Na. Peter Haule, WF, Dodoma
Serikali imeeleza kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuweka mazingira bora ya kisera na kimfumo ili kuziwezesha benki za biashara na za kijamii (Community Banks) kukua na kushamiri, ikiwemo Benki ya MUCOBA.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuzisaidia Benki za kijamii kama MUCOBA BANK iliyopo mkoani Iringa ili kukuza uchumi wa wananchi wa hali ya chini.
Mhe. Chande alisema kuwa Hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu ni pamoja na kutafuta mwekezaji mpya wa MUCOBA, ambaye ni Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), kurekebisha kanuni za usajili wa wakala wa benki kwa kuondoa kigezo cha uzoefu wa miezi 18.
Alizitaja hatua nyingine kuwa ni kuanzisha mfuko maalum wa shilingi trilioni moja kwa ajili ya mikopo kwa benki na taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwa wakulima kwa riba ya asilimia tatu kwa mwaka, kutoa unafuu wa kiasi cha amana ambacho benki na taasisi za fedha zinatakiwa kuweka Benki Kuu (SMR) kwa benki zinazotoa mikopo kwa sekta ya kilimo.
Mhe. Chande alisema BoT imepunguza kiwango cha riba kinachotolewa katika akaunti za wateja wa watoa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi (MNOs) kuwa sawa na riba za amana za sekta ya benki na kudhibiti uwiano wa gharama za uendeshaji wa benki na pato la benki usizidi asilimia 55 na mikopo chechefu isizidi asilimia tano ya mikopo yote.
Akijibu swali la nyongeza kuhusu Benki hiyo kusumbuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuchukua fedha zaidi ya milioni 600 kwenye Benki hiyo kupitia Benki ya NMB kwa kisingizio cha Kodi, Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alisema kuwa Fedha hazikuchukuliwa kwa kisingizio cha Kodi bali ilikuwa ni kodi halali.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania imeridhia kukutana na Benki hiyo ili kuona namna bora ya kuwasaidia ili benki iweze kujiendesha na kutoa huduma, hivyo amemuomba Mbunge wa Iringa Mjini kuwataarifu viongozi wa Benki hiyo kuonana na uongozi wa juu wa Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, ili kutatua changamoto hiyo.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu, alietaka kufafanuliwa hatua za kuisaidia Benki ya MUCOBA ambapo inadaiwa kusumbuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuzisaidia Benki za Jamii (Community Banks) kama MUCOBA BANK iliyopo mkoani Iringa ili kukuza uchumi wa wananchi wa hali ya chini.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha)
EmoticonEmoticon