MGAZA: Serikali itaendelea kuhamasisha kilimo cha Muhogo

July 11, 2013
Na Oscar Assenga, Mkinga.

MKUU wa wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza amesema serikali wilayani humo itaendelea kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kilimo cha Muhogo ili kiweza kuwa mkombozi wao katika maendeleo na kuinua kipato chao.

Kauli ya Mkuu huyo wa wilaya ilisomwa na Katibu Tawala wa wilaya ya Mkinga Zuwani Makame hivi karibuni aliyemuwakilisha katika uzinduzi wa kampeni ya kilimo cha muhogo iliyoanzishwa na shirika la Farm Radio Internationali kwa kushirikiana na kituo cha Radio Mwambao ya Tanga.

Makame alisema Serikali inatambua umuhimu wa elimu kwa wakulima ikiwemo kuwapatia wakulima elimu stahiki kuhusu kilimo chenye tija wataweza kunufaika na kilimo chao, hivyo itaendelea kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya kuwawezesha wakulima kupata elimu ya kilimo bora.

Aidha alisema kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali kwenye shughuli za kilimo katika maeneo mengi hasa ya wilaya ya Mkinga, na changamoto kubwa ni ukosefu wa elimu ya njia bora ya kuendesha kilimo chenye tija hivyo kampeni hizi zimekuja wakati muafaka, naamini zitawanufaisha wakulima na kuweza kupata mazao mengi katika kilimo chao.

Alieleza kuwa uzinduzi wa kilimo hicho utasaidia wananchi kujiondoa kwenye umasikini kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo, na ndicho ambacho wenzetu wa Farm Radio international kupitia mradi huu wanafanya kuelimisha wakulima kwa njia ya Radio.

Hata hivyo amesema licha ya kuwa na wataalamu wa ugani wachache na hivyo matumizi ya redio yatasaidia kuwafikia wakulima wengi sana kwani redio zinafika maeneo mengi ili kuweza kuongeza ujuzi kwa wakulima hao kabla ya kuanza msimu wa kilimo.

Katibu Tawala huyo amewataka wakulima wote wa vijiji vya Mzingi Mwagogo, Mapojoni, Mvunde manyinyi na vijiji vyote vya wilaya ya Mkinga na vijiji jirani vya wilaya za jirani ambapo kampeni hizi zinagusa kupitia mradi wa njia bora za uvunaji ,usindikaji na uhifadhi  wa zao la muhogo , mtumie vema fursa hii iliyoletwa na wenzetu wa Farm Radio   kwa kushiriki kwenye Kampeni hii kikamilifu.

Ameongeza kuwa kampeni hii itawanufaisha sana kwenye kilimo na itawasaidia kupata masoko na kujiongezea kipato ikiwa watazingatia vema yale yatakayokuwa yanafanyika na kuelezwa na wataalamu mbalimbali wa kilimo.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Mtaalamu wa Mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo kutoka shirika la Farm Radio International lenye makao yake makuu jijini Arusha, Terevael Aremu Nassary amesem,a shirika hilo limeona umuhimu wa kushirikiana na radio Mwambao ya Tanga katika kufikisha elimu yake juu ya njia bora za uvunaji,usindikaji na uhifadhi wa zao la muhogo ambalo lina soko na linazalishwa kwa wingi mkoani Tanga ikiwemo wilaya ya Mkinga.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa radio Mwambao FM, Mfaume Kikwato alisema vipindi vya elimu juu ya njia bora ya uvunaji, usindikaji na uhifadhi wa zao la Muhogo vitakuwa vikirushwa na kituo hicho kuanzia Julai 5 mwaka huu na kuendelea kila siku za Ijumaa saa moja hadi saa moja na nusu na marudio yake yatakuwa Jumapili saa moja na nusu mpaka saa mbili usiku.

Mwisho

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »