Vijana tushikamane.

July 22, 2013
(MWENYEKITI wa Jumuiya wa Umoja wa Vijana wilaya ya Tanga,Salim Perembo akizungumza mwishoni mwa wiki katika kikao cha Baraza la Vijana wilaya hiyo kulia kwake ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga (CCM)Kassim Mbuguni na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Tanga Halima Dendego)

Na Oscar Assenga, Tanga.
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga, Kassim Mbuguni amewataka vijana kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kukulinda na kukitumikia chama hicho pamoja na kujenga mshikamano miongoni mwao.
 
Mbuguni alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki wakati akifungua kikao cha baraza la Jumuiya ya Vijana Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga (UVCCM) kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa chama hicho uliopo barabara 20 jijini Tanga.
 
Alisema ili kuweza kuhakikisha chama hicho kinazirudisha kata tisa zilizochukuliwa na vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu ujao lazima umoja huo unapaswa kuwa macho kujua kinachotakiwa kwenye kata zao ili kuyafanyia kazi kwani chama hicho kipo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wote.
 
“Jumuiya ya umoja wa vijana lazima wawe macho ndani ya chama kwa kutoa taarifa na kinachotokea ndani ya chama lengo likiwa kuzifanyia kazi na kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye maeneo yao “Alisema Mbuguni.
 
Katika kikao hicho Jumuiya hiyo kilipitisha majina ya wajumbe wa kamati ya mipango, uchumi na fedha itakayokuwa na kazi ya kuhakikisha wanabuni miradi ambayo itaiwezesha jumuiya hiyo kuwa na vitega uchumi vyao wenyewe ili iweze kusimama imara lakini pia itawasaidia kujiendesha katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
 
Majina ya wajumbe ambao wataunda kamati hiyo yalipitishwa na kikao cha baraza la Vijana wilaya ya Tanga ni Mwenyekiti,Ameet Ranjit,Katibu Akida Machai, ambao watakuwa wakishirikiana na wajumbe Mbaruku Asilia,Khalid ,Yazidu Msika,Abdul Ahmed Kassim Kassim,huku wajumbe wengine wakina mama wakitarajiwa kuongeza kwenye kamati hiyo.
 
Awali akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Tanga, Salim Perembo aliwataka vijana kuendeleza mshikamao na umoja ili kuweza kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye umoja huo lengo likiwa kukiimarisha chama hicho huku akiwataka vijana kutokubali kutumiwa kama ngazi.
 
Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe 60 kutoka kata za Chongoleani, Tangasisi, Kiomoni, Usagara, Maweni, Duga,Msambweni,Majengo,Mzingani,Marungu,Chumbageni,Kirare,Ngamiani kusini,Nguvumali,Central ,Mzizima,Pongwe na Ngamiani .
 
Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »