“NIMEFARIJIKA " DKT. MLIMUKA

July 11, 2023

 NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID

MAKAMU Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Dkt. Aggrey Mlimuka ametembelea banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye viwanja vya Julius Nyerere barabara ya Kilwa na kusema amefarijika kuona Wanachama na Wastaafu wakitoka kwenye banda hilo wakiwa na nyuso za furaha.

Ameyasema hayo Julai 9, 2023 wakati akitoa tathmini yake baada ya kutembelea banda namba 13 la Ushirikiano wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSSSF na NSSF ili kujionea jinsi Wanachama na Wananchi kwa ujumla wanavyohudumiwa.

“Nimefurahishwa kuona huduma zinavyotolewa na wafanyakazi wetu, huduma zote zinazotolewa ofisini zinapatikana hapa,” alisema.

Alisema amefarijika zaidi kuona Wanachama wanaondoka katika banda hilo na nyuso zenye tabasamu na wenye furaha.

Alisema Mfuko umepita katika changamoto lakini sasa PSSSF iko katika hatua za mafanikio.

“hali hii imechagizwa zaidi na hatua za makusudi zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutoa non cash bond, ya trilioni 2.1, fedha hizi zimesaidia sana kuuwezesha Mfuko kuwa katika hali nzuri na hivyo kuweza kulipa Mafao kwa Wastaafu kwa wakati.” Alifafanua Dkt. Mlimuka.

Aliwataka watumishi wa Umma kuendelea kuchapa kazi kwani serikali inajali maslahi yao na iko tayari kutatua changamoto zinazowakabili.

“Tunawahakikishia hakuna haja ya kubabaika, Mafao yenu yanatunzwa vizuri na yako salama, Bodi ya Wadhamini tunafanya kazi kwa umakini mkubwa, jukumu tulilokabidhiwa na serikali yetu tunalitekeleza kwa uaminifu mkubwa na uadilifu mkubwa msiwe na wasi wasi wowote.” Alisisitiza Dkt. Mlimuka.

Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF Bw. Mbarouk Magawa alisema Mfuko ulipoanza miaka mitano baada ya kuunganishwa kwa Mifuko ya PSPF, PPF, GEPF na LAPF, kazi kubwa iliyokuwa ikifanyika ni kuunganisha mifumo ili iweze kusomana.

“Kingine tulichokuwa tunafanya ni kuweza kuwatambua Wanachama wetu, na tuweze kuwaeleza wanachama wajitambue kuwa sasa wao ni wanachama wa PSSSF (culture change) , hilo tumelifanikisha kwa asilimia kubwa sana na sasa Mfuko umeanza kwenda mbele na niwahakikishie wanachama wetu kuwa Mfuko uko imara, Mfuko unaendelea kufanya vizuri na kuimarika zaidi.” Alisema

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi alisema PSSSF imejiimarisha kuhakikisha Mwanachama akiwa amekamilisha nyaraka zake zinazohitajika analipwa Mafao yake kwa wakati ndani ya siku 60 kama sheria inavyoelekeza.

Ingawa Mfuko umejiwekea malengo endapo Mwanachama atakuwa amekamilisha nyaraka zake zote analipwa ndani ya siku 30, anasema Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Bw. James Mlowe.

“Biashara yote tunayofanya mwisho wa siku ni kuhakikisha kwamba Mafao yanalipwa, na Mafao yatalipwa kwa kuhakikisha kwamba kanuni za uandaaji wa hesabu, kanuni za utunzaji wa fedha ziko sahihi, ukaguzi unafanyika kwa kutumia taratibu sahihi,hivyo kupelekea kiasi ambacho kinatarajiwa wakati wowote wanachama wanapostaafu waweze kupata Mafao yao.” Alibainisha Mkurugenzi huyo wa Fedha PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi.

Alisema baada ya kukamilisha mchakato wa kuunganisha Mifuko kwa mafanikio ambapo kazi kubwa ya kuhakikisha wanaweka hesabu sahihi na hesabu zinazoweza kuaminika na umma, kazi iliyopo sasa ni kuwahudumia Wanachama kwa Viwango vya juu vinavyoendana na sheria na kanuni.

“Kwa miaka yote minne na sasa….. tunaelekea mitano,   Mfuko umepata hati safi kutoka ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG,  vile vile tumepata hati ya kutambuliwa uandaaji bora wa hesabu kutoka Bodi ya Hesabu na Ukaguzi (NBAA) kwa miaka minne mfululizo.” Alifafanua.

Kwa upande wao Wanachama wa PSSSF wameonyesha kuridhishwa kwao na huduma zinazotolewa na Mfuko.

“Pensheni yangu naipata kwa wakati muafaka, zile tarehe nilizoambiwa nitakuwa napata Pensheni ndio hizo hizo napata,” anasema Abdallah Mandwanga ambaye ni Mstaafu.

Bw. Mandwanga alisema “Wakati nafuatilia Mafao yangu ya kustaafu nilishughulikiwa vizuri mno,  ninaomba waendelee hivyo hivyo.” Alifafanua Bw. Mandwanga.

“Nayasema haya kutoka moyoni, na sio kuwafurahisha wahudumu hapa, nayasema haya kutoka moyoni na nimeridhishwa sana na huduma zao kwakweli nawapa hongera kubwa.” Alisema Bw. Mandwanga.

Aidha Mstaafu mwingine Bw. Dominic Chanchu alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa nyuma ya mabadiliko haya.

“Sisi tunaona ubora umeongezeka, mama Samia ameboresha hali, sisi tunakula vizuri na tunasema Alhamdullillah, Pensheni inaingia kwa wakati, wastaafu hakuna kulia lia siku hizi labda tu iwe vurugu zetu.” Alibainisha Bw. Chanchu.

MAKAMU Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Dkt. Aggrey Mlimuka (kushoto) akiongozwa na Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe alipotembelea banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ili kujionea utoaji huduma na elimu kwa Wanachama na Wananchi.
Dkt. Mlimuka (wapili kulia) akiongozwa na Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe akijionea utoaji huduma kwa Wanachama na Wananchi wanaotembeela banda la PSSSF. 
MAKAMU Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Dkt. Aggrey Mlimuka (katikti) akiwa na Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe (kulia) wakati akiangalia bidhaa za ngozi zinazozalishwa na kiwanda cha Kilimanjaro Leather International Company Limited, (KLIC) alipotembelea banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ili kujionea utoaji huduma na elimu kwa Wanachama na Wananchi. Kiwanda hicho ambacho kiko mkoani Kilimanjaro, kinamilikiwa kwa ubia kati ya PSSSF na Jeshi la Magereza
Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Bw. Mbarouk Magawa (kulia) akizungumza jambo na Mwanachama wa PSSSF aliyejawa na  furaha
Mkurugenzi wa Fedha PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi (katikati) akishuhudia jinsi Mwanachama wa Mfuko huo (kushoto) akijihakiki kwa kutumia mashine ya Biometric.
Mkurugenzi wa Fedha PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi , akimzawadia Mwanachama wa PSSSF aliyetembelea banda la Mfuko huo.
Kamishna wa Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bi. Suzan Mkangwa (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Afisa Uhusiano Mwandamizi PSSSF, Bi. Fatma Elhady alipotembelea banda la PSSSF.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »