Polisi mkoani Manyara wanawashikilia zaidi ya watu 13 wanaodaiwa
kuhusika na mauaji ya wakulima na wafugaji yaliyotokea wiki iliyopita
katika Kata za Matui na Kiperesa wilayani hapa.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki amesema bado wanaendelea
na uchunguzi kabla ya kuchukua hatua ya kuwafikisha mahakamani watu hao.
“Hatuwezi
kutaja idadi kamili wala majina yao ila ni zaidi ya watu 13
tunawashikilia, wanadaiwa kuhusika na tukio hilo la mauaji na baada ya
uchunguzi wetu wahusika tutakaowabaini tutawafikisha mahakamani,”
alisema.
Hata hivyo, jana na juzi hali ilikuwa shwari
katika eneo hilo huku wakazi wilayani humo wakishuhudia helikopta ya
polisi ikiwa na makamishna kutoka Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam
ikizunguka angani kuendelea na ulinzi.
Naye, Mkuu wa
Mkoa huo, Eraston Mbwilo akizungumza kwenye kikao cha ushauri cha mkoa,
alisema chanzo cha mgogoro wa ardhi na mauaji hayo ya Kiteto
yanasababishwa na baadhi ya watu kuhodhi ekari za ardhi bila ya kuwa na
vibali.
“Hili suala la baadhi ya watu kudai kuwa Kiteto
imegeuka kuwa Somalia siyo kweli, mgogoro wa Emboley Murtangos
unasababishwa na baadhi ya watu kujimilikisha ekari nyingi za ardhi
kiholela,” alisema Mbwilo na kuongeza:
“Unamkuta mtu
anamiliki ekari zaidi ya 500 kiholela, huu ni ukiukwaji wa sheria,
vijiji vina utaratibu wa kugawa maeneo, kwa nini wasiufuate?” alihoji.
Alisema
kwa sasa hali ni shwari katika eneo hilo na wanaendelea kufanya
mazungumzo na viongozi wa jamii ya wakulima na wafugaji ili kuhakikisha
kuwa mauaji na vurugu hizo havitokei tena.
EmoticonEmoticon