapofika ataweza kupata taarifa za uanachama wake, taarifa za
michango, taarifa za mafao, taarifa za uwekezaji, mstaafu ataweza kujihakiki na
kupata elimu ya hifadhi ya jamii kwa ujumla.
EmoticonEmoticon