Utoaji wa Chakula Mashuleni utasaidia kuongeza kiwango cha Taaluma kwa wanafunzi

April 30, 2013

Na Oscar Assenga, Mkinga.
IMEELEZWA kuwa utoaji wa chakula mashuleni utasaidia kupunguza utoro na kufanya mahudhurio ya wanafunzi kuwa mazuri ikiwemo kupanda kiwango cha taaluma kwani watoto watakuwa na nguvu ya kusoma na kuelewa watakachokuwa wakifundishwa.

Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa chakula kwa wanafunzi iliyofanyika Duga Maforoni na Maramba ambapo alisema anaamini ulaji wa chakula mashuleni utakuwa endelevu na kuwataka wazazi na viongozi kushirikiana na walimu ili kufanikisha suala hilo.
Mgaza alisema katika kufanikisha zoezi hilo la utoaji wa chakula wazazi na wadau wachangie kwa kiasi ambacho kitakuwa kikihitajika kwa kila mtoto kwani watakapopata chakula mashuleni itasaidia pia kuimarisha afya ya watoto wao.

Aidha Mgaza aliwashauri wazazi wilayani humo kujitahidi kuwapeleka watoto wao shuleni ili kuweza kuepuka gharama ambazo zitaweza kuwakuta baade kwani zitakuwa kubwa kuliko wanavyokuwa wakifiria.

Hata hiyo mkuu huyo wa wilaya alisisitiza suala la uvaaji vya viatu mashuleni ambapo alisema tatizo la watoto kukosa viatu linapaswa kuangaliwa na wazazi kwa kuhakikisha kila mtoto wake anavaa viatu ili kuweza kuwaepusha na magonjwa ambayo huenda wakayakuta wakati wakiwa beya.

Awali akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Elimu wilayani humo, Juma Mhina alisema wanaamini zoezi la uhamasishaji lishe shuleni kwa kushirikiana na wenyeviti wa vijiji na wazazi litaweza kupata mafanikio makubwa.
Mhina alisema wanaamini mpaka ifikapo mwezi wa saba mwaka huu shule zote zilizopo wilayani humo zitakuwa zinapata chakula cha mchana mashuleni ambapo alisema lengo la kampeni hiyo ni kuwawezasha wanafunzi kusoma kwa bidii na kuweza kuelewa wanachofundishwa.

      Mwisho.

 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »