BENKI YA CRDB YATUNUKIWA TUZO YA UBORA KUHUDUMIA WAJASIRIAMALI WADOGO NA JARIDA LA EUROMONEY

July 24, 2024

 

Mkurugenzi wa Biashara ya Awali na Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul (kulia) akiwa na Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Benki ya CRDB, Toyi Ruvumbagu mara baada ya Benki ya CRDB kutangazwa taasisibora ya kuhudumia biashara ndogo na za kati katika hafla iliyofanyika jijini London nchini Uingereza mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kutokana na ubunifu na umahiri wake katika mikakati tofauti ilinayo katika kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake pamoja na wadau wengine, Benki ya CRDB imetunukiwa tuzo ya kimataifa ya benki bora Tanzania inayohudumia biashara ndogo na za kati kwa mwaka 2024 na Jarida la Euromoney la nchini Uingereza.

Tuzo hizo zinazotolewa kwa miaka 30 sasa, huzitambua benki na taasisi za fedha zenye mchango mkubwa kwa jamii inazozihudumia kwa namna tofauti hivyo kuchangia uchumi wa mataifa yao na dunia kwa ujumla.

“Euromoney ni jarida kubwa duniani linalofanya utafiti wa kina kabla ya kuitambua na kutunuku benki tuzo yake. Wanao uzoefu mkubwa wa zaidi ya miaka 30 ya kuandaa tuzo za benki dunia nzima. Najisikia furaha kwa Benki yetu ya CRDB kushinda tuzo za Euromoney kwa mwaka wa tatu mfululizo sasa,” amesema Bonaventura Paul, Mkurugenzi wa Biashara ya Awali na Kati wa Benki ya CRDB aliyepokea tuzo hiyo.

Paul amesema Benki ya CRDB imeongeza juhudi katika kuwahudumia wajasiriamali nchini kwa kubuni bidhaa zinazoendana na mahitaji yao jambo lililowawezesha wafanyabiashara kuimarisha kipato na kukuza miradi yao pamoja na kukuza mchango wao kwenye pato la taifa. Kati ya juhudi hizo, mkurugenzi huyo amesema ni utaratibu wa kuwaruhusu wajasiriamali kukopa kwa kutumia taarifa za mtiririko wao wa mzunguko wa fedha za biashara bila kuhitaji kuwa na dhamana.

“Mfanyabiashara mwenye hati ya ununuzi anaweza kupata mkopo kutoka Benki yetu ya CRDB. Tunashirikiana na wadau tofauti kufanikisha hili. Mwaka jana kwa mfano, tulishirikiana na kampuni ya Silent Ocean kuwawezesha wafanyabiashara wanaoingiza mzigo nchini kutoka nje ya nchi kwa kuwakopesha hadi dola 63,000 za Marekani (zaidi ya shilingi milioni 170) kugharimia usafiri, gharama za bandari pamoja na kodi,” amesema Paul.

Mwaka 2023 Benki ya CRDB ilikopesha zaidi ya trilioni 8.9 na asilimia 12 ya kiasi hicho kilielekezwa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati. Tengo hili limekuwa likiongezeka kila mwaka kwani mwaka 2022 ilikuwa asilimia 11 ya mikopo yote tuliyoitoa.

Matumizi ya teknolojia hasa katika malipo, Paul amesema yameongeza ufanisi katika biashara za wajasiriamali wengi. Wajasiriamali wamekuwa wakiunganishwa na mifumo ya kidijitali ya upokeaji na ufanyaji wa malipo kwa urahisi ikiwamo mfumo wa LIPA Namba na msimbomilia (QR Code), Huduma za benki kupitia mtandao (Internet banking), na huduma ya SimBanking zinazowawezesha kusimamia kwa urahisi akaunti zao.

Ili kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi, Paul amesema benki imetanua wigo kwa kuwahusisha wafanyabiashara wachanga ambao nao hunufaika kwa mafunzi na elimu ya fedha inayotolewa kupitia majukwaa tofauti. Hali hiyo, amesema imeifanya benki iongeze fungu inalolitenga kwa ajili ya kundi hili.

Paul ameongezea kuwa katika mkakati wake wa muda wa kati wa miaka mitano 2023 -2027, Benki ya CRDB imetoa kipaumbele kikubwa katika uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo, na kati (MSMEs). Paul amesema katika nusu ya mwaka huu tayari Benki ya CRDB imesha toa mikopo yenye thamani ya jumla ya takribani Shilingi trilioni 1.5.

Hivi karibuni Benki ya CRDB iliadhimisha Siku ya Wajasiriamali Duniani, ambapo pamoja na maadhimisho hayo ilizindua akaunti maalum kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na wa kati iliyoboreshwa zaidi na inayoendana na mahitaji halisi ya wateja ijulikanayo kama ‘Biashara Account.’

Kila mwaka, zaidi ya benki na taasisi za fedha 600 kutoka zaidi ya nchi 100 duniani kote hushiriki tuzo za Euromoney zinazoheshimika zaidi katika sekta ya benki na fedha kutokana na utafiti unaofanywa dhidi ya washindi pamoja na ushauri elekezi kwa washiriki wote ambao umekuwa msaada mkubwa wa kuboresha huduma za benki nyingi ulimwenguni kote.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »