WATANZANIA
wamekumbushwa kuwajali na kuwangaalia watoto yatima na wale wanaoishi
katika mazingira magumu kwa kuwatimizia mahitaji yao ya kimwili na
kiroho.
Aidha, wamepaswa kutambua kwamba wana wajibu wa kusaidia watoto hao kwa kuwa wanawekeza kwa manufaa ya taifa na wao wenyewe.
Kauli
hiyo imetolewa na Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko wa
Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam, akizungumza baada ya
kukabidhi vifaa, bidhaa na mahitaji mbalimbali ya watoto yatima wa kituo
cha Amani, kilichopo Bagamoyo, kiasi cha kilomita 65 kutoka Dar es
salaam.
- na Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko (mwenye gauni la bluu) wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam akizungumza jambo mara baada ya kuwasili kwenye ofisi za Mkurugenzi wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Amani, Margareth Mwegalawa (katikati) kukabidhi vitu mbalimbali kituoni hapo akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi wa kanisa, waumini na wamama.
Akitoa maneno yanayogusa nyoyo huku akikariri maandiko Mchungaji Faith alisema:“Dini
iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu baba ni hii, kwenda kuwatazama
yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa”
Alifafanua
kwamba Kanisa lisiloangalia yatima na wajane si Kanisa, alisema na
kuongeza kuwa waumini wanastahili kuwajibika kwa hilo.
Aidha,
alisema kama Kanisa wanajali watoto na ndio maana wamefunga safari
kwenda kuwaona na wamefurahi kuwaona na kushiriki nao tafrija fupi baada
ya kuwakabidhi zawadi mbalimbali.
- na Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko (wa kwanza kulia) wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam na baadhi ya viongozi, wakinamama na waumini wakifungua tafrija hiyo fupi kwa maombi kabla ya kukabidhi mahitaji mbalimbali katika kituo cha kulelea watoto yatima kilichopo kijiji cha Zinga, Bagamoyo.
Waumini wa kanisa hilo walikabidhi mahitaji ya shule ya watoto, mavazi na chakula.
Aliwataka
watanzania kuwa na tabia ya kujali watoto hao kwa kuhakikisha wanapata
mahitaji yao kila siku na sio siku ya sikukuu tu.
Alisema
watoaji wanapaswa kutoa kwa hali na mali kwa ajili ya kuondoa dhiki za
watoto hao, ikiwa ni sehemu ya Baraka kamili kwa Mungu na pia kwa taifa.
Alisema
watoto hao hawajulikani kesho watakuwa watu gani na kama watalelewa
vyema watakuwa ni sehemu ya taifa lenye uadilifu na woga kwa Mungu.
Alisema kwa kuwezesha utulivu wa watoto hao, watoto watamjua Mungu na hivyo kujenga taifa lenye maisha yenye utukufu wa Mungu.
Naye,
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Esther Pilila alisema kwamba kama
wanawake katika Kanisa lao wamesukumwa na haja ya kuwaangalia watoto hao
kama wajibu wao.
Akizungumza
kushukuru Mkurugenzi wa kituo hicho Margareth Mwegalawa aliomba
watanzania kuwakumbuka watoto hao na kuitafadhalisha serikali kuwapitia
kila mara kwa kuwa wao ndio walezi wa watoto.
Alisema pamoja na chakula walichopewa wanatamani watu mbalimbali kuendelea kuwajali watoto kwa kuhakikisha wanakuwa salama.
Alisema
wadau mbalimbali wasiangalie tu vituo vya mashirika ya dini bali vituo
vyote ambavyo vinabeba mzigo wa malezi kwa watoto yatima na wale
wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Alisema kituo cha Amani chenye watoto 40 kinahitaji kupata uzio ili kuhakikisha watoto wapo salama.
Naye
mtoto Salama Ismail (12) alishukuru kwa misaada hiyo ya mavazi na
chakula, mafuta ya kupakaa, miswaki na madaftari na kutaka wananchi
wamjue Mungu kwa kuwajali.
Naye
Haji Joseph (11) aliomba viongozi wa serikali kuwatembelea kwani wao
ndio wazazi wao na kuwasaidia kuimarisha upatinakaji wa nishati katika
kituo chao hasa umeme wa REA.
“Tunaomba viongozi wa serikali watutembelee tuwajue na hasa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa” alisema mtoto huyo.
- Watoto wa kituo cha kulelea yatima cha Amani kilichopo Zinga, Bagamoyo wakitoa burudani sambamba na Mkurugenzi wa kituo hicho Margareth Mwegalawa walipotembelewa na waumini wa kanisa la Ukombozi wakiongozwa na Mchungaji Faith Tetemeko (hawapo pichani) wakati wa tafrija fupi ya kukabidhiwa mahitaji mbalimbali ya kujikumu kituoni hapo.
- Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko (mwenye gauni la bluu) wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam akicheza sambamba na mtoto Haji Joseph (11) katika tafrija fupi ambapo Kanisa la Ukombozi lilikabidhi vitu mbalimbali zikiwemo sare za shule, vyakula, madaftari, nguo na mahitaji mengine ya kujikimu.
- Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko (katikati) wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam akikabidhi vifaa, bidhaa na mahitaji mbalimbali ya watoto wa kituo cha Amani cha watoto yatima, kilichopo Bagamoyo kwa Mkurugenzi wa kituo hicho Bi. Margareth Mwegalawa (kulia) katika hafla fupi iliyofanyika kituoni hapo Bagamoyo. Kushoto ni , Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Kanisa la Ukombozi tawil la Dar es Salaam, Esther Pilila.