Benki ya CRDB yafungua tawi wilayani Magu mkoani Mwanza kusogeza huduma kwa wananchi

November 18, 2023

Magu. Tarehe 17 Novemba 2023: Siku chache baada ya kubeba tuzo za huduma bora na mtandao mpana wa mashine za kutolea fedha zinazotoa huduma, Benki ya CRDB imefungua tawi lake jipya wilayani Magu mkoani Mwanza.
 
Tawi hilo linaloifanya Benki ya CRDB kufikisha matawi 262 nchini kote, lilizinduliwa na Kaimu Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mheshimwa Hassan Masala ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Ilemela akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Amos Makalla.
 
Mheshimiwa Masala amesema jitihada za Benki ya CRDB kutanua wigo wake wa huduma zinaonekana na mchango wake utakuwa na tija kubwa kwenye jamii ya taifa zima kwani maendeleo ya kiuchumi yanategemea sana huduma za fedha.
“Tawi hili linaifanya Benki ya CRDB kufikisha jumla ya matawi 19 yanayotoa huduma mkoani mwetu hivyo nawasihi wananchi wenzangu wilayani Magu kulitumia vyema ili kujiinua kiuchumi. Hapa mtatunza fedha zenu kwa usalama zaidi, mtakopa kwa ajili ya biashara au malengo mengine binafsi hivyo kukamilisha mipango yenu kwa wakati. Nawashukuru Benki ya CRDB kwa kuja wilayani hapa, naamini wananchi watanufaika na fursa zenu bunifu zikiwamo za Programu ya Imbeju,” amesema Masala.
 
Akizungumza kwa niaba ya menejimenti, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya CRDB, Godfrey Rutasingwa amesema wateja watapata fursa ya kufungua akaunti zinazoendana na mahitaji yao halisi, mikopo binafsi, ya ujasirimali na biashara,  huduma za bima, kuunganishwa na mifumo ya kidijitali, pamoja na ushauri wa masuala ya fedha na uwekezaji.
 
Tangu ilipoanzishwa mwaka 1996, Rutasingwa amesema Benki ya CRDB imetanua mtandao wake wa huduma kutoka matawi 19 yaliyokuwepo mpaka 262, ukuaji unaoakisi dhima ya dhati ya benki hiyo kusogeza huduma karibu zaidi na Watanzania bila kujali wanaishi mjini au vijijini. 
“Tunakidhi mahitaji ya watumshi na wafanyakazi, wajasiriamali pamoja na wafanyabiashara. Kwa vijana na wanawake, tunayo Programu ya Imbeju inayotoa mtaji wezeshi. Programu hii ni mahsusi kwa makundi haya mawili hasa kwa wale ambao hawajakidhi vigezo vya benki. Ninawakaribisha wana Magu mje kupata huduma zetu,” amesema Rutasingwa.
 
Kwa wapenda michezo hasa mpira wa miguu, Rutasingwa amewaambia wana Magu na Watanzania wote kwa ujumla kuwa wateja waliopo na wale watakaofungua akaunti hivi sasa watapewa TemboCard itakayowapa fursa ya kushiriki kampeni ya 'Tisha na Tembocard Tukakiwashe AFCON' itakayowapeleka wateja 8 nchini Ivory Coast kushuhudia fainali za Michuano ya Mataifa Huru ya Afrika (AFCON).
 
“Safari znima italipiwa na Benki ya CRDB. Washindi watalipiwa kiingilio cha uwanjani na hoteli watakayolala itakuwa ni kwa gharama za Benki. Tunafahamu Watanzania wanapenda michezo hivyo huu ni wakati wao wa kuzitumia kadi zao ili washinde safari hiyo ya nchini Ivory Coast,” amesema Rutasingwa.
Wiki iliyopita, Benki ya CRDB ilishinda tuzo tatu kutoka Consumer Choice Awards Africa (CCAA) 2023 katika vipengele vya huduma kwa wateja, benki yeny emtandao mpana wa mashine za kutolea fedha (ATM) zinazofanya kazi pamoja na mkurugenzi mwenye usahawishi zaidi. 
 
Licha ya matawi yake yaliyoenea nchi nzima, Benki ya CRDB inao zaidi ya mawakala 25,000 wanaotoa huduma mtaani walipo wananchi nchi nzima, ATM 550 na matawi 21 yanayotembea. Vilevile, inazo mashine za ununuzi ya kadi (POS) zaidi ya 6,000 huku ikishirikiana na asasi ndogo washirika (microfinance) zaidi ya 500.
 
Kwa wanaopenda kulipa kidititali, Benki ya CRDB inayo programu ya Simbanking pamoja na huduma kupitia mtandao wa internet “Internet banking.”

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »