MAELEKEZO YA DKT. SAMIA YAWAVUTIA VIJANA KUJIAJIRI KWENYE UFUGAJI

February 17, 2023
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvui Mhe. Abdallah Ulega (Mb (wa tatu kushoto) akizungumza na vijana waliojiunga mafunzo ya vitendo ya ufugaji kwa tija na biashara na kunenepesha mifugo, kwenye Kituo Atamizi kilichopo Wakala ya Elimu ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Mkoani Tanga, kupitia programu ya Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI). (15.02.2023)



Na. Edward Kondela

Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeamua kukuza sekta ya mifugo kupitia unenepeshaji wa mifugo ili wananchi waweze kufuga kibiashara na kwa tija zaidi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amebainisha hayo (15.02.2023) Mkoani Tanga, wakati alipotembelea vijana waliojiunga kwenye vituo atamizi vilivyopo Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) ili kupata mafunzo ya vitendo ya ufugaji kibiashara na unenepeshaji bora wa mifugo.

Mhe. Ulega amefafanua kuwa kupitia dira na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia, serikali imeonelea kuichangamsha Sekta ya Mifugo, kupitia unenepeshaji na ufugaji wenye tija hivyo wizara kuja na programu ya Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI).

“Tunataka kutengeneza matokeo chanya kwa vijana katika maendeleo yao Rais Dkt. Samia anataka vijana wachakarikaji, wenye kasi ya maendeleo.” Amesema Mhe. Ulega

Nao baadhi ya vijana ambao wanapata mafunzo hayo wamemwambia Naibu Waziri Ulega kuwa wamejiwekea mikakati ya kufanya ufugaji wenye tija mara wakapomaliza mafunzo yao ambayo yanadumu kwa mwaka mmoja.

Wamebainisha kuwa ni wakati wao saa kufikiria kujiajiri na hata kutoa mafunzo kwa wafugaji wengine wa asili ili wafuge kisasa na kuingia katika biashara ya unenepeshaji wa mifugo

Programu ya SAUTI ambayo imeanzishwa kutokana na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyotoa wakati wa kuhitimisha sherehe za wakulima (Nanenane) Mwaka 2022, imelenga kuwabadilisha vijana kifikra kwa kuwapatia mbinu mbalimbali za ufugaji wa kisasa na kibiashara ikiwa ni pamoja na kuwaonyesha fursa zilizopo kupitia Sekta ya Mifugo.

Mwisho.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »