NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Mechi ya kwanza ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya
kucheza Fainali za Afrika 2015 nchini Morocco kati ya Tanzania (Taifa Stars) na
Zimbabwe (Mighty Warriors) itafanyika Jumapili (Mei 18 mwaka huu) Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Awali mechi hiyo tulipanga ichezwe Uwanja wa Sokoine
jijini Mbeya kwa nia ya kuhakikisha mikoa yote ya Tanzania inapata fursa ya
kuwa mwenyeji wa mechi za kimataifa.
Ili Uwanja wa Sokoine uweze kuchezwa mechi za
kimataifa za mashindano, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilituma
Mkaguzi (inspector) wake kwenye uwanja huo Jumamosi (Mei 10 mwaka huu) ambapo
imeamua kuwa marekebisho yanayofanyika hayatamalizika katika muda stahili,
hivyo mchezo huo kutochezwa Sokoine.
Tunatoa mwito kwa wamiliki wote wa viwanja kuwasiliana
na TFF ili Idara ya Ufundi iwaelekeze maboresho ya kufanya ili viwanja vingi
iwezekanavyo viweze kukidhi viwango vinavyotakiwa na CAF na Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Taifa Stars ambayo ilikuwa kambini mkoani Mbeya
itarejea Dar es Salaam keshokutwa (Mei 14 mwaka huu) kujiandaa kwa mechi hiyo.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
EmoticonEmoticon