DC Mgaza aitaka jamii kuona umuhimu wa kuhudhuria katika vituo vya Afya”

May 14, 2013


Na Mwandishi Wetu,Mkinga.
MKUU wa wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza ameitaka jamii kuona umuhimu wa kuhudhuria katika vituo vya afya kupatiwa tiba pindi wanapokuwa wanajisikia kuwa na maradhi badala ya kwenda kupata tiba asili ambazo hazina vipimo vya kitaalamu.

Mgaza aliitoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani ambapo kimkoa yaliazimishwa katika kituo cha Afya Maramba kilichopo wilayani hapa ambapo mkuu huyo wa wilaya alitembelea kituo hicho na kugawa misaada mbalimbali kwa wagonjwa katika halfa iliyohudhuriwa na wauguzi kutoka wilaya zote mkoani hapa.

Alisema wagonjwa ambao hawatapata matibabu ya kitaalamu wapo katika uwezekano mkubwa wa kupoteza maisha kwani hawatatambulika na wala hawatajulikana kuwa wamepoteza maisha kwa magonjwa gani na pia inawezakana ugonjwa huo ukawa ni wa mlipuko ambao unaweza kusababisha hatari ya maambukizi kwa jamii inayozunguka eneo husika.

Aidha alisema kuwa ni muhimu kwa wakinamama wote wajawazito kuhudhuria klinik kupima hali zao za ujauzito na kupata ushauri wa kitaalamu juu ya afya zao na watoto wanaotarajia kuwazaa na hatimaye unapofika wakati wa kujifungua wahakikishe wanazalia hospitalini au katika vituo vya huduma za afya vyenye wataalamu ili wapate elimu ya afya na ushauri juu ya malezi ya watoto wao.

Alieleza kuwa madhumuni makubwa ya siku hiyo ni kukumbuka tarehe aliyozaliwa mwanzilishi wa uunguzi ulimwenguni Mama Florence Night Ngale ambaye alizaliwa mwaka 1820 huko Italia katika mji uitwao Florence na hatimaye wazazi wake kuamua kumwita kwa jina la mji huo.

Mkuu huyo wa wilaya alisema aliguswa sana na kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema “Kuziba Mapengo kufikia malengo ya maendeleo ya Milenia”nayo ni kuhakikisha wanapunguza vifo vya watoto wachanga, kuboresha afya za mama wajawazito na kudhibiti magonjwa ya Ukimwi malaria na kifua kikuu.

Awali akisoma risali kwa mkuu huyo wa wilaya, Katibu wa Chama cha Wauguzi Mkoa wa Tanga(Tana), Hadija Mbasha alisema licha ya kuazimishwa siku hiyo lakini zipo changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili wauguzi mkoani hapa ikiwemo kukosa haki za zao za msingi kama vile malipo ya kazi saa za ziada pamoja na malipo ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi.

Mbasha alisema licha ya kuwepo kwa changamoto hizo lakini pia wanaiomba jamii ya Tanzania iwatambue wauguzi kama ni watu wenye huruma, upendo na msaada ikiwemo kuchukia sifa mbaya kama jamii nyengine zilivyo kwamba sio kila muuguzi ana kauli mbaya.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »