Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mh.Luhaga Mpina (mwenye miwani) akiangalia maboksi ya samaki aina ya Migebuka yenye kilo
240 yaliyokamatwa katika kituo kikuu cha basi cha mjini Kagera hapo jana.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mh.Luhaga Mpina(mwenye
miwani ) akitoa tamko la kumsimamisha kazi mara moja Afisa wa Kitengo cha Doria na
Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana Ayoub Ngoma kwa tuhuma za kushiriki
katika utoroshaji wa samaki wenye kilo 2530 kwenda nchini Burundi zenye
thamani ya shilingi 20,850,000/= hapo jana.
Moja
ya boti inayotumika kwenye doria katika ziwa Viktoria na Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa
mpakani katika Mkoa wa Kagera.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Yohana Budeba kumsimamisha kazi mara moja Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti
wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana
Ayoub Ngoma kwa tuhuma za
kushiriki katika utoroshaji wa
samaki wenye kilo 2530 kwenda nchini Burundi zenye thamani ya shilingi
20,850,000/= hapo jana.
Akizungumza katika ofisi ya Kitengo hicho iliyopo mjini
Kagera, Mpina alisema mnamo tarehe 03/12/2017 majira ya Saa 03:00 asubuhi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya
ya Ngara ilikamata gari lenye namba za uasajili T 614 CLQ aina ya Mitsubishi
Canter likiwa limepakia samaki zenye uzito wa kilo 2,000 aina ya Sangara na
kilo 530 wa aina ya Sato kwenye mpaka wa Murusagamba wilayani Ngara.
“Katika kipindi cha uongozi wangu, tayari nimesha waagiza
Makatibu Wakuu waliopo katika Wizara yangu kutembea na barua zilizozosainiwa za kusimamisha kazi
watumishi wote wanaohujumu jitihada za Serikali ibaki kujaza jina tu. Kwa sasa
hatuna hata nusu dakika ya uvumilivu kwa watu kama hawa, tutawaondoa mara
moja.” Alisisitiza Mpina
Aidha, Waziri alisema Afisa huyo na Dereva wa gari hilo bwana
Ayuob Sanga wanashikiliwa na polisi kwa hatua za kisheria kwa kuhusika na tukio
hilo, na kuongeza kwamba samaki hawa walikuwa
wakitoroshwa kwenda nje ya nchi bila ya kufuata Sheria ya Uvuvi Na 22 ya 2003
na taratibu mbalimbali za usafirishaji wa samaki na mazao yake nje ya nchi.
Afisa Mfawidhi wa Kanda wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi
wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana Gabrieli Mageni alimweleza Waziri Mpina
baadhi ya taratibu zilizokiukwa kuwa ni pamoja na samaki hao kutopaswa kuvuliwa
kwa kuwa walikuwa wakubwa zaidi ya
sentimeta 85 na wadogo chini ya sentimeta 50, msafirishaji kutokuwa na kibali
cha kusafirisha mazao ya uvuvi, kutolipia ushuru na mrabaha wa Serikali, kutokuwa
na cheti cha afya pamoja na leseni ya kuuza mazao ya uvuvi nje ya nchi.
Waziri Mpina alisema samaki
hao walitaifishwa na kugawanywa kwa wananchi wa Murusagamba, Kiteule cha Jeshi
la Wananchi la Tanzania Murusagamba, Kituo cha Polisi Murusagamba pamoja na Shule
ya Sekondari Murusagamba baada ya kupata kibali cha Mahakama.
Alisema kazi hiyo ilifanyika
chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ngara.
Luteni kanali,Michael Mtenjele. Aliongeza kuwa, uchunguzi wa awali ilibaini
kuwa samaki hao walitokea kwenye kijiji cha Izigo wilayani Muleba.
Ametaja baadhi ya matukio yaliyotokea hivi karibuni kuwa ni
pamoja na kukamatwa kwa furu kilo 9100 zilizokuwa
zinatoroshwa kwenda nchini Uganda ambapo zilitaifishwa na kuuzwa kwa amri ya mahakama
na watuhumiwa wawili kufikishwa mahakamani kwa kosa hilo.
Kukamatwa kwa uduvi
kilo 5000 ambazo zililipiwa mrabaha na mtuhumiwa kulipa faini ya shilingi
100,000/=,kukamatwa kwa mafurushi 6 ya Samaki
aina ya Migebuka yenye kilo 240 katika kituo cha Basi cha Bukoba zilizokuwa zikitoka
mkoani Kigoma kwenda Uganda ambapo mtuhumiwa alikimbia na samaki hao kutaifishwa.
Katika tukio jingine jumla ya kilo 100 za mabondo mabichi ya samaki
yamekamatwa kwenye doria mpakani Mtukula na mtuhumiwa amefikishwa polisi kwa hatua za kisheria.
Waziri Mpina amewaomba wavuvi kuzingatia Sheria na taratibu
mbalimbali za uvuvi nchini ili sekta hiyo iwe na tija na kuchangia katika
uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025.
Wakichangia kwa nyakati tofauti watumishi wa kituo hicho
waliiomba Serikali kupitia kwa Waziri Mpina kuangalia namna ya kuongeza nguvu
kazi na vitendea kazi mbalimbali vitakavyosaidia kudhibiti uvuvi haramu.
Nahodha Mkuu wa kituo hicho, bwana Ernest Maguzu alisema kazi
ya doria katika ziwa Viktoria imekuwa ngumu kutokana na maendeleo
makubwa ya teknolojia ya
mawasiliano kwa kuwa wavuvi wamekuwa wakiwasiliana mara moja kutumia simu za
mikononi pindi wanapoziona boti za doria zinaingia ziwani na kufanikiwa
kukimbia.
Naye Kaimu Afisa Mfawidhi wa Kitengo cha Udhibiti wa Ubora na
Masoko bi, Theresia Temu aliiomba kuongeza udhibiti wa usafirishaji wa bidaa
zitokanazo na mazao ya uvuvi nje ya nchi kwa kuwa hivi sasa Serikali imekuwa
ikipoteza fedha nyingi kutokana na wafanyabiashara kutorosha mazao hayo
mipakani bila kulipa ushuru.
Bi Temu alisema kuwa inakadiriwa kuwa zaidi ya tani mia moja
ya mazao ya uvuvi yanatoroshwa kila
mwezi katika mipaka ya nchi jirani hivyo jitihada za pamoja baina ya wadau
mbalimbali zinahitajika ili kupambana na tatizo hili
“Mheshimiwa Waziri hili ni tatizo kubwa tunaomba Serikali
kuliangalia kwa jicho la tatu namna nyingine tutaendelea kuibiwa” alisisitiza
bi Temu
Waziri Mpina alisema
Halimashauri zote nchini zinatakiwa kushiriki kikamilifu katika kulinza
raslimali za majini na baharini kwa
kuwa licha ya raslimali hizo kutoa mchango mkubwa wa uchumi kwa taifa pia manufaa yake
ni kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.
“Nataka suala la uvuvi wa mabomu na nyavu za kukokota liwe
historia katika nchi yetu. Tutaendelea kuchukua hatua kali kwa yeyote atakaje tuhujumu” alisisitiza Mpina