Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Maj. Gen. Gaudence S. Milanzi (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Historia Asilia ya Berlin Ujerumani (Berlin Museum of Natural History), Prof. Johannes Vogel kuhusu masalia ya mjusi wa Tanzania yaliyofadhiwa katika makumbusho hiyo.
.....................................................
Ujerumani
na Tanzania zimekubaliana kuendeleza tafiti za masalia ya mijusi katika eneo la
Tendaguru mkoani Lindi.
Makubaliano
hayo yamefikiwa baada ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen.
Gaudence Milanzi kutembelea Makumbusho ya Historia Asilia ya Berlin (Berlin
Museum of Natural History) nchini Ujerumani yanapohifadhiwa pia masalia ya
mijusi waliopatikana eneo la Mlima Tendaguru mkoani Lindi.
Maj.
Gen. Milanzi aliongoza msafara
wa Tanzania ulioshiriki maonesho ya Kimataifa ya utalii ya ITB Berlin 2018 yaliyohitimishwa
jana nchini Ujerumani. Maonesho hayo yaliyoanza tarehe 7 mwezi huu yalihusisha taasisi
5 za Serikali na Makampuni binafsi 60 kutoka Tanzania.
Mkurugenzi
Mkuu wa Makumbusho hiyo, Prof. Johannes Vogel alimueleza Maj. Gen. Milanzi kuwa
shughuli kubwa inayofanywa na makumbusho hiyo ni utafiti kwa ajili ya maendeleo
ya sayansi, elimu na ufahamu wa mambo mbalimbali kuhusu Dunia, viumbe pamoja na
mazingira ili maarifa na ufahamu huo usaidie binadamu kutawala maisha yake na
mazingira yanayomzunguka.
Akizungumzia
fursa zilizopo za kushirikiana kutafiti maeneo yalikopatikana masalia ya mijusi
hao na viumbe wengine Prof. Johannes alisema, Makumbusho yake ipo tayari
kushirikiana na Wanasayansi wa Tanzania ili kujenga uwezo wa kufanya utafiti na
kupata matokeo yatakayochangia katika hazina ya maarifa na sayansi ya viumbe na
mazingira.
“Ili
kuwa na utafiti endelevu, ni vema kwa nchi ikawekeza kwa wataalamu wake ili
kuendeleza utafiti na maendeleo ya sayansi.
Hivyo tupo tayari kushirikiana ili kujenga uwezo kwa wasomi wa Tanzania
kuweza hatimaye kufanya utafiti na kuleta maendeleo kwa nchi yao” alisema.
Akizungumzia
kuhusu masalia ya mijusi waliopatikana Tendaguru na ambayo yanahifadhiwa katika
makumbusho hiyo, alisema badala ya kuwarudisha nchini Tanzania, ni vema
wakachukuliwa kuwa elimu, utafiti na maendeleo ya sayansi yanayopatikana
kutokana na kuwafanyia utafiti ni kwa maendeleo na ustawi wa dunia nzima.
“Ichukuliwe
kuwa huu ni urithi wa dunia nzima na hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa
urithi huu hauachi ukapotea. Hivyo, ni
vema tukaimarisha utafiti katika eneo walikopatikana ili kupata masalia mengi
zaidi na kuitangaza Tanzania katika Nyanja za utafiti.
“Makumbusho
yangu ipo tayari kufanya ziara ya kuimarisha mazungumzo na mamlaka za Tanzania
mapema iwezekanavyo ili utafiti katika eneo la Tendaguru uendelee kwa manufaa
ya Tanzania na Dunia nzima”. alisema Prof. Johannes.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu Milanzi aliahidi kuwapa ushirikiano ili kuwezesha
tafiti hizo kufanyika kwa ajili ya ustawi wa sayansi na uchumi wa nchi zote mbili.
Alimkaribisha Prof. Johannes na timu
yake kuja Tanzania mapema iwezekanavyo ili kujadili na kukamilisha makubaliano
ya kuendeleza tafiti hizo.
Awali,
Maj. Gen. Milanzi alipata fursa ya kuonana na kufanya mazungumzo na Balozi wa
Tanzania nchini Ujerumani, Dk. Abdalla Possi. Miongoni mwa mambo waliyozungumza
ni pamoja na masalia hayo ya mjusi wa Tanzania anayehifadhiwa katika moja ya
makumbusho nchini humo.
Balozi
Possi alisema kuwa kwa maoni yake haoni kuwa wazo la kuhamisha masalia hayo
kurudishwa Tanzania kuwa litakuwa na tija kwa maendeleo ya utalii na utafiti wa
sayansi kwa nchi yetu.
Alitoa
baadhi ya sababu kuwa sio kweli kuwa masalia hayo ndiyo kivutio kikubwa pekee
kinachofanya wanasayansi na watalii wengi kutembelea makumbusho hiyo na hivyo
kuipa mapato makumbusho hiyo.
“Makumbusho
inapata ruzuku kutoka serikalini na kiingilio ni sehemu ndogo sana ya mapato ya
makumbusho hiyo. Fedha nyingi za
kufanyia shughuli za Makumbusho ya Berlin zinatokana na fedha zinazolipwa kwa
ajili ya kufanya utafiti na si viingilio katika makumbusho” alisema Dk. Possi.
Alisema
makumbusho hiyo ina mikusanyo mingi ya viumbe mbalimbali zaidi ya milioni 30
ikiwemo ya mijusi kutoka nchi nyingine duniani.
Mkusanyiko huo kwa pamoja unatoa mvuto kwa watafiti na watalii
kutembelea na kufanya shughuli zao chini ya makumbusho hiyo.
Dk.
Possi alisema kuendelea kuwepo masalia hayo katika makumbusho hiyo kuna manufaa
zaidi ya kuitangaza Tanzania kiutalii na utafiti wa kisayansi kuliko masalia
hayo yatakapoondolewa katika makumbusho hiyo na kurejeshwa nchini
Tanzania.
Alisema
kuwepo masalia hayo katika makumbusho hiyo ni kama Balozi wa utalii na utafiti
wa kisayansi anayeitangaza Tanzania sehemu mbalimbali duniani.
Akizungumzia
mchakato unaoendelea hivi sasa hapa nchini wa kuandaa Utambulisho mpya wa
Tanzania (National Branding), Balozi Possi alishauri kuwa ni vema mabadiliko
yatakayopelekea kuondokana na utambulisho unaotumika hivi sasa ukaangaliwa kwa
umakini kwa kuwa kuna hatari ya kupoteza msisitizo uliopo katika vivutio
maarufu vya utalii nchini na kutoa fursa kwa washindani kutangaza utalii wao
kupitia vivutio hivyo.
Alisema
endapo hakuna athari kwa kutumia utambulisho wa sasa ambao ni maarufu (Tanzania
the Land of Kilimanjaro, Serengeti and Zanzibar), ni vema zikaangaliwa pia
athari zitakazopatikana kwa kuachana na “brand” inayotumika hivi sasa.
Alisema
kuwa baadhi ya vitu vinavyotumika kwenye utambulisho wa sasa tayari ni
“brand”. Alitoa mfano kuwa Mlima
Kilimanjaro ni Brand maarufu na inayojiuza, hali kadhalika kwa Serengeti na
Zanzibar.