NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS),imeandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa matumizi salama ya kemikali,wadau wa biashara na matumizi ya kemikali Kanda ya Ziwa ili kulinda afya za watu na mazingira.
Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa MMS,Daniel Ndiyo,akifungua mafunzo hayo kwa wasimamizi wa kemikali Kanda ya Ziwa jijini hapa leo,amesema yanakwenda sambamba na Malengo Endelevu (SDG),ili kufikia maisha mazuri endelevu kwa wote ifikapo 2030.
“Ili kufikia lengo namba 3, juu ya afya njema na salama,suala la kuzuia au kupunguza madhara ya kemikali katika afya na mazingira ni lazima lipewe kipaumbele pia, kufikia lengo namba 6 linalohusu maji safi na salama lazima kuzuia au kupunguza utiririshaji wa kemikali na kemikali hatarishi katika vyanzo vya maji ili kulinda afya na mazingira,”amesema.
Ndiyo amesema malengo hayo yatafikiwa endapo wasimamizi hao wa kemikali watakuwa na elimu sahihi ya matumizi salama watakayoyazingatia katika maeneo ya kazi kuhakikisha usalama katika jamii inayozunguka maeneo hayo inafahamu matumizi,madhara na faida za kemikali.
“Matumizi na faida za kemikali ni nyingi,hazina mbadala kwa maisha ya mwanadamu na tunaona zikitumika katika sekta za afya,viwanda,kilimo,maji na madini,hivyo zisipotumika kwa kufuata utaratibu zina hatarisha afya na mazingira na baadhi ni sumu kali kama Sodium Cyanide na kemikali za kuunguza ngozi (Hydrochloric Acid,Sulphiric Acid, Caustic Soda TDI na Toluene,” amesema.
Ndiyo ameeleza licha ya madhara makubwa ya kemikali hizo bado ni muhimu katika uchumi wa mtu mmoja mmoja,zinatumika katika mchakato wa uchenjuaji na upatikanaji wa dhahabu na kutokana na faida na sifa katika uchumi pia kuzingatia madhara yanayoweza kusababishwa na kemikali zinazotumika katika sekta mbalimbali,Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali Na. 3 ya mwaka 2003 na Kanuni zake zilitungwa ili kulinda afya,wanyama na mazingira.
“Sheria na kanuni imeweka masharti mbalimbali kuwezesha kemikali kuingia nchini,kuhifadhiwa,kusafirishwa na kuzitumia bila kuathiri afya na mazingira,moja ya masharti ya msingi ni kutoa elimu kwa makundi ya wafanyakazi na jamii iliyo katika hali hatarishi kulingana na aina ya kemikali,”amesema.
Ndiyo amesema ili jamii iendelee kujenga uchumi wa nchi ikiwa salama ndiyo sababu mamlaka hiyo inawaelimisha wasimamizi matumizi salama ya kemikali watoe elimu sahihi katika kudhibiti madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi yasiyo salama katika maeneo yao ya kazi kwa kuzingatia usalama wa nchi.
Mkurugenzi huyo wa Huduma za Udhibiti ameeleza kuwa inawezekana wanauza ama wanatumia bila kufahamu athari ya kemikali,hivyo wasimamizi wakiwa na uelewa mpana wataisaidia kuwaelimisha wateja ni athari zipi zinaweza kutokea wasipozingatia matumizi salama ya kemikali.
“Kanda ya Ziwa ni maalumu kwa shughuli nyingi za uchimbaji na uchenjuaji wa madini hasa dhahabu,hutumika kemikali hatarishi iliyo hatari kwa watu na mazingira ambapo wadau (wasambazaji na watumiaji) zaidi ya 600 wamesajiliwa kulinganisha na wadau 150 miaka mitatu iliyopita,”amesema na kuongeza;
“Elimu hii itakuwa chachu na itawajengea uelewa wa namna ya kuzuia,kujikinga na kujiokoa endapo kutatokea hatari kemikali hizo wakati wa kuzitumia,mtafikisha elimu kwa makundi mengine kulingana na shughuli mnazozisimamia wakiwemo watumishi wa chini yenu pia,mtakuwa mabalozi wa kuwajengea uwezo wananchi karibu na maeneo yenu kutambua kemikali husika,madhara,kujikinga na njia za kusaidia tatizo likitokea”.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Huduma za Udhibiti wamezuia mapipa yaliyotumika kusafirishia kemikali yasiuzwe mtaani bali katika viwanda vya kuzalisha chuma (nondo)na makasha ya plastiki yauzwe katika viwanda vya kurejereza (Recyclig) bidhaa hiyo,watakaokiuka watawajibika kisheria.
Naye,Mkuu wa Kitengo cha Sheria Maabara ya Mkemia Mkuu, Gilbert Ndeoruo,amesema makasha ya kemikali ynayouzwa holela mtaani yakitumika vibaya wahusika watawajibika kisheria ingawa mengine yapo si ya kemikali zikiwemo za majumbani zinatumika bil shida na zipo taratibu za kufuata.
“Wanaokiuka sheria tunazosimamia,kwanza tunawaelimisha na sheria imetupa nguvu kifungu cha 61 (e),mdau anapokiri tunatoa adhabu (faini) na wanaokataa tunawapeleka mahakamani itoe adhabu ambayo ni sh. milioni 2 hadi 5 kulingana na kosa.Rai yetu wadau wazingatiye sheria bila shuruti,huduma zimesogezwa karibu kanda zote,tunatoa huduma kidijitali kupata leseni na vibali kwa wakati,hakuna mtu kutoa visingizio,”amesema
Kwa upande wa baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo Elizabert Chagu wa Buckreef Geita Gold Mine,amesema watumiaji na wauzaji wadogo wa kemikali hawana uelewa wa madhara ya kemikali na kushauri walete watumishi wao wapate elimu waongeze udhibiti.
Kinyogoli Juma wa Prochem Trading Ltd amesema mafunzo hayo yana manufaa makubwa kwa wasimamizi wa kemikali,wamepata uelewa mpana kuwa zisitumike vibaya,hivyo watazingatia sheria za kemikali na matumizi salama na sahihi kuepuka madhara ya kiafya.
EmoticonEmoticon