Magari awafunda wasanii chipukizi.

June 03, 2013
Na Oscar Assenga,Lushoto.
MSANII Gwiji wa filamu Tanzania,  
Charles Magari  maarufu kama "Mzee wa Magari" amewaasa wasanii chipukizi wa tasnia hiyo nchini kutambua kuwa sanaa ni kazi kama zilivyo nyingine ambayo inaweza ‘kumtoa’ kijana kutoka kwenye umaskini na kuwa katika hali nzuri ya kimaisha.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki kwenye sherehe za uzinduzi wa Filamu  mpya iitwayo “Hulka” iliyofanyika mjini Lushoto, Mkoani Tanga ambapo iliwashirikisha wasanii wengine nguli kama Mzee Jengua, Davina, Birigita na Sekuti.
Magari alisema vijana wengi wanaonekana wakipoteza muda kwenye vijiwe wakipiga porojo zisizo na tija huku wakilalamikia hali duni ya maisha yao wakidai kuwa hawana ajira.
“ Ajira huwezi kuipata kwa kukaa tu na kulalamika kwani fursa ya kujiajiri imepanuka sana”, alisema Magari na kuongeza, tasnia ya sanaa bado inahitaji vijana wengi wenye kujituma.
Alieleza kuwa nia ya kuja kuzindua filamu hiyo ni kutaka kuwapa fursa vijana wa wilaya ya Lushoto kujifunza maudhui yaliyomo katika filamu hiyo na kuchukua hatua ya kujisahihisha.
Katika filamu hiyo washiriki wanaigiza tabia ya kabila fulani ambalo halikutajwa ambapo mwanamke aliyeolewa huona hapendwi asipopigwa na muwe mara kwa mara.
Nafasi ya mume anacheza Sekuti ambapo Biligita anachukua nafasi ya mke,Mume ni mtoto wa Mzee Jengua na mke ni binti ya Mzee Magari.
Akizindua filamu hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Lushoto,Majid Mwanga, Ofisa Utamaduni wa wilaya hiyo, Ezekiel Almas alisema wakati sanaa inaanza kukubalika katika jamii, upo umuhimu kwa washiriki hao kujali na kudumisha tamaduni za kiafrika.
Almas aliitaka jamii kuondoa dhana iliyojengeka katika baadhi ya watu kwamba usanii ni uhuni ambapo alieleza uhuni ni tabia ya mtu binafsi sio fani yake.
Meneja wa Creator Entertainment iliyoandaa sherehe hizo, Mwanahawa Chongole alisema kampuni yake ilikubali kuchukua jukumu la kuandaa sherehe hizo kutokana na kutambua umuhimu wa maudhui yaliyomo ndani ya filamu hiyo kwani inatoa ujumbe utakaoelimisha jamii kwa ufasaha.
Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »