MWALALA:TUMEPANIA KUCHEZA LIGI DARAJA LA KWANZA

November 19, 2013

Muheza.
KOCHA Mkuu wa timu ya Halmashauri ya Muheza inayoshiriki Ligi ya mkoa wa Tanga,Benard Mwalala amesema timu hiyo kuendelea kufanya vizuri katika michuano hiyo ni ishara tosha wanakaribia kutimiza malengo yao ya kucheza ligi daraja la kwanza msimu ujao.

Mwalala alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Tanga Raha mara baada ya kumalizika kwa mechi ya ligi hiyo kati yao na Lushoto Stars ambapo walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 5-0,mchezo uliochezwa katika uwanja wa soka Jitegemee wilayani hapa.

Bao la kwanza la Halamshauri lilipatikana katika dakika ya 20 kupitia Chalengwa Sultani ambaye alitumia uzembe wa mabeki wa timu pinzani kupachika wavuni bao hilo kabla ya Abasi Athumani kupachika bao la pili dakika ya 25.

Mpaka timu zote zikienda mapumziko,Halmashauri FC waliweza kutoka kifua mbele kwenye mchezo huo na kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo iliwachukua dakika 16 ya kupindi hicho Halmashauri kupata bao la tatu ambalo lilifungwa na Abasi Athumani ambaye aliifungia timu hiyo na bao la nne kaatika dakika ya 70.

Karamu ya mwisho ya mabao kwa timu hiyo iliweza kuhitimishwa na Ramadhani Msumi aliyemalizia krosi maridadi iliyopigwa na Abasi Athumani na kukwamisha wavuni bao hilo .

Mwalala alisema malengo yake makubwa na timu hiyo ni kuhakikisha wanapambana vilivyo ili kuweza kupata nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa wa mikoa na hatimaye ligi daraja la kwanza na ligi kuu soka Tanzania ili kurudisha hamasa ya soka iliyokuwepo wilayani hapa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »