UCHUMI UKIIMARIKA, RIBA BoT YASALIA ASILIMIA 6

July 04, 2024

 •⁠ ⁠Mfumuko wa bei wapungua, Utayari wananchi kulipa kodi waongezeka huku Akiba fedha za kigeni ikiwa ya kutosha


Na Leandra Gabriel,Dar es Salaam

UCHUMI Wa Tanzania umeendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa sera thabiti na maboresho mbalimbali yenye lengo la kukuza uchumi unaotarajiwa kuimarika kwa siku zijazo kutokana jitihada za uboreshaji wa miundombinu hususani reli, barabara na bandari, upatikanaji wa uhakika wa umeme, hali nzuri ya hewa kwa ajili ya shughuli za kilimo pamoja na sera za programu za maboresho.

Hayo yameeelezwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa Benki Kuu (BOT,) anayeshughulikia Sera za Uchumi na Fedha Dkt. Yamungu Kayandabila wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC,) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Tanzania iliyoketi Julai 3, 2024 na kuamua Riba ya Benki Kuu (CBR,) kuendelea kuwa asilimia 6 kwa robo mwaka itakayoishia Septemba 2024.

Amesema, Katika kutathimini mwenendo wa uchumi wa dunia, kamati hiyo ilibaini kuimarika kwa shughuli za kiuchumi katika nchi nyingi kwa robo ya kwanza ya mwaka na pili ya mwaka 2024.

" Mfumuko wa bei umeendelea kupungua pamoja na kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani na benki kuu katika Nchi nyingi kuanza kupunguza viwango vya riba....Bei ya mafuta ghafi ilipungua licha ya kuongezeka kidogo mwishoni mwa mwezi juni 2024, Bei ya dhahabu iliendelea kuwa juu ikiashiria dhahabu kuendelea kutumika kama njia mbadala ya uwekezaji katika mazingira ya kushuka kwa thamani ya sarafu mbalimbali na migogoro ya kisiasa duniani, Na matarajio ni uchumi wa dunia kuendelea kuimarika katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2024 na 2025 licha ya kuwepo kwa hatari kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa na mizozo ya kibiashara." Ameeleza.

Pia amesema, Tathmini iliyofanywa na kamati hiyo kuhusu mwelekeo wa uchumi na vihatarishi mbalimbali inaonesha kwamba, Utekelezaji wa sera ya fedha kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2024 umefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei na kubaki chini ya lengo la asilimia 5.

"Maamuzi ya kamati pia yanazingatia mtazamo chanya wa uchumi wa dunia ambapo matarajio ni kuendelea kupungua kwa mfumuko wa bei katika Nchi nyingi, kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani na kushuka kwa bei ya bidhaa katika soko la Dunia. Na Kamati inatarajia uchumi wa ndani utaendelea kukua kwa kasi sambamba na upatikanaji wa chakula cha kutosha, kupungua kwa kasi ya kushuka kwa thamani ya shilingi kufuatia ongezeko la mapato ya fedha za kigeni yaliyotokana na shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu na mazao ya biashara na chakula." Amesema.

Akieleza kuhusu maeneo mahususi ya mwenendo wa uchumi yaliyofanyiwa tathmini na kamati hiyo amesema ni pamoja na ukuaji wa uchumi ambao ulikua kwa asimilia 5.1 kwa mwaka 2023 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.7 mwaka 2022 ambapo ukuaji huo ulichangiwa zaidi na shughuli za kilimo, uchimbaji wa madini na mawe, ujenzi na shughuli za kifedha hususani ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi.

Aidha shughuli za utalii zimeendelea kuchangia kuimarika kwa uchumi ambapo kamati hiyo imekadiria ukuaji wa uchumi kuwa takribani asilimia 5 na 5.4 katika robo ya kwanza na ya pili ya mwaka 2024.

" Uchumi wa Zanzibar umeendelea kuwa imara, mwaka 2023 ulikua kwa asilimia 7.3 ikilinganishwa na asilimia 6.8 mwaka 2022 na mwenendo huu unachangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za utalii, chakula na uwekezaji kwenye sekta ya ujenzi na mwenendo huu unatarajiwa kuendelea katika nusu ya pili ya mwaka 2024 na 2025." Amefafanua

Pia mfumuko wa bei uliendelea kuwa tulivu na chini ya lengo la Taifa la chini ya asilimia 5, Mwezi Aprili na Mei 2024 mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3 na 3.1 mwenendo uliosababishwa na kupungua kwa mfumuko wa bei ya chakula kufuatia uwepo wa chakula cha kutosha nchini na kwa upande wa Zanzibar mfumuko wa bei umeendelea kupungua hadi kufikia asilimia 5 kutokana na kupungua kwa bei za chakula na bidhaa zisizo za chakula na mfumuko wa bei unatarajiwa kubaki ndani ya wigo wa asilimia tatu hadi nne katika nusu ya pili ya mwaka 2024 na kuendelea.

Dkt. Yamungu amesema, utekelezaji bajeti ya Serikali umeendelea kuwa wa kuridhisha huku ukichagiza utekelezaji sera ya fedha ambapo; mapato ya Tanzania Bara yanakadiriwa kufikia asilimia 95 ya lengo na Zanzibar mapato yakivuka lengo kwa asilimia 0.3 kulikosababishwa na maboresho katika usimamizi wa kulipa kodi na kuongezeka kwa utayari wa wananchi kulipa kodi.

Akifafanua kuhusu akiba ya fedha za kigeni amesema akiba iliendelea kuwa ya kutosha ya zaidi ya dola bilioni 5 zinazotosheleza uagizaji bidhaa na huduma kutoka nje ya Nchi kwa zaidi ya miezi minne huku matarajio yakiwa ni kuongezeka zaidi kwa fedha za kigeni nchini kupitia mapato yatokanayo na shughuli za utalii, mauzo ya madini, bidhaa asilia na usafirishaji wa chakula kwenda Nchi jirani.

Naibu Gavana wa Benki Kuu (BOT,) anayeshughulikia Sera za Uchumi na Fedha Dkt. Yamungu Kayandabila akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC,) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Tanzania iliyoketi Julai 3, 2024 na kuamua Riba ya Benki Kuu (CBR,) kuendelea kuwa asilimia 6 kwa robo mwaka itakayoishia Septemba 2024.

 Matukio mbalimbali wakati wa mkutano huo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »