LIPENI KODI KUIWEZESHA TBA KUJENGA NYUMBA NYINGI ZAIDI - WAZIRI BASHUNGWA

July 24, 2024

 * TBA yapongezwa kwa ubunifu katika upangaji miji na teknolojia


Na Leandra Oltmanns, Dar es Salaam

WAZIRI Wa Ujenzi Innocent Bashungwa amewataka wapangaji wanaoishi katika nyumba za makazi zinazosimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) kulipa kodi kwa wakati na kuiagiza Wakala hiyo kukusanya madeni kwa wadaiwa sugu wote kwa mujibu wa sheria za mikataba ili fedha hizo zitumike katika ujenzi wa majengo mawili kwa ajili ya watumishi wa Umma (Block C na D,) Magomeni Kota awamu ya pili ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 15.

Akizungumza leo Magomeni Kota, jijini Dar es Salaam katika hafla ya ufunguzi wa jengo moja la ghorofa saba linalobeba Kaya 16 lililogharimu shilingi Bilioni 5.6 Bashungwa amesema; Serikali imeendelea na jitihada za kujenga makazi bora kwa watumishi ili kupunguza changamoto za makazi na kuwataka watumishi waliopata fursa ya kuishi katika nyumba hizo kutimiza wajibu kwa kulipa kodi kwa wakati ili kuiwezesha TBA kujenga nyumba nyingi zaidi katika mikoa mbalimbali nchini kwa kuwa uhitaji wa nyumba bora umefikia zaidi ya nyumba milioni tatu kwa ongezeko la nyumba laki tatu na tisini elfu kila mwaka.

Ameelekeza Wakala hiyo kuendelea kufanya kazi kiwango bora na ubunifu zaidi kwa wakati huu ambao Serikali imerekebisha sheria ya Wakala kwa kutoa fursa kwa TBA kushirikiana na sekta binafsi pamoja na Taasisi za fedha katika uendelezaji milki, kujenga nyumba za makazi kwa watumishi wa Umma pamoja na watanzania kwa ujumla.

Aidha ameipongeza Wakala hiyo kwa kuwa wabunifu katika ardhi na mipango ya majengo ya kisasa katika miradi wanayoisimamia, ambapo katika eneo la Magomeni lenye hekari 32 awali lilikuwa na wakazi 645 na baada ya TBA kusimamia ujenzi na ukadiriaji majengo ekari 9 zimejengwa nyumba za makazi zilizotosheleza wakazi 645.

"TBA inakwenda katika mwelekeo sahihi katika ubora wa majengo pamoja na teknolojia ikiwemo hii ya kitasa janja itakayosaidia kuwadhibiti wanaokwepa kulipa kodi.....TBA chukueni hatua kwa wadaiwa sugu bila kuangalia wadhifa." Ameongeza Bashungwa.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daud Kondoro amesema mradi huo umegharamiwa na Serikali kwa fedha za ruzuku zipatazo shilingi Bilioni 5.687 na utekelezaji wake ulianza Novemba 2022.

Amesema jengo hilo ni la pili kati ya majengo 5 yanayojengwa katika eneo hilo kwa ajili ya makazi ya watumishi wa Umma ambapo jengo moja tayari limekamilika na limepangishwa na hadi kukamilika kwa majengo yote matano jumla ya kaya 80 zitakuwa zikiishi hapo, Na ujenzi wake umezingatia kanuni na misingi ya ujenzi wa majengo ya Serikali.

"Jengo A limekamilika na tayari limepangishwa, jengo B ni hili ulilolizindua leo na majengo mawili C na D ujenzi wake umefikia asilimia 15 na ukamilishaji wa majengo hayo yaliyosalia kadiri ya mpango kabambe uliopo utategemea upatinaji wa fedha." Amesema.

Kuhusiana na ubunifu unaofanywa na Wakala hiyo Kondoro amesema; ujenzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM,) ya 2020/2025 ibara ya 55 (h) inayoelekeza maeneo yaliyorejeshwa Serikali Kuu chini ya Wakala hiyo kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI kuendelezwa kwa kujenga nyumba zinazoweza kubeba familia nyingi (apartments.) bora na za kisasa.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema, uzinduzi huo ni matokeo mazuri ya utendaji kazi TBA chini ya Wizara ya Ujenzi ambao wamekuwa wakitekeleza miradi kwa teknolojia ya ubora na upangaji wa miji.

"Nyumba hizi msiwape wahuni, wanaofanya kazi ya udalali na baadaye kuleta taharuki za madai ya kodi kubwa na gharama nyingine na kuharibu taswira ya eneo hili, nyumba hizi zinapangishwa kwa gharama ndogo ikilinganishwa na kodi ya soko." Amesema.

Aidha amemuomba Waziri wa Ujenzi kuweka mkakati wa pamoja wa kuipanga Dar es Salaam kwa kushirikiana Sekta binafsi akitolea mfano wa maeneo yaliyopo pembezoni mwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere ili kuliweka jiji hilo kuwa moja ya Miji mikubwa Afrika ifikapo 2030.

"Tutumie ubunifu katika kukusanya mapato ili kuendeleza Jiji hili...Tunaweza kuinusuru Dar es Salaam na mafuriko ambayo hadi sasa inahitajika takribani Bilioni 600 kwa TARURA Pekee ili kurudisha miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko; kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tunaweza kujenga nyumba za gharama nafuu na watu wakaishi katika miji iliyojengeka vizuri...Serikali ibaki kufanya marekebisho huku mifuko ya watu binafsi ikiendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya makazi."

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge amesema, wameridhika na utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na TBA katika Manispaa hiyo kwa kuwa imeboreshwa kwa kuzingatia mipango miji na mradi huo wa nyumba za watumishi wa Umma umezidi kupendezesha Manispaa ya Kinondoni pamoja na kupunguza changamoto ya makazi.


Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa (kulia,)akisogeza kitambaa kuashiria ufunguzi rasmi wa nyumba za makazi kwa watumishi wa Umma awamu ya pili zilizojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA.) Katika eneo la Magomeni Kota, kushoto ni Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro. Leo jijini Dar es Salaam

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa nyumba za makazi Magomeni Kota awamu ya pili 'B' zilizojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) na kuiagiza TBA kukusanya kodi kutoka kwa wadaiwa sugu kwa mujibu wa sheria ili fedha hizo zitumike katika ujenzi na nyumba nyingine zaidi. Leo jijini Dar es Salaam.


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daud Kondoro akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa Wakala hiyo inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi ili kupunguza changamoto iliyopo. Leo jijini Dar es Salaam.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa nyumba za makazi Magomeni Kota awamu ya pili 'B' zilizojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) na kueleza kuwa mradi huo ni matokeo chanya ya utendaji kazi wa TBA chini ya Wizara ya Ujenzi. Leo jijini Dar es Salaam.
Matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo.




Share this

Related Posts

Previous
Next Post »