Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imesema imesikitishwa na kitendo cha mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF) kujitangazia ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili tarehe 25 Oktoba, 2015 na imevitaka vyombo vinavyosimamia utii wa sheria kumchukulia hatua kiongozi huyo wa CUF.
“kitendo cha Maalim Seif kujitangaza mshindi amevunja kifungu cha 42 (5) cha sheria ya mwaka 1984 ambacho kinaipa mamlaka Tume ya Uchaguzi kuwa chombo pekee chenye mamlaka hayo” Mwenyekiti huyo alifafanua.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari leo, Mweyekiti wa ZEC Jecha Salum Jecha alisema kuwa Maalim Seif ametenda kosa la jinai hivyo mamlaka zinazohusika zinapaswa kumchukulia hatua.
Kwa mujibu wa kifungu hicho, mtu akithibitika ametenda kosa hilo atahukumiwa kulipa faini ya Tzs laki tano au kwenda jela miaka mitano au adhabu zote.
“Tume haina mamlaka ya kumkamata wala kumhoji Maalim lakini viko vyombo vyenye mamlaka hayo hivyo itakuwa ni vyema vikatimiza wajibu wao kwa kumkamata na kumhoji mhusika hasa ukizingatiwa kuwa hii ni mara ya pili kwa Maalim Seif kutenda kosa kama hilo”
Mwenyekiti wa Tume alieleza.
Alibainisha kuwa Tume yake imekijadili kitendo hicho kwa makini na uzito unaostahiki na kubainisha kuwa tangazo hilo linaweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu uliopo nchini.
Bwana Jecha alibainisha kuwa Maalim Seif, kama walivyo wagombea wengine 13 wa nafasi ya urais wa Zanzibar wanaelewa fika sheria hiyo hivyo alitoa wito kwa wagombea wengine kuwa watulivu kama walivyo wananchi.
Kuhusu kasi ndogo ya Tumeyake kutangaza matokeo, Mwenyekiti huyo alisema hivi sasa kazi kubwa wanayoifanya ni kuhakiki kura kujua kama hakuna tofauti ya kura baina ya zile zilizoandikwa na hali halisi.
“Wanaoandika na kuhesabu kura wote ni binadamu hivyo wanaweza kuchanganya mahesabu na ndio maana kazi yetu hivi sasa ni kulinganisha kura”alisisitiza Mwenyekiti wa Tume.
Kuhusu kukamatwa kwa karatasi za kupigia kura huko katika jimbo la uchaguzi la Chonga, Wilaya ya Chake Chake, mkoa wa Kusini Pemba, Bwana Jecha alikiri kutokea kwa hilo na kwamba suala hilo sasa liko chini ya mikono ya Jeshi la Polisi.
Alitahadharisha juu vitendo vya baadhi ya wagombea kuchukua vyeti bandia vinavyoonesha kuwa tayari wao wameshinda nafasi za ubunge au ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Bwana Jecha alitoa wito kwa wananchi kufanya subira wakati huu Tume yake ikifanya kazi ya kukusanya na kuhakiki kura na baadae kuwatangaza washindi.
--
----
Cathbert Angelo Kajuna,
Founder and Mananging Director
Kajunason Blog,
P.O Box 6482,
Dar es Salaam.
Tel: +255 787 999 774
Alt: +255 765 253 445
www.kajunason.blogspot.com
"Everything is Possible Through Peace & Stability''
EmoticonEmoticon