PPRA YAWAPIGA 'MSASA' WATUMISHI WA MSD KUHUSU MFUMO MPYA WA UNUNUZI WA UMMA KWA NJIA YA MTANDAO (NeST)

February 12, 2024

 Zaidi ya Watumishi 100 wa Bohari ya Dawa (MSD) wanapatiwa mafunzo ya Mfumo mpya wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Mtandao (NeST). Mafunzo hayo yanayotolewa na Mamlaka ya udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) yanafanyika jijini Dar es Salaam kwa Siku Tano.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bw. Mavere Tukai amesema watumishi wa MSD wanapaswa kushiriki na kujifunza kikamilifu mfumo huu ili kuhakikisha mfumo unatatua changamoto mbalimbali za kiutendaji na kuleta tija katika upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.

“ MSD tumewekeza sehemu kubwa katika kuhakikisha mfumo huu unakuwa na tija katika manunuzi ya bidhaa za afya. Tuna timu ambayo inafanyakazi na timu ya kitaifa inayotengeneza mfumo huu ili kuhakikisha unawezesha kwa ufasaha majukumu ya MSD”. Amesema Tukai.

Naye mkufunzi kutoka Mamlaka ya udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) Bw. Castor Claudius Komba - Meneja Mafunzo na Ushauri amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha watumishi wa MSD wanakuwa na uelewa wa hali ya juu katika matumizi ya mfumo huo, kwani MSD ina majukumu nyeti ya kununua bidhaa za afya hivyo mfumo huu haupaswi kuwa kikwazo katika manunuzi ya bidhaa za afya nchini.

Pia Bw. Komba ameongeza kuwa anatarajia kuwa mfumo huo mpya utatatua changamoto zilizokuwepo wakati wa matumizi ya mfumo wa ununuzi wa Taneps.

Mafunzo haya ya Mfumo mpya wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Mtandao (NeST) yanatolewa kwa siku tano kwa watumishi wa MSD wanaotoka Makao Makuu na Kanda za MSD.





Share this

Related Posts

Previous
Next Post »