MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
Baadhi ya Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es salaam wameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa Mradi waUboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaoendelea nchini chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mradi huo ambao unalenga kuboresha usalama wa milki za ardhi nchini, utatekelezwa katika Halmashauri zaidi ya 60 nchini, na umeelezwa kuwa suluhu ya migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiripotiwa katika mikoa mbalimbali.
Wakizungumza wakati wa kikao cha kamati za urasimishaji Ardhi kilichofanyika eneo la Kipunguni Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam April 24, 2024 wananchi hao wamesema serikali imefanya jambo sahihi kwa wakati muafaka.
Mjumbe wa mtaa wa Kipunguni Bw. John Malima Nunda, amesema mradi huo utazirahisishia serikali za mitaa kazi ya kutambua maeneo na mipaka, pamoja na shughuli zinazotakiwa kufanyika.
Kwa upande wake Bi. Sofia Mwalukuta Mkazi wa Kipunguni, ameeleza kufurahishwa kwake na mradi huo ambao amesema ndio suluhu ya migogoro ya ardhi iliyoendelea kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es salaam.
"Hii sasa itaenda kutatua matatizo mengi ambayo tulikuwa tunakutana nayo, lakini pia itaondoa ujanja uliokuwa unafanywa na wachache kujimilikisha maeneo au kubadilisha matumizi halisi ya ardhi" amesema Sofia.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa Mradi wa LTIP Mijini Bw. Leons Mwenda alisema Serikali itaendelea kushirikiana na kamati za urasimshaji ardhi, kwa ajili ya kuhakilisha kuwa zinatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
"Tupo hapa kuwahakikishia kuwa serikali imedhamiria kuona kwamba maeneo yenu yanakuwa rasmi, hivyo kamati hizi zitakuwa bega kwa bega na Serikali katika kila hatu ili kufanikisha mpango huu wenye maslahi makubwa kwa wananchi na Taifa" alisema Mwena.
Kwa upande wake Mratibu wa Ukwamuaji wa Urasimishaji Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul Mbembela, amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kamati na kujitokeza kutoa na kupokea mawazo mbalimbali wakati wote wa mradi.
" Upangaji huu wa maeneo ni shirikishi, jumuishi na wa makubaliano, hivyo wananchi wasisite kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima kwani unawahusu wote" amesisitiza Mbembela.
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi unatekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ukiwa na lengo la kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa kuzingatia makundi maalumu kama wanawake, walemavu, wafugaji, wakulima, wazee na vijana.
EmoticonEmoticon