MADJS WA DAR KUUWASHA MOTO CLUB BEN BISTRO LOUNGE MKESHA WA MWAKA MPYA

December 29, 2022


 Meneja wa Club Benbistro Hamisi Hassan akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu walivyojipanga kuaga mwaka 2022 na kuukaribisha mwaka 2023 kwa staili ya aina yake ikiwemo kuwashukuru wateja wao kushoto ni Marton wa Club hiyo Sarah Patrick 
Meneja wa Club Benbistro Hamisi Hassan akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu walivyojipanga kuaga mwaka 2022 na kuukaribisha mwaka 2023 kwa staili ya aina yake ikiwemo kuwashukuru wateja wao kushoto ni Marton wa Club hiyo Sarah Patrick 
Marton wa Club hiyo Sarah Patrick  akizungumza namna walivyojipanga kushoto ni Msimamizi wa Club hiyo Silvester Kasembe
Marton wa Club hiyo Sarah Patrick  akizungumza namna walivyojipanga kushoto ni Msimamizi wa Club hiyo Silvester Kasembe
Msimamizi wa Club Ben Bistro Lounge Silvester Kasembe


Na Mwanaidish wetu,Tanga.

MADJS Maarufu kutoka Jijini Dar es Salaam na wakishirikiana na wenyeji wa Jiji la Tanga wanatarajia kuuwasha moto Club Maarufu Jijini Tanga “BEN BISTRO” siku ya mkesha wa kuuaga mwaka 2022 na kuukaribisha mwaka 2023 kwa staili ya aina yake ikiwemo kuwashukuru wateja wao

Akizungumza leo na waandishi wa Habari Jijini Tanga Meneja wa Benbistro Hamisi Hassan alisema kwamba burudani hizo zitaanza siku ya kuuaga mwaka na kuukaribisha mwaka 2023 na wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha wateja wao wanapata burudani kali.

Alisema kwamba Pamoja na uwepo wa burudani hizo lakini wanawashukuru wateja na wadau wao tokea walipoanza mpaka sasa na kikubwa wamejiandaa kikamilifu na vitu ni vingi upande wa jikoni na club huku akieleza watahakikisha pia usalama unaimarishwa lengo kuwawezesha wadau wao na wateja kusheherekea mwaka mpya

“Kikubwa ni shukrani kwa wateja wetu na wadau wanaotusapoti tokea tumeanza mpaka sasa na tunawaambia mkesha wa Jumamosi na Jumampili kutokuwa na burudani kutoka kwa madjs kutoka Dar na tunaufunga mwaka “Alisema

Aidha alisema kwamba wanawahaidia wateja wao kuendelea kuboresha huduma zao ikiwemo kuhakikisha suala la usalama wao linaendelea kuwepo kila wakati na muda wote.

Awali akizungumza Mdau wa Club Benbistro Kamafa Forever alisema kwamba uwepo wa Club hiyo ambayo imekuwa tofauti na zile za awali umewasaidia wapenda burudani Jijini Tanga kupata ladha za uhakika ambazo hapo awali walikuwa wakizikosa

“Kinachofanyika Club Benibistro ni spesho sana na sehemu nzuri ambayo wadau wa burudani wataendea kupata burudani ya kuufunga mwaka na sababu za kupeleka uwepo wa madjs wapya ni kupata ladha tofauti ambazo zitakuwa na vionjo vya aina yake “Alisema

Naye kwa upande wake Matron wa Club hiyo Sarah Patrick alisema kwamba upande wa huduma ipo vizuri sana na wamejipanga kuhakikisha wanawahudumia wateja wao kama ilivyokuwa kawaida na kuhakikisha hakuna mtu ambaye anakosa vinywaji kutokana na aina ya wahudumu wachangamfu waliopo.

Hata hivyo msimamizi wa Club hiyo Silvester Kasembe alisema kwamba mwaka 2023 wanatarajia kufanya mambo makubwa Zaidi na sehemu hiyo ni nzuri ya Kwenda kupata burudani hivyo wanawakaribisha wateja wao kutoka ndani na nje ya Jiji la Tanga.


TANGA UWASA YAPONGEZWA KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI

December 23, 2022




Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa akizungumza mara baada ya kutembelea mradi wa kuboresha hali ya upatikanaji wa maji katika eneo la Mowe unaotekelezwa na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (Tanga Uwasa)
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly akionyesha katika ramani muonekano wa ujezi unaoendelea wa mradi wa kuboresha hali ya upatikanaji wa maji katika mji wa Tanga uliopo kwenye eneo la Mowe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly (katikati) akizungumza jambo na mstahiki meya wa jiji la Tanga Abdurahman Shillow (kushoto) pamoja Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Tanga Meja Mstaafu Hamis Mkoba wakiwa katika ziara ya kutembelea mradi wa maji unaotekelezwa na mamlaka hiyo.



Na Oscar Assenga,TANGA

MAMLAKA Maji safi na Usafi wa Mazingira (Tanga uwasa) imepongezwa kwa namna inavyoendelea kutekeleza na kuboresha mradi wa kuongeza huduma ya maji kwa wananchi katika Mtambo uliopo Mowe unaoghalimu kiasi cha shilingi Bilioni 9.18 ambapo kwa sasa upo katka hatua nzuri ya utekelezaji ukitarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2023. 

Pongezi hizo zilitolewa juzi na Kamati ya Siasa ya CCM pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Tanga ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashimu Mgandilwa wakati ilipofanya ziara kutembelea bwawa la Mabayani pamoja na eneo la Mowe kwenye mtambo wa kusafishia maji ambapo mradi huo utakapokamilika  unatarajiwa kuboresha huduma ya maji ikiwemo pembezoni mwa jiji la Tanga pamoja na wilaya za Pangani na Muheza. 

Akizungumza mara baada ya kutembelea na kujionea mradi huo pamoja na Bwawa la Mabayani Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashimu Mgandilwa alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani ambaye aliridhia na kutoa fedha Shilingi Bilioni 9.9  kwa ajili ya mradi huo ambao umelenga kupunguza au kuondoa kabisa adha ya maji iliyopo ndani ya jiji la Tanga. 

"Tanga ni moja ya miji ambayo inakuwa kwa kasi sana, sasa ukuwaji wa mji wa Tanga unatakiwa kwenda sambamba na ukuwaji wa miundombinu mingine na hiyo ikampendeza Rais wetu Samia Suluhu Hassan kutoa fedha kwaajili ya Mradi tunaamini baada ya kukamilika kwa mradi huu sasa Tanga inakwenda kutatua kabisa tatizo la maji " alisema Mgandilwa.

Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga (CCM)  Meja Mstaafu Hamis Mkoba ameishauri mamalaka ya maji na usafi wa mazingira (Tanga Uwasa) kuhakikisha inazidi kutatua na kuondoa kabisa changamoto ya kukatika katika kwa maji hii ikiendana sambamba na ukuwaji wa mji wa Tanga ambapo wananchi wanazidi kuongezeka.

 "Tumeridhika kama chama cha mapinduzi kwamba kazi hii inaenda vizuri, ili kusudi matatizo ya kukatika katika kwa maji yasitokee tulikuwa tunawashauri muwe na mipango ya muda mrefu sana ushauri wetu kama chama kwa mamlaka pamoja na kuwapa watu taarifa panatokea changamoto ya kukatika kwa maji lakini tunawapongeza sana Tanga Uwasa kwa jitihada nilizoziona ambazo zinaendelea vizuri kama tutaendelea hivi ninaamini Tanga tutakuwa hatuna shida ya maji" Alisema Meja Mkoba 

Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Tanga uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly alisema kuwa miradi wanayoitekeleza katika kituo kikubwa cha kutibu maji cha Mowe ina lengo la kuboresha hali ya upatikanaji wa maji inaendele vizuri ambapo ifikapo mwezi January 2023 wanatarajia kuanza kuyafanyia majaribio ya kupeleka huduma ya maji kwa wananchi. 


Mamlaka hiyo kwa sasa ipo kwenye mchakato wa kuboresha mtambo wa kusafisha maji katika kituo kikubwa cha Mowe pamoja na kujenga tanki za kuhifadhia maji ambazo zitasaidia kupeleka maji kwa wananchi hata panapotokea changamoto ya kukatika kwa umeme au uzalishaji wa maji kupungua kutoka kwenye vyanzo vinavyoyegemewa . 

"Hali ya utekelezaji mradi mpaka sasa tunaenda vizuri na tunatarajia kwamba mpaka mwishoni mwa mwezi huu December na mwanzoni mwa January miradi yote itakuwa imekamilika na January mwishoni tunatatajia kufanya majaribiao ya kutumia mradi mpya ambao tumeujenga, lengo kuu hasa ni kuboresha hali ya upatikanaji wa maji kwa jiji letu la Tanga lakini pia maji haya yataweza kuhudumia mji wa Muheza pamoja na vijiji vya njiani" alisema Hilly.

 Alisema kuwa changamoto ya kukatika kwa umeme inaathiri utendaji wa mamlaka hiyo katika kuwafikishia wananchi huduma ya maji ikisababisha kusimama kwa kazi za uendeshaji wa mitambo ya kuzalisha maji ambapo hata hivyo mamlaka ipo kwenye hatua za kuongea na shirika la umeme Tanzania TANESCO katika kuona njia bora ya itakayotumika kuondokana na adha hiyo.

 "Kuna changamoto ya umeme kipindi hiki ambapo inasababisha mitambo yetu ishindwe kuendeshwa hivyo kusababisha upatikanaji wa maji kuwa hafifu sana, sasa hivi tuna tatizo la kukatika kwa umeme kwa takribani masaa matatu hadi matano kwa siku na inaathiri sana uendeshaji wa mitambo"

 " Kwa sasa tuna changamoto ya kutokuwa na tanki kubwa la kuhifadhia maji kwahiyo umeme ukikatika pia na hali ya upatikanaji maji baada ya masaa mawili au matatu hali inakuwa ni tete kwa wananchi lakini tuko katika mipango ya kuongea na Tanesco waangalie namna gani ya kutusaidia lakini pia sisi tupo katika mipango ya kutafuta vifaa madhubuti vya kudhibiti mapungufu ya umeme" alisema Mkurugenzi huyo. 

Bwawa la Mabayani ambalo ni moja wapo ya chanzo kikubwa kinachotegemewa na mamlaka ya maji na usafi wa mazingira (Tanga uwasa ) katika kuwahudumia wananchi wa jiji la Tanga lilianza kujengwa mnamo mwaka 1976 hadi 1978 likiwa na ujazo wa mita bilion 7.7 kwa sasa ,ambapo lina uwezo wa kuzalisha maji lita Milion 30 kwa siku. 

WAZIRI NDAKI ASEMA MABORESHO YA MWONGOZO WA UWEKEJI HERENI YATAMFIKIA KILA MDAU

December 21, 2022
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.  Mashimba Ndaki  akizungumza (20.12.2022) wakati akifunga mkutano wa Wadau wa sekta ya Mifugo uliofanyika kwa siku mbili kwenye jengo la PSSSF, Makole jijini Dodoma



Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda akifafanua moja ya maazimio yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa wadau wa sekta ya Mifugo uliofanyika Disemba 19-20, 2022 kwenye jengo la PSSSF Makole, jijini Dodoma.
 Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Mbaraka Stambuli akisoma maazimio yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa wadau wa sekta ya Mifugo uliofanyika Disemba 19-20, 2022 kwenye jengo la PSSSF Makole, jijini Dodoma.




Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.  Mashimba Ndaki amebainisha kuwa Wizara yake inaendelea kufanya maboresho ya Mwongozo unaosimamia zoezi la uwekaji wa hereni za kielektroniki kwenye mifugo ili kufanya zoezi hilo kuwa shirikishi kwa pande zote zinazohusiana na sekta ya ufugaji.

Mhe. Ndaki ameyasema hayo jana (20.12.2022) wakati akifunga mkutano wa Wadau wa sekta ya Mifugo uliofanyika kwa siku mbili kwenye jengo la PSSSF, Makole jijini Dodoma ambapo amebainisha kuwa mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuboresha mwongozo huo utakabidhiwa kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu ili atoe hatma ya zoezi hilo.

“Kwenye maboresho ya mwongozo huu tutamfikia kila mdau anayehusika na sekta ya mifugo kwa nafasi yake ili baada ya kukamilika kwake kusiwe na malalamiko ya baadhi ya wadau kutoshirikishwa” Amesisitiza Mhe. Ndaki.

Mhe. Ndaki ametoa rai kwa wafugaji wote walioshiriki kwenye mkutano huo kuwafikishia wafugaji wenzao elimu waliyoipata kupitia mada mbalimbali zilizowasilishwa wakati wote wa mkutano huo ili waweze kutekeleza kwa pamoja maazimio yaliyofikiwa.

“Ni lazima wote kwa pamoja tuelewe sekta ya Mifugo inapaswa kwenda kwenye mwelekeo mpya, hatuwezi kuwa walewale kwa sababu tunalazimishwa kubadilika sasa hivi kwa namna yoyote ile kutokana na mazingira tuliyopo, mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la watu” Amesema Mhe. Ndaki.

Akizungumzia kuhusu marufuku ya uingizwaji wa vifaranga vya kuku kutoka nje, Mhe. Ndaki amesema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo ili kuwalinda wawekezaji na wafanyaiashara wa ndani ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan zinazolenga kuongeza idadi ya wawekezaji nchini.

“Lakini natoa rai kweu mhakikishe mnaboresha mazao yenu ili yawe shindani kwenye masoko ya ndani na nje kwa sababu hivi sasa tupo kwenye ushirikiano wa Afrika Mashariki na hivi karibuni tutaingia kwenye sarafu moja hivyo ni lazima mjipange” Ameongeza Mhe. Ndaki.

Akizungumzia ubora wa nyama inayozalishwa hapa nchini na namna inavyokubalika katika masoko ya nje, Mkurugenzi wa Kiwanda cha kusindika nyama cha Eliya kilichopo mkoani Arusha Bw. Irfhan Virjee amesema kuwa kwa sasa nyama inayozalishwa hapa nchini na kusafirishwa kwenye masoko ya nje ina ubora na kuhitajika hasa kwenye soko la nchi za falme za kiarabu  kiasi cha kushindwa kukidhi mahitaji ya soko hilo.

Naye Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la kimataifa la Heifer ambao ni moja wa wadau wakubwa kwenye sekta ya Mifugo nchini Bw. Mark Tsoxo amesema kuwa ili kufanikisha  mwelekeo mpya wa sekta ya Mifugo ni lazima Serikali na wadau wote kufanya mabadiliko ya teknolojia na mifumo inayoratibu sekta hiyo.  

“Jambo jingine ni muhimu kuhakikisha kwenye mwelekeo huu mpya wa sekta ya Mifugo tunawajumuisha kwa kiasi kikubwa vijana ambao wanakadiriwa kufikia asilimia 31 ya idadi ya watu wote nchini  na wanawake ambao ni asilimia 51 ya idadi ya watu wote waliopo nchini, kinyume na hapo tutatengeneza changamoto kubwa wakati tukitekeleza mwelekeo huu” Amesisitiza Bw. Tsoxo.

Mkutano huo wa wadau wa sekta ya Mifugo ulifunguliwa Disemba 19 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambapo wadau mbalimbali walioshiriki mkutano huo walifanikiwa kutoa maoni mbalimbali yaliyolenga kutekeleza kauli mbiu ya Mkutano huo ya “ Mwelekeo Mpya wa Sekta ya Mifugo nchini  


NHC TANGA KUWAONDOA KWENYE NYUMBA ZAO WAPANGAJI WENYE MADENI SUGU

December 09, 2022

 Meneja wa Shirika la Taifa la Nyumba(NHC) Mkoani Tanga  Mhandisi Mussa Kamendu  akizungumza na waandishi wa habari
Meneja wa Shirika la Taifa la Nyumba(NHC) Mkoani Tanga  Mhandisi Mussa Kamendu  akizungumza na waandishi wa habari



 Na Oscar Assenga,Tanga


SHIRIKA la Taifa la Nyumba Mkoani Tanga (NHC) limesema kwamba wapangaji wenye madeni sugu iwapo watashindwa kulipa mpaka mwezi Desemba mwaka huu mapema mwakani watalazimika kuwaondoa kwenye nyumba zao kupitia madalali ambao wameingia nao mkataba wa kukusanyia madeni hayo.

Hatua hiyo inatokana na kampeni ambayo waliianzisha ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Octoba-Desemba kuhakikisha wapangaji wanaodaiwa wanalipa madeni yao huku akieleza baada ya kupita muda huo watalazimika kuchukua hatua hizo.

Hayo yalisemwa na Meneja wa Shirika la Nyumba Mkoani Tanga  Mhandisi Mussa Kamendu wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ambapo alisema kwa mkoa wa Tanga wana dalali wanaowasaidia kukusanya madeni kwa niaba ya Shirika hilo

Mhandisi Kamendu  alisema kwamba utaratibu ulipo mtu akiwa anadaiwa kodi shirika huwa linamwandikia notisi ndani ya  siku 30 kumjulisha kwamba shirika litavunja mkataba iwapo deni lake hatalipwa ndani ya kipindi hicho .

Alisema baada ya kupita muda huo shirika huwa linampa kazi dalali ambaye wameinga naye mkataba kwa kumpatia orodha ya watu ambao katika siku 30 ambazo wamewapa hawajalipa madeni yao na dalai wanatoa notisi siku 14.


" Deni lao likishaenda kwa Dalali wao wanakuwa wanamsubiri akusanye hilo yule mpangaji anabaki yeye na dalali waendelea na zoezi la kudai ikishapita siku 14 kama hajalipa kinachofuata anatolewa kwa nguvu kwenye nyumba kwa kukamatiwa mali zake ambazo dalali atakaa nazo kwa kipindi fulani huku akimjulisha aliyekamatiwa vitu  vyake alipe deni ili kuweza kufidia kodi anayodaiwa kama hajalipa dalali atauza hivyo vitu kuweza kupata pesa ya kulipa deni la nyumba "Alisema

Hata hivyo Meneja huyo alisema kwa mkoa huo wana dalali anaitwa Cops Option Mat hao ndio wanawakusanya  madeni kwa wadaiwa sugu waliopo kwenye mkoani humo.

Meneja huyo alisema kwamba kwa mkoa huo malimbikizo ya madeni mpaka mwezi Novemba mwaka huu ni zaidi ya Milioni 105 ambapo kati yao ni watu binafsi,taasisi za Serikali,binafsi na nyengine mbalimbali.

Alisema kulikuwa na wapangaji ambao waliwatoa na baada ya hilo zoezi waliweza kulipa na wengine wanaendelea kulipa hivyo wanategemea mwitikio utaendelea kuwa mzuri wa kulipa kodi wanaodaiwa.

Mwisho.

DAS KOROGWE AFUNGUA MAFUNZO YA MRADI WA SHULE BORA ATOA NENO WANAHABARI MKOANI TANGA

December 07, 2022


KATIBU Tawala wa wilaya ya Korogwe (DAS) Rahel Mhando akizungumza wakati akifungua mafunzo ya mradi wa shule Bora kwa waandishi wa habari mkoa wa Tanga.


Na Oscar Assenga,KOROGWE

MAFUNZO ya mradi wa Shule Bora kwa waandishi wa Habari Mkoani Tanga yamefanyika wilayani Korogwe huku Katibu Tawala wa wilaya ya Korogwe Rahel Mhando akiwataka wanahabari kutumia kalamu zao vizuri katika kuelimisha jamii juu ya mradi wa shule bora wakizingatia taratibu, kanuni sheria zinazowaongoza katika taaluma yao

Ambapo alisema ili kuweza kuboresha na kufanikisha malengo ya mradi wanaamini mawasiliano kupitia vyombo vya habari ni nyenzo muhimu sana ili kuifikia jamii kubwa zaidi.

Alisema hivyo ni jukumu lao kuhakikisha taarifa zote za shughuli za mradi na maendeleo yake katika mkoa wa Tanga ni lao wote hivyo kila anatakiwa kutekeleza jukumu hilo kwa uhakika , weledi na kwa uadilifu kwa lengo la kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu iliyobora "alisema Mhando.

Hata hivyo akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Elimu Mkoa wa Tanga Newaho Mkisi alisema ujio wa mradi huo utakuwa chachu ya kwenda kusaidia na kuongeza kiwango cha ufaulu hatua ambayo itakwenda kuuwezesha mkoa kupata fedha zaidi zinazotolewa na serikali kupitia mradi wa lipa kwa matokeo 'Ep for

Alisema fedha hizo hutolewa kulingana na vigezo na masharti yaliyowekwa na seikali zikiwa na lengo la kuendelea kuweka mazingira rafiki katika sekta ya elimu hapa nchini.

Hata hivyo alisema kwa mkoa huo wa Tanga ufaulu umeongezeka ukilinganisha na wa mwaka jana ukilinganisha na mwaka huu japo sio kwa wastani mkubwa kwenye mradi wa EpforR walikuwa wanashindwa kupata fedha nyingi kwa sababu ya kushindwa kufikia vile vigezo vilivyowekwa ikiwemo ufaulu .

Aliongeza kwamba ili waweze kupata ufaulu mzuri lazima wafanye kazi kwa kushirikiana tukikidhi hivyo vigezo tunapata fedha zaidi abazo zitasaidia katika maswala ya elimu

Mikoa itakayonufaika na mradi huo wa shule bora kwa kipindi chote cha utekelezaji kwa miaka 6 ni Tanga, Dodoma , Pwani , Katavi, Kigoma , Mara, Rukwa , Singida na Simiyu

Naye kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Shule Bora Mkoa wa Tanga Thomas Aikaruwa alisema lengo la mradi huo ni kuboresha na kuinua kiwango cha elimu kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya awali hadi darasa la saba unatarajiwa kutekelezwa kwenye mikoa tisa nchini kwa kwa kipindi cha miaka 6 .

Utekelezaji wa mradi huo unafanywa na serikali ya Tanzania kwa ufadhili wea serikali ya uingereza umelenga pia kuboresha ufundishaji kwa walimu, kuboresha elimu jumuishi kwa makundi ya watoto wenye mahitaji maalum , kuboresha ujifunzaji kwa wanafunzi pamoja na kuboresha mfumo wa usimamiaji wa sekta ya elimu katika kuhakikisha kila kiongozi anawajibika ipasavyo kwa nafasi yake ili kufikia adhima iliyokusudiwa.

Alisema mradi huo unakusudia kuongeza muda wa miaka mitatu ambapo itatokana na matokeo yatakayopatikana kwa kipindi chote cha utekelezaji.

Alisema kwamba mradi huo una lengo la kuondoa changamoto zinazowakabili watoto wengi kushindwa kusoma, kuandika na kuhesabu vizuri, tatizo la utoro mashuleni, kupambana na mimba za za utotoni.

Alieleza pia mradi huo utawapa fursa watoto wenye mahitaji maalumu katika kuendelea na elimu ya sekondari ambapo wengi wao wamekuwa wakishindwa kuendelea kutokana na vikwazo mbalimbali.

“Hivyo kwa kutambua mchango wenu kama wana habari kwani ni wadau muhimu katika mradi huo na maendeleo ya sekta ya elimu kwa ujumla hapa nchini tunatarajia kuifikia jamii katika kuwaelimisha, kuhamasisha kwa kupitia vyombo vya habari matarajio yakiwa ni kuweza kuleta matokeo chanya ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanapatikana”Alisema

Aidha alisema matarajio yao makubwa ni kuona elimu ya msingi inaboreka hivyo wanategemea baada ya miaka ya utekelezaji wa mradi wuone hali tofauti kwenye mikoa hii 9 katika sekta ya elimu ikiwemo mahudhurio ya watoto mashuleni yanaboreka,kujua kusoma na kuandika vizuri kabisa , tuone watoto wa kike wakiwa wanapata fursa sawa sawa na watoto wa kiume na watoto wenye mahitaji maalumu wanaendeleea na elimu ya sekondari.

Akizungumzia lengo la kutoa semina kwa waandishi wa habari alisema kwamba wameona wafanye hivyo kutokana na kwamba ni wadau muhimu hivyo wakaona ipo haja ya kufanya nao kazi katika kuelimisha kuhusiana na mradi huo ili nao waweze kuieleza jamii.


Hata hivyo Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari mkoa wa Tanga( Tanga Press Club) Burhan Yakub alitoa shukrani kwa waandaaji wa mafunzo hayo ambayo yataleta tija kwa waandishi katika kuendelea kuuhabarisha umma.


Alisema kwa uzoefu uliopo kwa waandishi katika kuandika habari za elimu, imeonekana Tanga kuingia kwenye mradi huo ni tofauti ya matokeo ya darasa la saba.

Makamu Mwenyekiti huyo alisema tatizo ni  kwamba wananchi wengi wanaona shule siyo zao kwamba shule ni ya mwalimu na mwenyekiti wa kijiji, na hii inatokana na kukosekana kwa uwazi na ushirikishwaji, unaweza ukakuta hata hizo fedha zinzoletwa kutoka serikalini hawapati taarifa na ndiomaana wanaona hakuna umuhimu wa kuchangia hata chakula shuleni.

DC TANGA ALISHUKURU SHIRIKA LA BRAC MAENDELEO TANZANIA KWA KUWAKOMBOA WASICHANA KIELIMU

December 07, 2022




Mkuu wa Wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa akizungumza wakati akifungua wa kikao cha wadau cha kujadili na kutathimini mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa miaka minne uliokuwa unaotoa elimu, uwezeshaji na stadi za maisha ( Education Empowerment and Life Skills for Adolescent and Young Children -EELAY) Mkoa wa Tanga tangu Juni 2018 hadi Desemba 2022. kulia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdurhaman Shiloo 
Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdurhaman Shiloo wakati akifungua wa kikao cha wadau cha kujadili na kutathimini mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa miaka minne uliokuwa unaotoa elimu, uwezeshaji na stadi za maisha ( Education Empowerment and Life Skills for Adolescent and Young Children -EELAY) Mkoa wa Tanga tangu Juni 2018 hadi Desemba 2022
Meneja awa Mradi huo kutoka Shirika la Brac Maendeleo Tanzania Hope Jassson akizungumza wakati wa kikao hicho
Meneja awa Mradi huo kutoka Shirika la Brac Maendeleo Tanzania Hope Jassson akizungumza wakati wa kikao hicho
Afisa Elimu Msingi Jiji la Tanga Kassim Kaonekana akizungumza
Mmoja wa wanafunzi walionufaika na mradi 
Maafisa wa Shirika la Brac Maendeleo Tanzania mkoani Tanga wakiwemo na wadau wengine
Wadau wakiwa kwenye kikao hicho
Sehemu ya wadau wa kikao hoicho
Waheshimiwa madiwani wakiwa kwenye kikao hicho


Na Oscar Assenga,TANGA.


Mkuu wa Wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa amelishukuru Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania kwa kuwakomboa Mabinti na Wasichana ambao hawakupata elimu kupitia mfumo maalumu,

Mgandilwa aliyasema hayo wakati wa kikao cha wadau cha kujadili na kutathimini mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa miaka minne uliokuwa unaotoa elimu, uwezeshaji na stadi za maisha ( Education Empowerment and Life Skills for Adolescent and Young Children -EELAY) Mkoa wa Tanga tangu Juni 2018 hadi Desemba 2022.

Mradi huo ulikuwa na vipengele viwili muhimu,kipengele cha kwanza kinalenga wasichana walioko kwenye rika balehe wenye umri kati ya miaka 15-24 kwa kutoa elimu ya Sekondari ,mafunzo ya stadi za maisha na fursa za ajira kwa wasichana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu kwa kutumia programu ya muda mfupi yenye matokeo chanya kusaidia wasichana katika kukamilisha miaka minne ya elimu ya Sekondari ndani ya miaka miwili.

Alisema kwamba wanashukuru sana kwa mradi huo ambao unawaachia urithi mkubwa wa elimu kwa Watoto hivyo wap kama Serikali wanawaomba wakakae chini watathmini upya kisha warudi tena katika Mkoa huo na Halmashauri ya Jiji la Tanga kuendelea.

Alisema miradi yote ambayo inaachwa na mradi huo itaendelezwa na kwamba hakuna mradi hata mmoja ambao utatelekezwa huku akiwakikishia kuwa miradi yote itaendelezwa kwa gharama yoyote ile na Serikali itasimamia kuhakikisha watoto wanaendelea kupata elimu.

Awali akizungumza Meneja awa Mradi huo kutoka Shirika la Brac Maendeleo Tanzania Hope Jassson alisema kwamba hadi sasa zaidi ya Wasichana 900 ambao hawakufanikiwa kupata Elimu katika mfumo maalumu wa Elimu ya upili ( Sekondari) wamefanikiwa kupata Elimu hiyo kupitia Mradi wa Elimu na Stadi za Maisha unaotekelezwa  katika Mkoa wa Tanga.

Hope alisema Shirika hilo Chini ya Ufadhili wa Shirika la Norad la Nchini wamefanikiwa kuwapatia Elimu ya Sekondari Mabinti hao zaidi ya 900 chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,

" Asilimia 86.8 ya Wasichana walioko kwenye Rika Balehe wamefaulu na kupewa Cheti Cha Elimu ya Sekondari kuanzia Mwaka 2017 Hadi 2021, Vituo 30 vya Masomo vinaendelea ya Elimu chini ya usimamizi wa Jamii ambapo Kati ya hivyo Vituo 20 vipo katika Halmashauri ya Jiji la Tanga na 10 vipo Wilaya ya Korogwe " Alisisitiza Hope

Alisema Wasichana zaidi ya 1161 walipatiwa Mafunzo ya kuanzisha Biashara ndogo pamoja na Mitaji kupitia SIDO,VETA na Ustawi wa Jamii,

"Zaidi ya asilimia 65 ya Wasichana hususani katika Halmashauri ya Jiji la Tanga Wanajishughulisha na shughuli za kujiongezea kipato na kubadili mfumo wao wa Maisha ya awali kabla ya kupata Elimu " Alisisitiza Hope

Aliongeza kuwa Wasichana 10 wa wamefanikiwa kujiunga na Chuo kikuu kwa kozi za Shahada ya Kwanza huku Wasichana 22 Walioko kwenye Rika Balehe Wamehitimu ngazi ya Cheti kutoka Chuo Cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Kampasi ya Tanga Wakati,


"Wasichana wengine 3 waliandikishwa katika Vyuo mbalimbali vikiwamo chuo Cha maji,chuo Cha Taifa Cha Zanzibar na Chuo Cha Usimamizi wa Fedha, Watoto 1670 wa miaka 3-5 walipata Elimu ya Makuzi ,Malezi na Maendeleo ya awali, nafasi za kazi zaidi ya 450, Ujenzi wa Madara mapya 22 na Ukarabati wa madarasa 13 pamoja na Walimu 41 wa Elimu ya Awali kutoka Shule za Serikali walipatiwa Mafunzo juu ya Mtaala wa Elimu ya Awali pamoja na kutoa Vifaa vya kufundishia" Alisisitiza Hope

PSSSF TAYARI IMEWALIPA WANACHAMA 750 WALIOKUMBWA KWENYE SAKATA LA VYETI FEKI

December 02, 2022

 NA MWANDISHI WETU, ARUSHA.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) tayari umewalipa wanachama 750 waliokumbwa na sakata la vyeti “feki”, baada ya kuwasilisha madai yao na nyaraka stahiki.

Akizungumza wakati wa kikao kazi na wanachama wapatao 60 wa klabu ya waandishi wa habari jiji la Arusha kwenye ukumbi wa Kituo Cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) leo Ijumaa Desemba 2, 2022, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama PSSSF, Bw. James Mlowe amesema, zoezi la kuwalipa lilianza Novemba 1, 2022 na ni endelevu.

“Zoezi linaendelea vizuri, Wanachama waliopo katika orodha ya serikali na PSSSF  ni 9,771 ambao wanadai malipo ya takribani shilingi bilioni 22.22.” Alifafanua. 

Akizungumzia madhumuni ya kikao hicho na wanachama wa klabu hiyo ya waandishi wa habari jijini Arusha wapatao 60,  Bw. Mlowe alisema “lengo ni kutoa ufafanuzi juu ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko pamoja na kuendeleza uhusiano mzuri ukiopo kati ya Mfuko na wanahabari wa Arusha”.

Mambo mengine aliyozungumzia Bw. Mlowe ni pamoja na Malipo ya Mafao na Pensheni, Uwekezaji, Thamani ya Mfuko pamoja na mafanikio ambayo PSSSF imeyapata tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018 baada ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSPF, PPF,LAPF na GEPF.

“ Kila mwezi PSSSF inaingiza kwenye mzunguko zaidi ya shilingi bilioni 180 ikijumuisha malipo ya pensheni ya mwezi zaidi ya shilingi bilioni 60 zinazolipwa kwa wastaafu 158,000 pamoja na Mafao mengine zaidi ya shilingi bilioni 120,” alibainisha.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanachama wa klabu hiyo, Katibu wa klabu hiyo, Bw. Seif alisema wanashukuru kwa fursa hii na wameweza kufahamu kwa undani juu ya PSSSF na utekelezaji wa majukumu yake na sasa wanaweza kutoa taarifa sahihi na muhimu kwa wadau wa PSSSF.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama PSSSF, Bw. James Mlowe(kulia), akizungumza kwenye kikao hicho, kushoto ni Kaimu Meneja wa Klabu ya Waandishi wa Habari Kanda ya Kaskazini, Bw. Baraka Kitundu.
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama PSSSF, Bw. James Mlowe(kulia), akizungumza kwenye kikao hicho.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho.
Bi. Hilda Kileo, akizungumza kwenye kikao hicho.
Bw.Allan Kileo akizungumza kwenye kikao hicho.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho.


. KHALFAN S. 0716745281

AFRIKA YAKUTANA KUJADILI HATMA YA PUNDA

December 02, 2022
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) na baadhi ya Viongozi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) na Shirika la Umoja wa nchi za Afrika linaloshughulika na tafiti na haki za wanyama (AU-IBAR) wakifurahia jambo muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano uliokuwa ukijadili hatma ya wanyama aina ya Punda uliofanyika leo (01.12.2022) jijini Dar-es-salaam.
Mkurugenzi wa Mtandao wa kutetea haki za wanyama kutoka Kenya Bw. Josphat Ngonyo akiwaeleza Waziri wa Mifugo na Uzalishaji wa wanyama kutoka Chad Dkt. Abderahim Awat (kushoto) na  Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kushoto) namna wanyama aina ya Punda wanavyotumika nchini kwake  muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano uliokuwa ukijadili hatma ya wanyama aina ya Punda uliofanyika leo (01.12.2022) jijini Dar-es-salaam. Wa pili kutoka kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na Vuongozi na watendaji kutoka zaidi ya mataifa 20 wanachama wa Umoja wa Afrika na watendaji kutoka Shirika la Umoja wa nchi za Afrika linaloshughulika na tafiti na haki za wanyama (AU-IBAR) na Shirika linaloshughulikia haki za wanyama kazi (Brooke East Africa) wakati wa Mkutano uliokuwa ukijadili hatma ya wanyama aina ya Punda uliofanyika leo (01.12.2022) jijini Dar-es-salaam.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameziongoza nchi zaidi ya 20 wanachama wa Umoja wa  Afrika ambazo zimekutana leo (01.12.2022) jijini Dar-es-salaam kwa ajili ya kujadili hata ya wanyama aina ya punda wanaodaiwa kuwa kwenye hatari ya kutoweka.

Akizungumza katika Mkutano huo Mhe. Ulega amewataka wataalam kutoka katika nchi hizo kujadili kwa kina na kutoa mapendekezo ya kitafiti na kisayansi kuhusu njia zinazoweza kutumika kuwaokoa wanyama hao na kuziwasilisha ili zijumuishwe  katika sera na kanuni  kwa ajili ya utekelezaji.

“Kama tulivyofanikiwa katika kupiga vita biashara nyingine ambazo zilikuwa zikitupelekea kwenye kupoteza wanyama wetu basi mtafakari kama wataalam na kuja na tafiti za kisayansi zitakazotushawishi sisi watunga sera ili tuweke mkazo wa kupiga marufuku kama tulivyoweka kwa upande wa biashara ya meno ya Tembo” Amesisitiza Mhe. Ulega

Aidha Mhe Ulega amependekeza wanyama aina ya punda kujumuishwa kwenye kundi la viumbe waliopo hatarini kutoweka ili kuongeza nguvu ya jitihada zinazofanywa kwa ajili ya kuokoa hatma yao ambapo amesema kuwa hatua hiyo itafufua jitihada za kuongeza idadi ya wanyama hao.

“Lakini pia wakati mkijadili mnapaswa kujua kuwa pamoja na umuhimu wake kule vijijini wananchi wanashawishiwa kuuza punda wao kwa sababu ya umasikini hivyo wakati tunafikiria namna ya kudhibiti hali hii ya utowekaji wa Punda tufikirie namna ya kuwaelimisha na kuangalia njia mbadala kwa wanakijiji hao ili wasiwauze”Ameongeza Mhe. Ulega.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Sekta ya Mifugo Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa msisitizo mkubwa wa Tanzania katika mkutano huo ni kuueleza ulimwengu kuhusu hatua walizochukua katika kudhibiti hali ya kutoweka kwa punda ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku uuzwaji na uchinjwaji wa wanyama hao.

“Lakini jambo jingine tumeiambia dunia kuwa sisi kupitia mfumo wetu wa Sera tumeamua kulinda wanyama hawa kupitia eneo la ustawi wa wanyama lililopo kwenye mabadiliko ya sera ya Mifugo ya mwaka huu ambayo yanaendelea kufanyika” Amesema Nzunda.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa nchi za Afrika linaloshughulika na tafiti na haki za wanyama (AU-IBAR) Dkt. Nick Nwankpa amesema kuwa katika nchi zote za Afrika wanyama aina ya Punda wamekuwa na msaada mkubwa kwa jamii ikiwa ni pamoja na kusaidia katika shughuli zote za kiuchumi.

“Lakini pamoja na msaada huo, Punda wamekuwa wakichukuliwa kama wanyama kazi tu ambao wamesahaulika hata kwenye sera na kanuni mbalimbali zinazolinda haki za wanyama na kadri idadi kubwa ya watu inavyoongezeka ndipo idadi ya punda inavyopungua” Amesema Dkt. Nwakpa.

Akielezea sababu za kufanyika kwa mkutano huo nchini Tanzania Mwenyekiti wa Shirika linaloshughulikia haki za wanyama kazi (Brooke East Africa) Bw. Erick Kimani amesema kuwa hatua hiyo imetokana nchi hiyo kuwa ya kwanza kupiga marufuku biashara ya Punda ambapo amezitaka nchi nyingine za Afrika kuchukua hatua hiyo ili kuondoa hatari ya kutoweka kwa wanyama hao.

Mkutano huo unaofanyika kwa siku mbili jijini Dar-es-salaam umelenga kujadili kwa kina umuhimu wa wanyama aina ya punda kiuchumi na kijamii na unatarajia kuwa na maazimio yatakayosaidia kuwaondoa wanyama hao kwenye hatari ya kutoweka.

 

WAZIRI MKUU MGENI RASMI MKUTANO WADAU WA MKONGE

WAZIRI MKUU MGENI RASMI MKUTANO WADAU WA MKONGE

December 02, 2022

 



Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa Tatu wa Wadau wa Mkonge utakaofanyika Desemba 4, mwaka huu jijini Tanga.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona katika taarifa iliyotolewa kwa umma na Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa bodi hiyo Esther Mbusi, mkutano huo utawakutanisha viongozi mbalimbali wa kitaifa na Wadau wa Sekta ya Mkonge nchini.

“Napenda kuwakaribisha wakazi wa Tanga na maeneo jirani kuhudhuria kwenye Mkutano huo mkubwa wa Wadau wa Sekta ya Mkonge unaofanyika kwa mujibu wa Sheria ya Na. 2 ya Sekta ya Mkonge ya Mwaka 1997.  
 
“Katika mkutano huo tunatarajia Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, lakini viongozi wengine watakaokuwepo kwenye ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde ambaye atamwakilisha Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, viongozi wote wa Mkoa, Waheshimiwa Wabunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa jirani hususani ile inayolima Mkonge.
 
“Kama mnavyofahamu, Waziri Mkuu amekuwa mstari wa mbele na ameshika bendera ya kuhamasisha Kilimo cha Mkonge, tulianza naye tangu mwaka 2019 hadi mwaka 2021 amekuwa akija Tanga kuhimiza watu waingie kwenye Kilimo cha Mkonge kwa sababu anafahamu faida za Mkonge zao ambalo linaweza kubadilisha maisha ya Watanzania kwa muda mfupi sana, zao la kudumu la uhakika na biashara ya Mkonge ni nzuri,” amesema Kambona kwenye taarifa hiyo. 

Kambona amesema mkutano huo pia ni fursa kwa Wanatanga kibiashara kwani kutakuwa na wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali nchini ambao watahudhuria mkutano huo muhimu kwa maendeleo ya Sekta ya Mkonge nchini.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo utatanguliwa na Mkutano wa Bodi ya Wakurugenzi Desemba 2, na Kikao cha Kamati Ndogo ya Maendeleo ya Zao la Mkonge inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima na Mwenyekiti Mwenza, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigella utakaofanyika Desemba 3, wilayani Korogwe jijini Tanga. Kauli mbiu ya mkutano huo ni; ‘Mkonge ni biashara, wekeza sasa.’

TRA TANGA WAADHIMISHI SIKU YA SHUKRANI KWA KUWAKATIA BIMA YA AFYA WATOTO 25

November 26, 2022
 Kaimu Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Tanga Bombo Opra Msuya kulia akisisitiza jambo kwa Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Specioza Owure wakati walipowatembelea wakati wakiadhimisha sherehe za shukrani  ambapo walitembelea wodi ya watoto kwenye Hospitali ya Mkoa wa Tanga Bombo kugawa misaada mbalimbali ikiwemo kuhaidi kutoa fedha za matibabu za wagonjwa wawili kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.


Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Specioza Owure kulia akimkabidhi mmoja msaada ya vitu mbalimbali Kaimu Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Tanga Bombo Opra Msuya

Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Specioza Owure akizngumza mara baada ya kukabidhi msaada huo







Na Oscar Assenga,TANGA.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga imeadhimisha sherehe za shukrani  kwa kuwatembelea wodi ya watoto kwenye Hospitali ya Mkoa wa Tanga Bombo kugawa misaada mbalimbali ikiwemo kuhaidi kutoa fedha za matibabu za wagonjwa wawili kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

Ugawaji wa msaada huo wenye thamani ya Milioni 3.5 ulitolewa katika wodi ya watoto katika halfa iliongozwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Specioza Owure akiwa ameambatana na maafisa mbalimbali wa mamlaka hiyo na watumishi.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo kwa uongozi wa Hospitali hiyo Meneja Specioza alisema kwamba wao katika kuadhimisha wiki ya shukrani kwa mteja waliona watoe shukrani kwa walipa kodi wao kwa kuwapatia msaada huo.

Alisema kwamba walishakutana na wafanyabiashara wao na kwamba katika kipindi hiki wamekuwa na utaratibu wa kuwambuka jamii inayowazunguka hivyo wameona kutembelea hospitali ya mkoa wa Tanga Bombo kutembelea wodi ya watoto.

Meneja huyo alisema kwamba wametoa shukrani kwa jamii kutokana na kwamba wamaani jamii ikiwa imara na afya bora na kodi itaongezeka maana wanapokuwa na afya ndipo wana pata nguvu za kufanya biashara na kulipa kodi stahiki.

“Tumeona tuje tuwaone watoto tujue matatizo yao na tunalengo la kuwakatia bima ya afya watoto 25 kwa sababu kuna watoto wengi wanahitaji bima lakini wakati tunaendelea na watoto wao tumetembelea pia wodi ya watu wazima tukakutana na wagonjwa wawili.

Alieleza kwamba wagonjwa hao walikuwa wanahitaji msaada wa kufanyiwa upasuaji ambao ni Frank na Mzee Hamisi na hivyo watatoa fedha kuwasaidia waweze kuwafanyiwa upasuaji ikiwa ni kusheherekea sherehe ya kuwashukuru walipa kodi na jamii kwa ujumla.

Awali akizungumza wakati akipokea msaada huo. Kaimu Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Tanga Bombo Opra Msuya aliwashukuru Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga kwa kuwapatia msaada huo wagonjwa hasa kwa ajili ya wenzao wenye uhitaji mungu awabariki wanawaomba wasiiishie hapo waendelee kujitolea.

Hata hivyo kwa upande wake mmoja wa wagonjwa ambaye alipatiwa msaada wa kufanyiwa upasuaji Frank Beda anayetokoea wilayani Muheza aliyegongwa na aliyehusika na tukio hilo alikimbia aliwashukuru TRA kwa kuwapatia msaada huo na kwamba mwenyezi mungu awabariki sana katika maisha yao

Mwisho.