Na Said Mwishehe, Michuzi TV- Tabora
WAZIRI wa Kilimo Hussein Bashe amezindua Ofisi za Benki ya Meandeleo ya Kilimo(TADB) Kanda ya Magharibi huku akitumia nafasi hiyo kueleza umefika wakati wa kuwa na sera ya fedha katika kilimo lengo likiwa kuwawezesha wakulima kupata mikopo yenye riba nafuu tofauti na ilivyosasa ambapo wanakopa katika benki zenye mlengo wa kibiashara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ofisi za Benki ya TADB Kanda ya Magharibi Mjini Tabora , Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema kanda hiyo inajumuisha Mkoa wa Tabora, Kigoma na Katavi na uwepo wa ofisi za benki hiyo katika kanda hiyo inakwenda kusogeza huduma karibu na wakulima.
Akielezea zaidi kuhusu mikakati ya Serikali katika kilimo amesema pamoja na mambo mengine iko haja ya kuwa na sera ya fedha itakayohusu sekta ya kilimo ambayo itatoa fursa ya wakulima kuwa na uwezo wa kukopesheka kwa urahisi na bila ya kuwepo kwa vikwazo ambavyo vinasababishwa na kutokuwepo kwa sera ya fedha katika kilimo.
"Jambo la pili ambalo nataka niseme na kwa kuwa mwakilishi wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) yuko hapa , mikopo katika sekta ya uchumi wa nchi yetu uchumi wote mikopo inayoingia ni zaidi ya Sh.trilioni 20 na inayokwenda sekta ya kilimo ni asilimia chini ya 10...
"Na bado ukienda kwenye uzalishaji katika kilimo fedha inayotolewa kama mkopo ni ndogo sana.Sasa hoja yangu na nimeshaongea na Waziri wa Fedha , Gavana wa Benki Kuu , Waziri wa Mipango na ninawaandikia barua.
"Tunahitaji sera ya fedha ya kilimo kwani haiwezekani kilimo kikopeshwe kwa kutumia sera za benki za biashara.Kutumia sera hiyo bado hatutoweza kutoa watu kwenye umasikini," amesema Waziri Bashe.
Ameongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anafanya jitihada kubwa katika kuinua sekta ya kilimo na kuboresha maisha ya wakulima akitolea mfano ujenzi wa miundombinu ikiwemo ya kilimo cha umwagiliaji unaofanywa na Serikali.
"Serikali ikashamaliza kuboresha miundombinu mkulima anahitaji fedha ya kununua mbolea , pembejeo na mambo mengine yanayohusu kilimo.Kwa hiyo ni muhimu tukawa na sera ya kupata mitaji kwenye sekta za uzalishaji kilimo, mifugo na uvuvi."
Amesisitiza lazima kuwe na sera inayoeleweka na yeye kama Waziri wa Kilimo atawasukuma wote wanaohusika ili kupata sera hiyo na anaamini itafanikiwa.
Amefafanua katika kipindi kisichozidi miaka miwili Rais Samia ameipatia TADB Sh.Bilioni 632."Sasa ni sheria zipi zinazoisimamia TADB kukopesha ?Kwa sasa ni kama benki za biashara.Hatuwezi, kwa hiyo lazima tutoe maamuzi na nimuombe Gavana , Waziri wa Fedha amenielewa, Waziri wa Mipango amenielewa tufanikishe jambo hili.
"Tutahakikisha tunasukuma tuwe na sera ya fedha katika sekta ya kilimo katika nchi hii ili tuweze kufika mahali ambako tunatakiwa kwenda, " amesema Waziri Bashe huku akitumia nafasi hiyo kuagiza jengo la ofisi za TADB kupewa jina la aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Hassan Mwakasuvi aliyefariki dunia juzi na lengo la ofisi kupewa jina lake ni kuenzi mchango wake mkubwa katika kilimo ndani na nje ya Mkoa wa Tabora.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) Frank Nyabundege amekieleza umuhinu wa ofisi ya TADB Kanda ya Magharibi amesema toka mwaka 2018, mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora ilikuwa ikihudumiwa na ofisi ndogo iliyokuwa Kigoma na baadae kuhamishiwa Tabora.
Ameongeza kwamba hadi kufikia Februari, 2024, TADB imekwisha wezesha wakulima na wafugaji kwa kutoa mikopo yenye jumla ya thamani ya Sh.bilioni 19.59 (Mkoa wa Kigoma, Sh. bilioni 7.209, Mkoa wa Katavi, Sh. bilioni 2.394, na Mkoa wa Tabora, Sh.bilioni 9.996).
"Mikopo hii imetolewa kwenye miradi ya mpunga, chikichi, maharage, mahindi, unenepeshaji wa ng’ombe, tangawizi, ufugaji wa kuku, ufugaji wa nguruwe, na ufugaji wa kondoo. Benki inaendelea kuweka mikakati thabiti ya kukopesha kwenye zao la tumbaku, pamba na asali, kwani mazao haya yanachangia kukuza uchumi wa mkoa wa Tabora."
Aidha ameishukuru Ofisi ya Manispaa ya Tabora, kwa kutupatia jengo hilo la ofisi kwa miaka 33 bure. Hiyo ni ishara kubwa ya ushirikiano kati ya Mkoa wa Tabora na benki yao, hivyo ameahidi jengo hilo kutumika vizuri.
Ameongeza wanatamani kuendelea kusogeza huduma kwa wananchi na endapo ikimpendeza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kutoa jengo Kigoma Mjini bure, anaahidi benki hiyo iko tayari kufungua ofisi ndani ya mwaka huu wa 2024.
Waziri wa Kilimo Husen Bashe akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kilimo nchini(TADB)Frank Nyabundege mara baada ya kuwasili wakati wauzinduzi wa Tawi la benki hiyo mkoani Tabora
Waziri wa Kilimo Husen Bashe akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kilimo nchini(TADB)Frank Nyabundege mara baada ya kuwasili wakati wauzinduzi wa Tawi la benki hiyo mkoani Tabora
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) akomuonesha ramani ya mikoa na wilaya ambayo benki hiyo ipo nchini Waziri wa Kilimo Hussen Bashe wakati wa uzinduzi wa tawi la benki yiyo mkoani Tabora.
Waziri wa Kilimo Hussen Bashe akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tawi la Benki ya TADB Kanda ya Magharibi inayojumuisha Mkoa wa Kigoma, Tabora na Katavi.
EmoticonEmoticon