Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano
wa Tatu wa Wadau wa Mkonge utakaofanyika Desemba 4, mwaka huu jijini
Tanga.
Kwa mujibu wa
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona katika
taarifa iliyotolewa kwa umma na Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa bodi
hiyo Esther Mbusi, mkutano huo utawakutanisha viongozi mbalimbali wa
kitaifa na Wadau wa Sekta ya Mkonge nchini.
“Napenda
kuwakaribisha wakazi wa Tanga na maeneo jirani kuhudhuria kwenye
Mkutano huo mkubwa wa Wadau wa Sekta ya Mkonge unaofanyika kwa mujibu wa
Sheria ya Na. 2 ya Sekta ya Mkonge ya Mwaka 1997.
“Katika
mkutano huo tunatarajia Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, lakini
viongozi wengine watakaokuwepo kwenye ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.
Anthony Mavunde ambaye atamwakilisha Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe,
viongozi wote wa Mkoa, Waheshimiwa Wabunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa jirani hususani ile inayolima
Mkonge.
“Kama mnavyofahamu, Waziri Mkuu amekuwa
mstari wa mbele na ameshika bendera ya kuhamasisha Kilimo cha Mkonge,
tulianza naye tangu mwaka 2019 hadi mwaka 2021 amekuwa akija Tanga
kuhimiza watu waingie kwenye Kilimo cha Mkonge kwa sababu anafahamu
faida za Mkonge zao ambalo linaweza kubadilisha maisha ya Watanzania kwa
muda mfupi sana, zao la kudumu la uhakika na biashara ya Mkonge ni
nzuri,” amesema Kambona kwenye taarifa hiyo.
Kambona
amesema mkutano huo pia ni fursa kwa Wanatanga kibiashara kwani
kutakuwa na wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali nchini ambao
watahudhuria mkutano huo muhimu kwa maendeleo ya Sekta ya Mkonge nchini.
Pamoja
na mambo mengine, mkutano huo utatanguliwa na Mkutano wa Bodi ya
Wakurugenzi Desemba 2, na Kikao cha Kamati Ndogo ya Maendeleo ya Zao la
Mkonge inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima na
Mwenyekiti Mwenza, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigella
utakaofanyika Desemba 3, wilayani Korogwe jijini Tanga. Kauli mbiu ya
mkutano huo ni; ‘Mkonge ni biashara, wekeza sasa.’
EmoticonEmoticon