TIMU
ya Mpira wa Kikapu ya Tanga Warriors mwishoni mwa wiki iliifunga City Kings
vikapu 46-37 katika bonanza la Michezo ambalo liliandaliwa na Bandari Tanga
lengo likiwa ni kuwaweka vijana pamoja na kuinua michezo.
Katika
mchezo huo Tanga Warriors walionekana kucheza kwa kujipanga na kupeleka
mashambulizi mara kwa mara kwenye lango la City Kings ambapo mpaka mzunguko wa
kwanza unamalizika Tanga Warriors walikuwa wanaongoza kwa vikapi 37-22 kwenye
mechi hiyo ambayo ilichezwa viwanja vya Bandari jijini Tanga.
Baada
ya kumalizika mechi hiyo ilifuatiwa na mchezo wa Pete ambapo timu ya Umiseta
Tanga iliweza kuumana na Bandari Tanga na kumalizika kwa Bandari Tanga kuibuka
na ushindi wa mabao 24-19,katika mchezo ambao ulikuwa na upinzani wa hali ya
juu.
Bonanza
hilo ambalo lilikuwa la aina yake kutokana na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali
wa michezo mkoani ambapo kwenye mchezo wa kikapu timu ya Umiseta Tanga waliweza kuifunga Bandari kwa
vikapu 24-17.
Mechi
ya mwisho ambayo ilikuwa na upinzani mkubwa ni ya kuvuta kamba ambapo timu ya
City Kings iliweza kuibuka kidede baada ya kuwavuta Tanga Warriors seti 2-1
michezo ambayo ilichezwa viwanja vya Bandari jijini Tanga.
Nyota
wa bonanza hilo alikuwa ni Adam Mkondo kutoka timu ya Tanga Warriors ambaye
alichangia kwa kiasi kikubwa kuipa ushindi timu yao kwenye mechi hiyo .
Akizungumza
kabla ya kuanza bonanza hilo mgeni rasmi, Kaimu Meneja wa Bandari Tanga,Moshi
Mtambalike Chawala alisema lengo la bonanza hilo lilikuwa kuwapa hamasa vijana
kupenda michezo pamoja na kuwataka vijana kupenda kujituma na kucheza kwa moyo
kwani michezo ni ajira ambayo inaweza kuwainua katika maisha yao.
Kwa
upande wake, Afisa Utumishi wa Bandari ya Tanga, Teckla Malombe alisifu viwango
vya wachezaji walioshiriki bonanza hilo na kuwataka vijana kuendelea kupenda
michezo na kuipa kipaumbele.
Nae
Mratibu wa Bonanza hilo, Dr.Omari Khupe alisema Bonanza hilo ni endelevu ambalo
hufanyika kila wiki ya mwishoni mwa mwezi lengo ni kuwakutanisha wanamichezo
pamoja na kuinua viwango vya michezo.
Mwisho.