ZAIDI YA WAGONJWA 1000 WAFANYIWA UCHUNGUZI NA KUPATIWA MATIBABU KAMBI YA MADAKTARI BINGWA TANGA

September 27, 2023
Mratibu wa Kambi hiyo ambaye pia ni Mhazini wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt Mathew Shao kulia akiteta wakati wa kambi ya Huduma za Madaktari Bingwa wa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali inayoendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga.

Wananchi wakiendelea kupatiwa huduma mbalimbali wakati wa kambi hiyo inayoendelea kwenye viwanja vya CCM Mkwakwani Jijini Tanga






Na Oscar Assenga, TANGA

ZAIDI ya wagonjwa 1000 wamefanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu katika kambi ya Huduma za Madaktari Bingwa wa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali inayoendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga.

Kambi hiyo iliyoandaliwa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Tanga Mhe. Ummy Mwalimu iliyoanza Septemba 25 mwaka huu na inayotarajiwa kumalizika leo tarehe 27 September ilikuwa ikitoa huduma za kibingwa katika magonjwa mbalimbali.

Akizungumza leo Mratibu wa Kambi hiyo ambaye pia ni Mhazini wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt Mathew Shao alisema mwamko wa wananchi umekuwa kuridhisha kutokana na kuongezeka idadi yao kila siku.

Dkt Shao ambaye pia ni Daktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa alitaja magonjwa hayo ya kibingwa ni Moyo,Sukari,Mifupa,Pua/koo,masikio,wanawake na uzazi,kinywa na meno,watoto ,mfumo wa mkojo(Urojolia) na Macho.

Aliyataja magonjwa mengine ni ya Upasuaji,utoaji wa dawa na vipimo vya sukari,moyo-Echo,ECG,Utrasound,Sickle Cell,Uzito na urefu,hali ya lishe,ukimwi/TB,Ushauri na nasaha na elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza (NCD)

Mwisho.

RC SENYAMULE AIPONGEZA PSSSF KWA KUWASHIRIKISHA WANACHAMA NA WATUMISHI WAKE KUHIFADHI MAZINGIRA, AZITAKA TAASISI NYINGINE KUIGA MFANO HUO

September 26, 2023

 

 

Na Jacquiline Mrisho- MAELEZO

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ametoa rai kwa watumishi hasa wa mkoani Dodoma kuiga mfano wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wa kuhamasisha watumishi wake kupanda miti katika maeneo mbalimbali ili kuendelea kutunza mazingira.

Mhe. Senyamule ameyasema hayo leo mkoani Dodoma wakati akifunga semina ya wastaafu watarajiwa wa Mfuko huo iliyofanyika kwa siku mbili kuanzia Septemba 25 - 26, 2023 mkoani humo.

Mhe. Senyamule ameipongeza PSSSF kwa  kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo mpaka sasa PSSSF imegawa miche ya miti kwa wastaafu watarajiwa na waliostaafu sasa wanafikia 739,000,

"Nimefurahi kusikia kuwa mmewashirikisha watumishi wa PSSSF kwa kuhakikisha kila mtumishi anapanda na kuitunza miche kumi ya miti, kampeni ambayo mmepanga iendelee hadi Disemba 2023 ambako mnatarajia mtakuwa mmepanda miche takribani milioni 7. Mimi na wenzangu mkoani, tunalipokea jambo hili jema kwa mikono miwili na natoa rai kwa watumishi wengine kuiga mfano huu". Amesema Mhe. Senyamule.

Awali Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bi. Beatrice Musa – Lupi amesema kuwa Mfuko huo unatambua na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo umetoa mche mmoja wa mti kwa kila mstaafu mtarajiwa wa PSSSF aliyehudhuria semina wanazozitoa  lengo likiwa ni kila mmoja aweze kuupanda na kuutunza mche aliopatiwa.

"Pia kwa kushirikiana na watumishi wa PSSSF tutaendesha kampeni ya kuhakikisha kila mtumishi anapanda na kuitunza miche kumi ya miti, kampeni hii itaendelea hadi Disemba 2023 ambapo tunatarajia kuwa tumepanda miche takribani milioni moja katika maeneo mbalimbali", amesema bi. Beatrice.

Kwa upande wake Mstaafu mtarajiwa, Mhandisi Salum Omary ameishukuru PSSSF kwa kugawa miti kwa wastaafu watarajiwa ili nao waendelee kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutunza mazingira. Aidha, ametoa rai kwa wastaafu watarajiwa wenzie kuendelea kupanda miti zaidi ya hiyo waliyopewa na PSSSF.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule (katikati), akipokea mche wa mti, kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha, Bi. Beatrice Musa – Lupi, huku Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Bw. Mbaruku Magawa akishuhudia, wakati wa kufunga kikao kazoi cha wastaafu watarajiwa wa PSSSF kilichofanyika jijini Dodoma Septemba 26, 2023.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bi. Beatrice Musa – Lupi, akizunhguzma wakati wa kufunga kikao kazi
Baadhi ya washiriki
Baadhi ya washiriki
Baadhi ya washiriki
Watendaji wa Mfuko
Meza kuu na viongozi wa Mfuko
Meza kuu na watumishi wa Mfuko
Meza kuu na baadhi ya wastaafu watarajiwa wa PSSSF.

MAMIA YA WANANCHI WAJITOKEZA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA UCHUNGUZI TANGA

September 25, 2023
Huduma Matibabu ya Kibingwa zikiendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga 
Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Moi Dkt Hellena Mwijage akizungumza kuhusiana na kambi hiyo ya matibabu
Wananchi kutoka maeneo mbalimbali Jijini Tanga wakipatiwa huduma 

Huduma za upimaji urefu zikiendelea katika kambi hiyo
Sehemu ya Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo wakiendelea wakiwa tayari kuwahudumia wananchi kwenye kambi hiyo


Na Oscar Assenga, TANGA.

MAMIA ya Wananchi kutoka maeneo mbalimbali Jijini Tanga wamejitokeza kwa wingi kwenye kambi ya Huduma za Madaktari Bingwa kwa Uchunguzi wa magonjwa mbalimbali inayoendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani.

Kambi hiyo ya Huduma za Madaktari Bingwa imeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) ambapo siku ya kwanza ya zoezi hilo mwitikio wa wananchi walijitokeza kwa wingi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kupata matibabu wananchi hao walifurahia huduma hiyo huku wakikipongeza chama cha madaktari kwa kuwa na utaratibu huo mzuri kwa wananchi.

Akizungumza mmoja wa wananchi hao Jonas Mwakifuo ambaye ni Mkazi wa Mwanzange Jijini Tanga alisema kwamba huduma ambazo zinatolewa ni nzuri kwa sababu wananchi wengi wanakabiliwa na magonjwa mbalimbali lakini hawana fedha za kuweza kugharamia matibabu.

Alisema hivi sasa kumekuwa na wimbi kubwa la magonjwa mbalimbali ikiwemo tezi dume na mfumo wa mkojo na figo ambayo yamekuwa yakiwatesa wananchi wengi hivyo uwepo wa madaktari hao utawasaidia kuweza kupata matibabu ya kibingwa.

“Kwa kweli tunawashukuru madaktari Bingwa hawa maana hii imekuwa ni faraja kubwa sana kwetu kwa sababu tunapata huduma kwa hakika niwapongeeza madaktari hao kwa kazi nzuri wanayoifanya”Alisema

Kwa upande wake mkazi wa Sahare Jijini Tanga Zuhura Omari alisema kwamba kambi hiyo imekuja wakati muafaka kwani hivi sasa wananchi wengi wamekuwa wakikabiliwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari na uzito mkubwa.

Alisema hivyo huduma hiyo inakwenda kuwa mwarobaini wa kutibu magonjwa hayo hivyo wanashukuru kwa madaktari wote ambao wamefanikisha huduma hiyo muhimu kwao.

Hata hivyo Mariam Saidi ambaye ni mkazi wa Barabara 12 Jijini Tanga alisema kwamba kambi hizo ni muhimu kutokana na kwamba zinawapa fursa wananchi kuweza kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali yanayowakabili kwa muda mchache.

Akizungumza katika kambi hiyo Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Moi Dkt Hellena Mwijage alisema kambi hiyo ni utaratibu ambao wamekuwa wamejiwekea kila wanapoadhimisha Kongamano la Madaktari nchini wanaanza na shughuli za kijamii.

Mwijage alisema kwa mwaka huu Kongamano hilo linafanyika mkoani Tanga hivyo wameanza na huduma za kijamii na wamepiga kambi kwenye uwanja wa Mkwakwani kwa muda wa siku tatu

Hellena ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) alisema kambi hiyo ya uchunguzi kwa magonjwa mbalimbali itakuwa ya siku tatu huku wananchi wakikaribishwa wajitokeze kuweza kupata huduma na matibabu rasmi na muhimu kutokana na matatizo yao.

BILIONI 3.5 ZA RAIS DKT SAMIA ZILIVYOBORESHA HUDUMA ZA AFYA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA TANGA –BOMBO

September 24, 2023

 

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo Dkt Naima Yusuf



Na Oscar Assenga,Tanga.


Ni ukweli usiopingika kwamba huduma za Afya ni muhimu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jamii katika harakati za kujiletea maendeleo na kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Jamii isipopata huduma nzuri za afya inaweza kushindwa kutimiza ipasavyo majukumu yake hususani katika shughuli zake za kila siku za kujiletea maendeleo na hivyo kupelekea kuwa tegemezi.

Kwa kutambua umuhimu wa jambo hilo Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ilipoingia madarakani ilianza na kufanya uwekezaji na maboresho makubwa katika Hospitali mbalimbali za Rufaa,Kanda na Taifa hapa nchini.

Uwekezaji huo umekuwa ni chachu  katika kuboresha huduma kwa watanzania waliopo katika maeneo hayo na hivyo kuwapunguzia mzigo  wa gharama ambazo awali walikuwa wakizipata kufuata huduma hizo kwenye mikoa mengine.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga –Bombo ni miongoni mwa Hospitali za Rufaa hapa nchini ambazo zimenufaika na uwekezaji mkubwa wa Bilioni 3.5 ambao umefanya na Rais Dkt Samia Suluhu hapa nchini katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarika.

Dkt Naima Yusuf ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo anasema wanamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya Afya ikiwemo uboreshaji miundombinu katika Hospitali hiyo.

Anasema kwamba Serikali imewasaidia katika mambo tofauti tofauti ikiwemo ujenzi na upanuzi wa majengo mbapo awali walikuwa wanatoa huduma  muhimu nne ambazo ni pamoja  na ya upasuaji wa kawaida ya watoto,mama na magonjwa ya ndani.

Anaeleza Serikali imewasaidia kujenga jengo la wagonjwa mahututi ,magonjwa ya dharura pamoja na kutanua sehemu ya matibabu ikiwemo ya vijana wanaotumia dawa za kulevya (Methadone) huku miradi mingine ikitarajiwa kujengwa kwenye Hospitali hiyo.

Dkt Naima anaeleza kwamba pia kuna mradi wa damu salama ambapo watakuwa wanapataa huduma ya damu salama kwenye mkoa  na hospitali ya Rufaa ambao utakuwa ni mkombozi kwa wananchi.

Anaeleza kuhusu vifaa tiba anasema Serikali awamu ya sita imewasaidia kununua vifaa tiba vingi vya uchunguzi mpaka vya kutolea matibabu ambavyo ni CT Scan ambayo imeleta huduma ya uchunguzi,vifaa vya dharura pamoja na kuweka fedha kwenye mafunzo ,ujenzi kwa ajili ya watalaamu.

“Uwekezaji huo umegharimu sh Bilioni 3.5 kwa  ujumla ambao umefanywa chini ya mwaka mmoja na hivyo huduma zimepanuka Bombo wagonjwa wengi waliokuwa wakipata rufaa sasa hivi wanapata huduma hapa hapa  hayo ni mafanikio makubwa sana”Anasema Dkt Naima

 “Tulikuwa tunatoa rufaa wagonjwa 50 mpaka 60 kwa wiki mbili lakini kwa sasa  ni chini ya rufaa 25 kwa wiki mbili hayo ni mafanikio makubwa sana na wananchi wa Tanga wanamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu kwa uwekezaji huo mkubwa”Anasema Dkt Naima

Anasema wameweza kupanua huduma za uchujaji wa damu  na  huduma za watoto njiti ambao wanahudumiwa hapo hapo kwa ajili ya vifaa na kupanua huduma za dharura ambazo kwa sasa zimeimarika.

Hata hivyo anasema wameweza pia kupanua huduma ya mkojo kutokana na kwamba unapofikia uzee wapo wanaopata shida ya tezi dume huduma sasa inapatikana ikiwemo zile za macho,pua koo na masikio na meno na huduma mahututi.

“Nikisema huduma za mahututi na dharura tumeweza kufufua wagonjwa waliokuja bila mapigo ya moyo kama watano ambayo hiyo ingekuwa haiwezekani bila kuwa na vifaa tiba msaada huo ambao tumesaidiwa na Serikali utusaidia kufanikisha hayo”anasema

Kuhusu Ajira. Dkt Naima anaendelea  kuishukuru Serikali ya awamu sita kwenye kuwasaidia kuwapelekea waajiriwa wapya 50  kutokana na kwamba hiyo imesaidia kuleta huduma kwenye maeneo walioyapanua kuwa na madaktari ,manesi pamojà na wataalumu katika kada mbalimbali.

“Nakumbuka nilivyoanza hapa Hospitali ya Rufaa ya Bombo mwaka 2008 Bombo kulikuwa na madaktari bingwa chini ya 11 na waliokuwa wanatoa huduma walikuwa wanne tu leo tuna madaktari bingwa 21 kwa kweli ni hii ni pongezi kubwa sana kwake Rais Dkt Samia Suluhu na Waziri wetu wa Afya Ummy Mwalumu”alisema Dkt Naima

Alisema leo wameona umuhimu wa kuwapeleka madaktari na wameweka bajeti ya kuwaongeze ujuzi  madaktari bingwa watano kufikia kwenye Ubingwa Bobezi wanasubiri bajeti ikipita waende kwenye mafunzo na warudi kutoa huduma hapo.

Kuhusu upatikanaji wa Dawa

Dkt Naima anasema kuhusu suala la upatikanaji wa dawa wameongezewa bajeti ya kununua dawa na mfumo wa upatikanaji wa dawa umekuwa mzuri mwanzoni walikuwa wanapata shida kutoka MSD .

Alisema kwa maana dawa nyingi zilikuwa hazipatikana lakini sasa hivi alikuwa amekaa na Meneja MSD  na wameona ongezeko lilivyokuwa sasa hivi imefikia asilimia 57 na dawa nyingi watapa MSD na mlolongo wa upatikjaji wa dawa utapungua.

Hata hivyo Dkt Naima anasema hospitali hiyo inatambua kuwa na madaktari bingwa 21 sio sahihi kubaki tu Hospitalini kuna wananchi wengi wanashindwa kuja hospitaklini Tanga kutokana na umbali wa maeneo ya wilayani hivyo kwakutambua hilo wanakwenda kutoa huduma kwenye hospitali hizo ikiwemo kuwafundisha wataalamu walipo kwa hiyo kwa mwaka wanafanya mara nne na wanajaribu kwenda wilaya zote za Tanga.

Anaeleza kwamba Bombo Hospitali ni miongoni mwa Hospitali za Rufaa 28 nchini ambapo kwa sasa wanajivunia kwenye umahiri wa Plastic Surgery mradi ambao ulianza 2011 kuna madatari wanatoka nchini Ujerumaani kwenye hospitali yao na kufika kwenye Hospitali hiyo ya Bombo wanafanya kliniki za ubobezi za Plastic Surgery.

Anasema hiyo imesaidia watu wengi hapa nchini ambao wakati wa kliniki hizo wamekwa wakijitokeza kupata huduma hiyo na  wamechukua hatua baada ya Waziri kuona kuna umihumu wa kuendelea nayo hapa  hivyo wameanzisha Programu ya  Plastic Surgery unaitwa Tazzy Plastic ambao utakuwa unatoa huduma ndani ya Hospitali.

Dkt Naima anasema huduma hiyo itakwenda sambamba na  kuanzisha program ya kufundisha madaktari ili kuweza kupata madaktari bobezi katika eneo hilo na madaktari wawili wanakwenda kusoma wapo na ushirikiana na Muhas na Muhimbili na watakachokifanya ni  kufanya eneo la Umahiri katika Urekebishaji Viungo(Plastic Surgery) hapa nchini .

Anasema unapoongelea urekebishaji wa viungo sio ya kufanya mtu awe mrembo ila ni watu waliozaliwa mfano mdomo au pua haijaka vizuri au walioungua na mikono yao haijakaa vizuri wanachofanya wanamuweka vizuri ili waweze kufanya kazi kama kawaida na kuirudisha ngozi na kufanya kidonda kukaa vizuri kwa hiyo ni huduma kama hizo.


DKT.BITEKO AANZA ZIARA YA KIKAZI BUKOMBE MKOANI GEITA

September 24, 2023

 --APATA MAPOKEZI MAKUBWA YA WANANCHI


---AAGIZA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA ZA SERIKALI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko ameanza ziara ya kikazi katika jimbo hilo lililoko mkoani Geita ikiwa ni ziara ya kwanza kufanyika  kutoka ateuliwe na kuapishwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.

Mara baada ya kuwasili katika Jimbo hilo tarehe 24 Septemba, 2023, Dkt.Biteko alipokelewa na wananchi wa Jimbo hilo pamoja na viongozi mbalimbali katika Wilaya Bukombe na Mkoa wa Geita.

Akizugumza  katika Mkutano wa hadhara, Dkt.Biteko amemshukuru Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kuona kuwa anaweza kumsaidia katika majukumu aliyokabidhiwa na kuahidi kuwa, atatekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kuwatumikia wananchi ili kuitendea haki imani iliyooneshwa kwake.

Amesema kuwa, chini ya uongozi wa Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kila kitu kilichopangwa kufanyika  kinaendelea kufanyika kutokana fedha anazotoa katika  miradi ya sekta mbalimbali ikiwemo mradi wa umeme wa Julius Nyerere (MW 2115), ujenzi wa Daraja wa Busisi, ununuzi wa ndege, madarasa, vituo vya afya, utalii n.k.

Kutokana na hilo, Dkt. Biteko amewataka watendaji na watumishi nchini kusimamia matumizi sahihi ya fedha za Serikali kwani fedha hizo ndizo zinategemewa na watanzania katika kuwaletea maendeleo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa Mkoa wa Geita wamemshukuru Rais,  Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini Dkt.Doto Biteko katika nafasi hiyo kubwa na adhimu na kwamba wana imani kuwa ataitendea haki nafasi hiyo kutokana na historia yake ya uchapakazi na uadilifu.

Viongozi hao wakiwemo Wabunge na Wakuu wa Wilaya katika Mkoa wa Geita wamemshukuru Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara wilayani Chato, ujenzi wa Chuo cha VETA wilayani Nyang'hwale na upelekaji umeme vijijini katika vijiji vya Mkoa huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesifu juhudi zilizofanywa na Dkt.Biteko wakati akihudumu kama Waziri wa Madini  na kueleza kuwa amesaidia kuinua mchango sekta ya madini katika uchumi wa nchi na ameahidi kuwa ataendeleza misingi hiyo mizuri ikiwemo ya kufanya utafiti wa madini katika eneo lote la nchi ili wachimbaji wachimbe madini kwa uhakika na hivyo kuongeza mapato ya nchi.

Aidha, ameendelea kusisitiza kuwa, hatalifanyia mzaha suala la utoroshaji wa  madini nchini na kwamba wote watakaotorosha madini watachukuliwa hatua za kisheria kwani wanakosesha nchi mapato.

kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amemshukuru Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo shule, hospitali na umeme katika Mkoa Geita.


DC KISARE ASISITIZA TRA KUENDELEA NA MWENDO WA KUKUSANYA KODI BILA VITISHO

September 22, 2023

 

Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mh. Kisare Makori Akiongea na Timu ya Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu waliofika katika Wilaya yake kwaajili yakutoa elimu ya Kodi kwa  Wafanyabiashara wa Mkoa wa Kilimanjaro.Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mh. Kisare Makori Akiongea na Timu ya Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu waliofika katika ofisi zake kwa ajili ya kujitambulisha kabla ya kuanza kwa kwa zoezi la kutoa Elimu ya Kodi ya Mlango kwa mlango kwa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Kilimanjaro


Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kisare Makori amesema kuwa anakumbuka kauli ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo amewataka maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi bila vitisho na hilo linajidhihirisha kwa kusema kuwa siku hizi TRA ni rafiki sana na wafanyabiashara na hilo ni jambo jema na lenye kudumisha uzalendo wa ulipaji kodi wa hiari.

Ameyasema hayo mwanzoni mwa wiki katika ofisi yake iyopo Moshi wakati alipotembelewa na maafisa kutoka TRA Makao makuu walipofika katika ofisi yake kwa ajili ya kujitambulisha kabla ya kuanza ya zoezi la Elimu ya kodi Mlango kwa Mlango kwa wafanyabiashara wa Moshi sambamba na kusikiliza changamoto zao ili waweze kuzifanyia kazi.

Makori amesema kuwa anafurahia kuwepo kwa elimu ambayo itawafikia wafanyabiashara moja kwa moja katika maeneo yao ya biashara na kuwataka wafanyabiashara hao kushirikiana na maafisa wa TRA ili kufikia lengo lilokusudiwa.

“Natoa pongezi kwa hatua waliyofikia Maafisa wa TRA ya kukusanya kodi bila Mitulinga kama maagizo ya Mh. Rais yalivosema kwaajili ya faida ya Nchi yetu na maendeleo ya Taifa letu, pia kama tujuavyo Serikali haina biashara yoyote isipokua kodi, hivyo utoaji wa elimu ni hatua kubwa sana na itaongeza “sovereignty” na uwezo wakulipakodi utaongezeka.”

Nae kiongozi wa zoezi hilo, Afisa Mkuu Elimu kwa Walipakodi na Mawasiliano Lydia Shio kutoka TRA Makao Makuu amesema uwepo wa maafisa ni kutoa elimu ya kodi na kusikiliza changamoto zao ambazo hata wao wanashindwa kuzileta katika ofisi zao hivyo wameamua kuwafata katika maeneo yao ili kujua uhalisia wa biashara zao na kuwakumbusha malipo ya kodi kwa hiari.

“Tumekuja kwa lengo la kutoa elimu kwa Walipakodi na wafanyabiashara wa Mkoa wa Kilimanjaro tukianzia na Wilaya ya Moshi Mjini ili kuwakumbusha walipakodi waweze kujua wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati kwaajili ya kuongeza pato la Taifa, wafanyabiashara wengi wamesema kua huko nyuma walikua wakiwaona maafisa kutoka TRA wanawakimbia na hawajui wanakimbia kwa kosa gani ila kwa sasa hawana haja ya kukimbia maana tukifika wanatusikiliza na kufanya kilichotuleta na wao wanauliza maswali na kuwasilisha changamoto zao kwa ufafanuzi Zaidi ili aweze kulipakodi inavotakiwa”

Mmoja wa wafanyabiashara wa mtumba katika eneo la soko kuu la Memorial Betty Urono ameeleza kuwa yeye anatumia machine ya risiti na inamsaidia sana na angependa kuwaona wafanyabiashara wenzake wanatumia pia ili kulipakodi kwa usahihi na kujenga taifa letu na maendeleo ya nchi.

“mimi natumia machine ya risiti EFD ni nzuri na inasaidia sana katika kutunza kumbukumbu zetu ni nzuri katika bishara yangu, mimi natoa risiti na nawaomba wengine pia watoe risiti kwa faida yao na ya Nchi yetu pia.”

Mkoa wa Kilimanjaro umekua ni moja wapo ya mkoa wenye historia nzuri katika ulipaji na ukusanyaji kodi na kufikia malengo na muendelezo wa gurudumu la kuongeza pato la Taifa na maendeleo kiujumla hii ni kutokana na ushirikiano unaopatikana kutoka kwa wafanyabiashara na taasisi ya TRA ya Mkoa wa Kilimanjaro katika kutimiza malengo ya Serikali yetu katika kuendeleza maendeleo ya Mkoa na Nchi kiujumla.

Benki ya CRDB kuendelea kurahisisha ukusanyaji mapato Hospitali ya KCMC

September 22, 2023

 


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Benki ya CRDB na Hospitali ya Kanda ya KCMC iliyopo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, zimeingia makubaliano ya kuendelea kuifanya Benki ya CRDB kuwa mtoaji wa huduma za fedha hasa ukusanyaji mapato hospitalini hapo.

Azma ya Benki ya CRDB siku zote ni kuhakikisha inatoa huduma bora na shindani zinazokidhi mahitaji ya wateja wake ikiamini kuwa huduma bora, za kisasa, jumuishi na rahisi za fedha ni muhimu kwa maendeleo ya taifa. Hivyo, Benki ya CRDB imewekeza rasilimali zake katika ubunifu wa huduma na bidhaa zake, ikiwamo kuanzisha na kuboresha kiendelevu mfumo wa upokeaji na ufanyaji malipo kwa njia za kieletroniki unaotumika kwenye taasisi tofauti ikiwemo hii ya Hospitali ya KCMC.

Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema Hospitali ya KCMC ni moja ya taasisi za mwanzo kuingia ubia na Benki ya CRDB kutumia mfumo huu wa malipo, mwaka 2014. Ubia huu ulienda sambamba na uzinduzi wa kadi maalum ya malipo ya Hospitali ya KCMC iliyopewa jina “TemboCard KCMC.”

Katika mwaka wa kwanza tangu kuanza kutumika kwa mfumo huo hospitalini hapo, zaidi ya shilingi bilioni 4.1 zilikusanywa na mpaka mwaka 2022, makusanyo hayo yameongezeka mara mbili na kufika shilingi bilioni 8.7 kwa mwaka.

“Tangu tulipoingia mkataba na Hospitali ya KCMC kuanza kuutumia mfumo wetu mpaka mwaka jana, tumeiwezesha Hospitali ya KCMC kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 52.8. Hiki ni kiasi kikubwa kukusanywa ndani ya miaka minane na makusanyo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka,” amesema Raballa.

Raballa amesema katika kuimarisha ushirikiano na hospitali na pia ili kusogeza karibu zaidi huduma kwa wateja wake mwaka 2020 Benki ya CRDB ilifungua tawi hospitaini hapo. Tawi hilo linawafaa pia wafanyakazi wa hospitali, wanafunzi wanaojifunza hospitalini hapa, wagonjwa, wafanyabiashra na wananchi kwa ujumla wanaoishi au kupita maeneo ya hospitali.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya KCMC, Profesa Gileard Masenga amesema kabla hawajaanza kutumia mfumo wa Benki ya CRDB, walikuwa wanakusanya mapato kidogo na kuna nyakati walilipwa hata kwa fedha bandia .

“Kama mnavyofahamu uendeshaji wa hospitali ni wa gharama kubwa, hivyo usimamizi wa mapato ni kati ya vipaumbele muhimu vya hospitali yoyote. Ndio maana leo tupo tena hapa kuuhuisha mkataba wetu ili kuendelea kuwa na ufanisi mkubwa katika ukusanyaji wa mapato yetu,” amesema Profesa Masenga.

Awali, mkurugenzi huyo amesema wahasibu walilazimika kukaa na fedha nyingi kwenye ofisi zao jambo lililokuwa linawaweka kwenye hatari ya kuvamiwa hivyo kupoteza mapato ya hospitali ndio maana mwaka 2004 ilikuwa rahisi kwa menejimenti ya hospitali kushawishika kuingia makubaliano na Benki ya CRDB kutumia teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato na kwamba mfumo huu umeondoa makosa ya kibinadamu kwa kiasi kikubwa hivyo kuongeza makusanyo.

Profesa Masenga pia amesema uhusiano wa Benki ya CRDB na Hospitali ya KCMC hauishii kwenye huduma za benki pekee kwani wao ni miongoni mwa wanufaika wa uwekezaji unaofanywa kwa jamii na Benki ya CRDB.

Profesa Masenga amesema Benki ya CRDB imewajengea eneo la mapumziko kwa wagonjwa na wasaidizi wao, na mara kadhaa imewasaidia vifaatiba na kompyuta ili kuboresha utoaji wa huduma hospitalini.

Kutokana na makubaliana haya, sio hospitali pekee itakayonufaika na mfumo huu bali pia wale wote wanaohudumiwa hospitalini hapa. Malipo sasa yatakuwa yanafanyika kutumia ‘control number’ . Hivyo yeyote anayehudumiwa Hospitali ya KCMC hata hitaji kufanya malipo kwa fedha taslimu, hivyo kuweza kufanya malipo kielektroniki.

Mhudumiwa ataweza kulipa kwa kutumia kadi za benki ikiwemo za Visa na MasterCard, pia ataweza kutumia SimBanking, internet banking na pia CRDB wakala. Malipo haya ya kisasa yanamwezesha mfanya malipo yoyote kulipia huduma ya kwake au ya mtu mwingine moja kwa moja hospitalini, akiwa popote alipo, ndani au nje ya nchi ilimradi awe na control number, ulipo tupo!








TMDA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE KATIKA KIPINDI CHA MIONGO MIWILI

TMDA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE KATIKA KIPINDI CHA MIONGO MIWILI

September 22, 2023

 Na Mwandishi Wetu


MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba ( TMDA) imesema imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yake kwa kuhakikisha jamii inalindwa afya zao na inakuwa salama kutokana matumizi ya dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa nyinginezo zinazohusiana na afya.

Akizungumza leo wakati wa Kikao kazi cha Wahariri na Waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Adan Fimbo amesema katika kipindi cha miongo miwili katika usimamizi wa bidhaa za dawa, vifaa tibana na vitendanishi wanajivunia mafanikio makubwa katika kutoa huduma.

Ametaja baadhi ya mafanikio yaliyokiwa katika kipindi cha miaka 20, ni kuanzishwa kwa Mamlaka ya udhibiti, Kukamilisha ujenzi wa upanuzi wa Maabara ya Dar es Salaam, Kubuni, kuanzisha na kutekeleza mradi wa Duka la Dawa Muhimu (DLDM / ADDO)

Pia kuzindua na kuanzisha Ofisi ya Kanda ya Ziwa, jijini Mwanza (sasa Kanda ya Ziwa Mashariki), kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa - TFDA (sasa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu TMDA na Kanda ya Mashariki)

Ametaja mafanikio mengine ni kuzindua rasmi jengo la Ofisi ya Makao Makuu ya iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa - TFDA (sasa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu TMDA na Kanda ya Mashariki), kuanzisha, kukidhi na kutekeleza mifumo ya utendaji kazi ya kimataifa ya ISO 1901:2018

Pia kupata tuzo ya kuwa taasisi ya kwanza yenye mifumo bora ya utendaji kazi Serikalini (Best Managed Institution in Tanzania), Maabara ya TMDA kuwa na umahiri unaotambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO Prequlified Laboratory) na Kituo cha umahiri wa usajili dawa barani Afrika

Ametaja pia Maabara ya mafunzo ya umahiri kwa Mamlaka za Udhibiti Dawa barani Afrika, Kuanzisha mifumo ya kielekroniki ya utoaji huduma kwa wateja,Kutoa huduma za udhibiti kwa njia ya kielektroniki (automation of regulatory services)

Fimbo ametaja kuimarika kwa makusanyo hivyo kuchangia asilimia 15 ya mapato yake katika gawio la Serikali na kuwa na ziada ya asilimia 70 kama inavyoekekezwa na Hazina

Mengine ni Kukamilisha ujenzi wa jengo la Ofisi ya TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki Mwanza na kuanza kutumi, Kuanzisha mazingira wezeshi na rafiki ya ufanyaji biashar nchini kwa bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA

Pia Kufikia Ngazi ya tatu ya Shirika la Afya Duniani - WHO(WHO Maturity L-3) kwa kuwa na mifumo bora ya udhibiti dawa barani Afrika hivyo kuwa taasisi ya kwanza ya udhibiti na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia ngazi hiyo

Aidha Maabara ya TMDA kupata hadhi ya juu ya ngazi ya nne umahiri wa Shirika la Afya D\uniani, Kubadili jina kutoka TFDA kuwa TMDA, Kukamilisha ujenzi wa jengo la Ofisi ya TMDA Kanda ya Kati Dodoma na kuanza kutumika

Pia Mamlaka kupewa jukumu la udhibiti wa bidhaa za tumbaku,kuanzisha mfumo wa kufuatilia utoaji taarifa za madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kwa njia ya simu

Mafanikio mengine ni Mamlaka kupata Hati safi kwa miaka 20 mfululizo kutokana na ukaguzi wa hesabu za taasisi kwa ukaguzi unaofanywa na ofisi ya CAG na kutimiza miaka 20 ya taasisi katika kulinda afya ya jamii kwa ufanisi.

Akifafanua pamoja na mafanikio tajwa, Mamlaka inaendelea kuboresha huduma zake kwa kuzingatia maoni ya wateja. mathalan, kwa Mujibu wa utafiti uuliofanywa na Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (University of Dar es Salaam Business School) wa Desemba 2020 kuhusu wateja kuridhika na huduma zitolewazo na Mamlaka.

Amesema katika halmashauri 28 kwenye mikoa 14 ya Tanzania, ulibaini kuwa asilimia 47 tu ya wananchi ndiyo wanaifahamu TMDA. Ni dhahiri kwamba matokeo haya yanaakisi mabadiliko ya jina la taasisi yaliyofanyika mwaka 2019.

"Hata hivyo, Mamlaka inatambua mchango wa vyombo vya habari katika kuongeza uelewa wa wananchi kuifahamu Mamlaka.Kwa kuwa upo umuhimu mkubwa wa wadau wote wa TMDA kuifahamu Mamlaka na majukumu yake...

"Wahariri na Waandishi wa Habari wana wajibu mkubwa katika kuhakikisha kuwa Mamlaka inajulikana kwa jamii na Sheria tajwa inasimamiwa kiufanisi, TMDA imekuwa na utaratibu wa kukutana na wadau wake kwa lengo la kuwaelimisha juu ya kazi zake sanjari na majukumu ya kila mdau katika kutekeleza Sheria husika."

Kuhusu suala la uelimishaji jamii limepewa kipaumbele kikubwa na TMDA na ndiyo sababu tumewaita hapa Wahariri walioko mbele yako kwa lengo la kuwashirikisha mafanikio yaliyofikiwa na TMDA ili kujadiliana kwa pamoja namna ya kushirikiana zaidi katika kuhakikisha kuwa soko la Tanzania lina bidhaa zilizo bora, salama na fanisi ili kumlinda mlaji.

Amesema kimsingi, kazi hii sio rahisi na inahitaji ushirikiano wa karibu kati yetu sisi TMDA, waandishi wa habari na wananchi wote kwa ujumla wao.

Ameongeza ni matumaini yao kupitia tasnia ya habari, wataweza kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwapa elimu endelevu ili waweze kufanya maamuzi sahihi wakati wa kuchagua, kununua na kutumia bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA kutoka katika soko.

Kuhusu Kikao kazi hicho amesema mada mbalimbali zimewasilishwa katika kikao hiki ambapo ni matarajio yao kuwa baada ya semina hiyo, washiriki waweze kuelewa vyema nini Mamalaka imetekeleza na katika kuhakikisha sheria na majukumu ya TMDA yanatekelezwa katika kulinda afya ya jamii.

Aidha, kupitia hoja zitakazoibuliwa baada ya mada husika kutolewa, tutaainisha kwa pamoja maeneo ya ushirikiano katika kuielimisha zaidi jamii kupitia vyombo vya habari kuhusu masuala yahusuyo udhibiti wa bidhaa za dawa vifaa tiba na vitendanishi kutokana na ukweli usimamizi wa Sheria hautakuwa na mafanikio kama hatutakuwepo na ushirikishwaji wa wadau wetu hususan vyombo vya habari.

"Ni imani yetu kuwa Wahariri na Waandishi hawa wakirudi kwenye maeneo yao ya kazi wataweza kueneza ujumbe watakaopata leo kwa watu wengi zaidi na hivyo kuwezesha jamii kupata elimu, kujilinda na kutumia dawa, vifaa tiba na vitendanishi vilivyosajiliwa au kupitishwa na TMDA."
Mkurugenzi Mkuu wa TMDA Adam Fimbo akizungumza wakati wa Kikao kazi cha Wahariri na Waandishi wa habari kilichofanyika jijini Dar es Salaam

 Baadhi ya Wahariri wa Habari na watendaji wa TMDA wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, albert Chalamila alipokuwa akizungumza katika kikao kazi hicho.

Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Gaudencia Simwanza akitoa neno la ukaribisho kwa Wahariri wa Habari waliohudhuria katika kikao kazi hicho.

  Baadhi ya Wahariri wa Habari na Watendaji wa TMDA katika kikao kazi hicho. 

Picha ya Pamoja. Kaimu Meneja Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Martha Malle, akitoa mada katika kikao kazi hicho kuhusu Sheria na Kanuni mbalimbali za udhibiti, za Mamlaka hiyo.