Tamasha la Handeni Kwetu kufanyika Desemba 13 mwaka huu

September 01, 2014
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TAMASHA kubwa la umataduni linalojulikana kama 'Handeni Kwetu' limepangwa kufanyika Desemba 13 mwaka huu, katika Uwanja wa Azimio, wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Katika tamasha hilo linalofanyika kwa mara pili, burudani mbalimbali za ngoma za asili zinatarajiwa kuonekana jukwaani, ambapo pia vikundi kutoka nje ya Handeni, mkoani Tanga navyo vitaalikwa kwa ajili ya kwenda kutoa burudani wilayani humo.

Akizungumza  jijini Dar es Salaam, Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kuwa maandalizi ya tamasha hilo yanawekwa ili kuliweka katika kilele cha ubora na kuchangia maendeleo ya sanaa na uchumi kwa ujumla.

Alisema kuwa mwaka jana tamasha hilo lilianza kwa mafanikio makubwa, ambapo wageni mbalimbali walifika wilayani humo, jambo lililochangia pia kuitangaza Handeni na mkoa mzima wa Tanga.

“Mwaka huu tumeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa tamasha letu linaendelea kukua kwa kasi baada ya kuanzishwa kwa mafanikio makubwa mwaka jana.

“Naamini kuwa haya ni matunda ya kushirikiana kwa pamoja na wadau wote, ikiwamo serikali kwa kupitia ofisi zote za wilaya ya Handeni, hivyo watu wajiandae mmbo mazuri na makubwa kutoka kwenye tamasha hili,” alisema Mbwana.

Tamasha la utamaduni la Handeni, linalojulikana kama Handeni Kwetu, ni miongoni mwa matamasha yenye mchango mkubwa, ambapo kwa mwaka jana Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ndio waliokuwa wadhamini wakuu na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuliweka katika mguso wa aina yake.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »