Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiongea na Wakurugenzi wa
Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji na
kuwaagiza kuweka alama za x na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika
miji yao bila kibali na yale yanayojengwa katika viwanja vya watu
wengine walio na hati za kumiliki ardhi kwa dhuruma.
Baadhi ya viongozi, Wakurugenzi
wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji wa
mkoani Rukwa wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi.
Baadhi ya viongozi, Wakurugenzi
wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji wa
mkoani Rukwa wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi
Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
Kamishna Mstaafu Zelote Stephen wakati walipoenda kutatua mgogoro wa
ardhi wa shamba la mifugo la Malonje wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa
lenye ukubwa wa ekari 12,750, ambapo ameagiza eneo hilo lirejeshwe
serikalini.
…………………………………………………………………………
Na. Hassan Mabuye
Serikali imewaagiza Wakurugenzi
wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji
kuweka alama za x na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika miji yao
bila kibali na yale yanayojengwa katika viwanja vya watu wengine walio
na hati miliki zao za ardhi kwa dhuruma.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameyasema hayo alipofanya ziara
wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa alipoenda kutatua mgogoro wa ardhi
ambapo ameagiza eneo ya lililokuwa shamba la mifugo la Malonje wilayani
Sumbawanga mkoani Rukwa lenye ukubwa wa ekari 12,750, lirejeshwe
serikalini kwa vile utaratibu wa kuligawa umekiukwa kwa kiwango kikubwa,
na masharti ya uendeshaji hayajazingatiwa kabisa.
Waziri Lukuvi amesema tatizo la
ujenzi holela lianaanza pale ambapo Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa
Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji wanawaacha majengo
yanaibuka katika miji yao bila kujua ujenzi huo una kibali au unajengwa
katika kiwanja chenye hati na muhusika wa hati hiyo ndio anayejenga.
“Hatuwezi kuendelea na zoezi la
kufanya urasimishaji wa makazi kila siku wakati chanzo cha tatizo hilo
kinajulikana, kwa hiyo naagiza Wakurugenzi, Maafisa Ardhi, Maafisa
Ujenzi na Maafisa Mipangomiji kuweka x katika majengo yote yanayojengwa
bila vibali na ujenzi unaofanywa kwenye viwanja vya watu masikini kwa
dhuruma” amesema Lukuvi.
Lukuvi amesema atapambana na
viongozi hao pale ambapo atakuta majengo yamekithiri katika miji yao na
hayana vibali vya ujenzi na baya zaidi majengo hayo yamejengwa katika
maeneo ambayo hayaruhusiwi kujenga au yamejengwa katika kiwanja cha mtu
mwingine na viongozi hao wameshindwa kufuatilia kwa kuyavunja au
kuyaweka alama ya x majengo hayo, kwa kuwa huu ni uzembe unaotokea nchi
nzima.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna
Mstaafu Zelote Stephen amemhakikishia Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kuwa atayafanyia kazi
mapendekezo yake kikamilifu na kwa haraka ili kuondoa migogoro na kero
zinazoukabili mkoa wake katika masuala yote ya ardhi.
Aidha, katika hatua nyingine
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi
amesema Serikali imekusudia kuwanyang’anya mashamba watu wote
waliokopeshwa kwa kuyatumia kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo
kutoka kwenye mabenki ndani na nje ya nchi lakini mikopo hiyo hawaitumii
kuinufaisha nchi wala kuiendeleza ardhi waliyoitumia kama dhamana.
Waziri Lukuvi ameongeza kuwa
kumekuwa na changamoto kubwa ya wawekezaji wengi wenye mashamba makubwa
kutumia ardhi kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye
mabenki ndani na nje ya nchi lakini mikopo hiyo wanaitumia kuwekeza nje
ya nchi na kujenga majengo nchi za Ulaya, dubai na kwingine duniani.
Lukuvi amesema Haiwezekani mtu
atumie ardhi yetu kujipatia fedha halafu fedha hizo azitumie kuendeleza
nchi nyingine na kuiacha ardhi yetu kama pori jambo ambalo linaleta
migogoro mikubwa katika jamii inayoyazunguka maeneo hayo.
“Kwa hiyo Wizara yangu imekusudia
mwezi ujao kupeleka Bungeni marekebisho ya sheria namba 24 ya mwaka
1999 ili kuongeza vifungu ambavyo vitadhibiti mikopo inayopatikana kwa
kutumia ardhi kama dhamana” amesema Waziri Lukuvi.
Marekebisho haya tunalenga
kuwezesha fedha zinazopatikana kutokana na mikopo iliyotolewa itumike
kuendeleza sehemu ya ardhi husika iliyotumika kama dhamana ya kuomba
mkopo katika mabenki. Kwa kuwa Tathmini iliyopo inaonesha, baada ya
wekezaji hao kupata mikopo kwa kutumia ardhi kama dhamana fedha hizo
hawazitumii kuendeleza ardhi husika au katika uwekezaji wowote hapa
nchini.
Lukuvi amesema, kuanzia mwezi
Novemba tatizo hilo litakwisha kabisa kwa kuwa jukumu hili yatapewa
mabenki na wakopeshaji wote ambao watafuatilia kwa karibu maombi ya
mikopo kutokana na mpango mkakati uliowasilishwa katika Benki husika.
“na kama Benki husika
haitowafuatilia na kuamua kumuachia mtu huyo kwa kuwekeza fedha hizo
anavyotaka bila kuendeleza ardhi husika, basi Serikali itamyang’anya
mkopeshwaji huyo shamba hilo kwa kuwa atakua amekiuka sheria halafu
Benki ambayo itamuachia mtu achukue fedha na asiendeleza shamba lile
itakuwa imekula hasara yenyewe” amesema Waziri Lukuvi.
EmoticonEmoticon