RUCO MABINGWA WA POOL VYUO VIKUU WAPONGEZWA

May 12, 2014


SAM_4505 
 Nahodha wa timu ya Pool ya chuo kikuu cha Ruco , Said Mohamed akimkabidhi mgeni rasmi kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Ramadhani Mungi kikombe cha ubingwa wa mchezo huo baada kuandaliwa hafla ya kuwakaribisha iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Gentle Hill  juzi kushoto ni meneja mauzo wa tbl mikoa ya Iringa,Njombe na Ruvuma Raymond Degera.
SAM_4480 
Kikosi cha timu ya Ruco kikiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasili mkoani Iringa
Na Denis Mlowe,iringa
 
WANAFUNZI wa chuo kikuu cha Ruaha (RUCO) cha mkoani Iringa nchini wameshauriwa kuundeleza mchezo wa Pool sambamba na kufanya vema katika masomo yao na kuwapongeza kwa kuuletea sifa mkoa wa Iringa katika mchezo huo kwa vyuo vikuu.
 
Wito huo umetolewa na mgeni rasmi, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa, ACP Ramadhani Mungi katika hafla ya kuwapongeza  mabingwa wa mchezo huo kitaifa katika ngazi ya vyuo vikuu uliondaliwa na kampuni ya TBL kupitia kinywaji chake cha safari Lager na chuo cha RUCO kuchukua ubingwa kwa mara ya kwanza iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Gentle Hill.
 
Mungi alisema wanafunzi wengi wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kubanwa na mambo ya burudani na michezo na kuwapongeza vijana hao kuwa na ratiba nzuri ya masomo na michezo hadi kufanikiwa kuchukua ubingwa wa vyuo vikuu kitaifa.
 
“Naupongeza sana uongozi wa chuo cha ruco kwa kuweka ratiba nzuri ya vipindi na michezo, utaratibu wa kujua ni wakati gani wa kusoma, wakati gani wa kufanya mazoezi hivyo bila uongozi wa chuo hicho msingefikia hapo na ndio chanzo hadi nyie kuchukua ubingwa huu na kuuletea sifa mkoa wa Iringa nawapongeza uongozi wa chuo cha ruco na vijana wangu” alisema Mungi
 
Alisema kuwa mchezo wa pool unazidi kukua kwa kasi kubwa nchini na lakini viongozi wake wanatakiwa kuwa makini na vijana wanaoweza kuharibu sifa ya mchezo huo hasa kwa vijana wanaofanya pool kama kijiwe cha kuvutia bangi.
 
Aliongeza asilimia kubwa ya vijana wanajiajiri kwa kuppitia michezo hivyo juhudi kubwa inatakiwa kuwekwa kuweza kuwawezesha vijana kuingia katika sekta ya michezo kwa kuwa ni ajira tosha katika maisha ya sasa.
 
Mungi alisema kupitia michezo hata uhalifu huwa unapungua kwa kuwa wengi wamekuwa wakijishughulisha hasa katika tasnia ya burudani kwa kuwa  hata wao wanapenda kujishughulisha katika michezo.
 
“Katika burudani uhalifu huo unapungua kwani wahalifu nao wanapenda kuburudika kwa hiyo tujitahidi sana kushughulikia michezo na burudani kuweza kupunguza uhalifu, mfano mmoja ni kuwa kuna tamasha kubwa liliwahi kufanyika hapa mkoani iringa katika kuripoti matukio siku ya pili kwa kweli polisi kulikuwa hakuna tukio lolote la uhalifu siku hiyo kwa kuwa wahalifu hao walikwenda nao kuburudika siku hiyo” alisema na kuwafanya wageni waalikwa kucheka .
 
Aliitaka serikali kuwa jirani na sekta ya michezo yote na kuiboresha kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana ambao asilimia kubwa hawana ajira na kuongeza kuwa michezo uleta afya ya akili na afya ya mwili hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kufanya mazoezi.
 
Mungi alivitaka vijiwe vyote vya mchezo wa pool kujiepusha na kuuza na kununua madawa ya kulevya na kuahidi kufanya msako mkali kwa kila kijiwe cha mchezo huo wanaojihusisha na biashara hiyo kwa kuwa vinajulikana na jeshi la polisi.
 
Alivitaja vijiwe vinavyojihusisaha na biashara hiyo kwa kigezo cha mchezo wa pool kuwa ni Mashine tatu, Ipogoro, Kihesa na Mlandege ndio vinaongoza kwa biashara hiyo inayoharibu sifa ya mchezo wa Pool.
 
Kwa upande wake nahodha wa timu ya mchezo wa Pool kutoka Ruco, Said Mohamed aliutaka uongozi wa chuo hicho kuwapa ushirikiano katika kuundeleza mchezo huo kwa kuwaandalia ratibu nzuri ya mazoezi na muda wa masomo.
 
Alisema kupitia mchezo huo wamefanikiwa kukitangaza chuo kitaifa na kimataifa hivyo ni jukumu la chuo sasa kuweka kipaumbele katika michezo mingine kuweza kukiletea sifa chuo na mkoa kwa ujumla.
 
Aliupongeza uongozi wa Tbl kuptia kinywaji cha Safari Lager kwa kudhamini mchezo huo na kuongeza soko la ajira kupitia michezo na kuutaka kuendelea  kudhamini mchezo huo.
 
Naye meneja mauzo mikoa ya Iringa,Njombe na Ruvuma Raymonda Degera aliwapongeza mabingwa hao na aliwataka kuongeza juhudi na maarifa ilikuweza kuuchukua tena mwakani katika mashindano mengine ya vyuo vikuu nchini wa mchezo wa pool

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »