February 15, 2024

 

Dar es Salaam. Tarehe 09 Februari 2024: Baada ya wateja wanne wa Benki ya CRDB kupelekwa nchini Ivory Coast kutizama mechi za ufunguzi za Michuano ya Mataifa Huru Barani Afrika (Afcon), wateja wengine watatu wamepata nafasi ya kwenda kuangalia fainali za michuano hiyo.

Waliobahatika awamu hii ni Bakari Mikidadi kutoka jijini Dodoma pamoja na Veronica Mshometa na Dickson Kabaka wote wa wawili wa jijini Dar es Salaam.

Katika droo hiyo, washindi walipatikana baada ya droo kadhaa zilizochezeshwa wiki iliyopita ambazo ama wateja hawakupokea simu au walipokea lakini hawakukidhi vigezo hasa kile cha kuwa na pasi ya kusafiria iliyo hai.

Akiwaaga washindi hao katika hafla fupi iliyofanyika kwenye studio za Redio ya Wasafi, Mkuu wa Idara ya Huduma za Kadi wa Benki ya CRDB, Farid Seif amesema washindi wa awamu hii wamepatikana kwenye kampeni ya Tisha na Tembocard Tukakiwashe Afcon iliyozinduliwa Novemba 2023 ambayo sasa imehitimishwa baada ya kudumu kwa miezi mitatu ikiwahamasisha Watanzania kutumia kadi zao kufanya malipo ya matumizi wanayoifanya kila siku.
“Kigezo kikubwa cha kushinda zawadi zetu zilizojumuisha samani za ndani, vifaa vya kielektroniki pamoja na safari ya kwenda Ivory Coast kutizama michuano ya Afcon ilikuwa kutumia kadi yako ya Tembocard.

Washindi hawa watatu tunaowaaga leo wamekuwa vinara wa kufanya hivyo kwa mwezi Januari. Tunafurahi kuwaaga wateja wetu hawa wanapoelekea Abidjan kuungana na mashabiki wengine wa soka kutoka kila pembe ya Afrika na dunia kwa ujumla,” amesema Seif.
Licha ya wateja hao wanaoenda Ivory Coast, mteja mwingine, Charles Onesmo Lyimo wa jijini hapa amejishindia samani za ndani pamoja na vifaa vya kielekitroniki hivyo kuungana na Fatima Mwatime Nundu kutoka jijini Tanga alinyakua samani za ndani zinazojumuisha seti ya sofa na meza zenye thamani ya shilingi milioni 8 kwenye droo ya kwanza iliyochezeshwa Desemba 2023 pamoja na Marion Albert Casari aliyeshinda seti ya vifaa vya kielektroniki inayojumuisha runinga, friji na ‘sound bar’ kwenye droo ya pili.

Katika kampeni hiyo ya matumizi ya kadi, Benki ya CRDB ilikuwa inashirikiana na kampuni ya kimataifa ya Visa hivyo washindi waliopatikana watalipiwa kila kitu katika safari yao hiyo  kuanzia malazi, nauli mpaka kiingilio cha uwanjani pamoja na mizunguko yote watakayoifanya nchini Ivory Coast.

“Dunia inaondoka kwenye mfumo wa kulipa kwa fedha taslimu. Benki ya CRDB inachukua kila hatua muhimu kushawishi matumizi ya mifumo mbadala ya kufanya miamala kwa kuwahamasisha wateja wake kulipa kwa kutumia kadi. Ukiwa na Tembocard, unao uhakika wa kununua bidhaa au kulipia huduma mahali popote duniani.
Huna haja tena ya kuhangaika kubadili shilingi ulizonazo au kutembea na fedha taslimu kwani hilo tumeshalifanya ndani ya kadi yako. Tunawakaribisha Watanzania ambao hawajajiunga na huduma zao kuja kupata uzoefu wa aina yake wanapotaka kufanya miamala iwe ndani ya nchi au nje ya mipaka ya Tanzania,” amesisitiza Seif.

Katika awamu ya kwanza, Benki ya CRDB iliwapeleka nchini ivory Coast kushuhudia mechi za ufunguzi wateja wake wanne akiwamo Mbunge wa Morogoro Kusini, Mheshimiwa Hamisi Shaban Taletale pamoja na Evelyne Gasper Rwebugisa na Josephine William Marealle pamoja na Dickson Christian Kabaka wa jijini Dar es Salaam.
Seif amesema zawadi kubwa ya kampeni hii ilikuwa safari ya kwenda nchini Ivory Coast ikilenga kutimiza malengo mawili kwa wateja wao. Kwanza ikiwa ni kuwapa nafasi ya kuungana na mashabiki wenzao wa mpira wa miguu kwani mchezo huo unapendwa zaidi nchini na Afcon ndio michuano mikubwa kwa Bara la Afrika. Pili, amesema ni kuwapa nafasi ya kutanua jiografia kwa kulifahamu zaidi bara lao.

“Nimefurahi kupata fursa hii kati ya wateja wengi wa Benki ya CRDB ambapo katika safari hii mbali na kufika Ivory Coast tutapata nafasi ya kupita na  kukaa Dubai kwa muda kabla ya kuunganisha ndege ya kwenda Ivory Coast. Huu mzunguko nimeupenda, unatoa nafasi ya kushuhudia na kujifunza mengi,” amesema Veronika Mshometa, mmoja wa washindi hao.









Share this

Related Posts

Previous
Next Post »