RAIS TFF AAGIZA USIMAMIZI MECHI ZA MWISHO VPL

May 08, 2015

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amewaagiza wasimamizi wa vituo vya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuhakikisha sheria na taratibu zote za mechi zinafuatwa.

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu huu 2014/2015 inafikia tamati kesho (Mei 9, 2015) ambapo timu zote 14 zitakuwa viwanjani katika mechi ambazo ndizo zitakazotoa hatma ya timu zinazoshuka daraja.

Mechi hizo zitakuwa kati ya Ndanda na Yanga (Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara), JKT Ruvu na Simba (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Azam na Mgambo Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), Stand United na Ruvu Shooting (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga), Kagera Sugar na Tanzania Prisons (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Mbeya City na Polisi Morogoro (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya), na Mtibwa Sugar na Coastal Union (Uwanja wa Manungu, Morogoro).

KUMRADHI WANAHABARI
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Mwesigwa Selestine ameomba radhi kwa vyombo kufuatia madai ya waandishi wa habari kupata usumbufu wakati wa utoaji wa Zawadi kwa Mabingwa na washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom.

Mwesigwa alisema kwa niaba ya TFF anaomba radhi kwa usumbufu wowote uliowapata waandishi na wadau wote walioshindwa kushuhudia vema tukio hilo.

“TFF na FIFA vinatambua umuhimu na nafasi ya wanahabri na vyombo vya habari si tu katika kuutangaza mchezo, bali pia katika kutia chachu maendeleo ya mchezo wenyewe “ alisema Mwesigwa.

Hali mbaya ya hewa ilivuruga utaratibu uliokuwa umepangwa awali kuanzia itifaki ya shughuli za kabla na wakati wa mchezo na zile za utoaji tuzo.

Aidha Mwesigwa alisema TFF itaendelea kushirikiana vema na jumuiya ya wanahabari ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wana mazingira mazuri wanapofanya kazi kwenye matukio ya mpira wa miguu.


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »