Baadhi ya waandishi wa habari waliwasikiliza wawasilishaji toka Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
(Picha na Hassan Silayo)
Na Fatma Salum
Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma imeendelea kuimarisha Kiwango cha uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za masuala ya ajira katika Utumishi wa Umma.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu wa Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma Bi Neema Tawale katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Bi Tawale alisema kuwa tathmini kuhusu uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za masuala ya ajira iliyofanywa na Tume hiyo mwaka 2010/2011 katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekretarieti za Mikoa imebainisha kuwa kiwango cha uzingatiaji kimeongezeka hadi kufikia asilimia 64 kwenye vipengele vya Uajiri, Upimaji wa Utendaji Kazi wa Wazi (OPRAS), Likizo ya Mwaka na Likizo ya Ugonjwa.
Akifafanua zaidi Bi Tawale aliongeza kuwa ukilinganisha na utafiti wa kwanza uliofanyika mwaka 2005/2006 ambapo kiwango kilikuwa ni asilimia 50 ongezeko hilo limetokana na elimu inayotolewa na Tume kwa wadau kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 ya mwaka 2002 na Marekebisho yake Na.18 ya mwaka 2007.
“Tume ya Utumishi wa Umma inajitahidi kuweka mikakati ili kuhakikisha inakabiliana na changamoto za masuala ya ajira katika kuongeza uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu kwa kuendelea kutoa elimu kupitia miongozo, vipindi kwenye vyombo vya habari na maonyesho mbalimbali ya kitaifa”. Alisema Bi Tawale.
Aidha Bi Tawale alisema kuwa Mwongozo uliotolewa na Tume hiyo kuhusu masuala ya ajira katika Utumishi wa Umma unawawezesha Waajiri na Mamlaka za Ajira kufuata taratibu wanaposhughulikia masuala ya ajira kwenye mamlaka zao.
Aliongeza kuwa katika kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za ajira zinatekelezwa ipasavyo Tume huagiza Waajiri au Mamlaka za Ajira kuchukuliwa hatua ikiwemo kuwaita mbele ya Tume kujieleza ikithibitika wamekiuka sheria au wameshindwa kutekeleza majukumu yao.
Naye Kaimu Katibu Msaidizi wa Tume hiyo Bw. John Mbisso alitoa msisitizo kwa waajiri kushughulikia masuala ya ajira ya watumishi wao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuepuka migogoro na kupunguza malalamiko kuhusu masuala ya ajira kwenye utumishi wa umma.
|
EmoticonEmoticon